IGP Sirro apangua makamanda wa Polisi

Muktasari:

  • Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko madogo ya makamanda wa Polisi wa mikoa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa jeshi hilo.


Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko madogo ya makamanda wa Polisi wa mikoa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa jeshi hilo.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 3, 2022 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Wankyo Nyigesa amehamishwa kutoka mkoa wa Pwani kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera.

“Kamanda Nyigesa amechukua nafasi ya aliyekuwa Kamanda wa mkoa huo, Awadhi Juma Haji ambaye Januari 31, 2022 alipandishwa cheo kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na pia kuteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Pius Lutumo ambaye alikuwa Operesheni Ofisa wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni amehamishwa kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani.