Ijumaa Kuu fursa ya kuondoa chuki, uonevu na ukatili
Muktasari:
- Waumini wamehimizwa kuishi kwa unyenyekevu, kushirikiana kwa amani, kuacha uonevu na kuchagua mema. Siku hiyo imetajwa chachu ya msamaha, uvumilivu na matumaini, ikiwakumbusha Watanzania thamani ya mateso ya Yesu Kristo, kifo chake na ufufuko wake kama msingi wa maisha mapya.
Dar/Mikoani. Waumini wa dini ya Kikristo nchini wameshiriki ibada ya Ijumaa Kuu katika makanisa mbalimbali, wakitafakari mateso na kifo cha Yesu Kristo msalabani, huku viongozi wakihubiri ujumbe wa matumaini, msamaha na mabadiliko ya kiroho katika maisha ya kila siku.
Ibada hiyo, inayosherehekewa kama siku ya huzuni na maombolezo, pia imekuwa fursa kwa viongozi wa kidini kuhimiza waumini kutojihusisha na vitendo vya uonevu, ukatili wa kijinsia, usaliti na tabia za kiburi zinazoharibu jamii.
Huko Arusha, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoa wa Arusha (Ukama), Askofu Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, ametoa wito kwa Watanzania kuadhimisha Ijumaa Kuu kwa kuchagua mema, kusamehe na kuacha chuki, ujinga na ujeuri.
“Kutokana na majeraha ya kisiasa, kijamii na kibiashara, Taifa letu linahitaji msamaha. Kusamehe ni kufunguliwa, si aibu na ni hatua ya kweli ya kupona,” amesema Askofu Hotay.
Askofu wa Jimbo katoliki la Shinyanga Liberatus Sangu akizungumza wakati wa tafakari ya mateso ya Bwana Yesu kristo katika parokia ya Kitangili iliyopo Manispaa ya Shinyanga.
Huku akihimiza waumini kutoacha kuombea na kusamehe, Askofu Hotay amesisitiza kuwa msamaha ni msingi wa mshikamano wa kijamii, ikiwemo kwa wale waliokosewa au walioteswa kihalali.
Ameongeza kuwa ibada ya Ijumaa Kuu inafundisha kuishi kwa unyenyekevu na upendo, kuondoa mateso na uonevu kwa watu wasiokuwa na hatia.
Mkoani Geita, Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala, amewataka Wakristo kujitenga na usaliti na kuishi kwa unyenyekevu na upendo, ili kuondoa mateso na uonevu kwa wasiokuwa na hatia.
Akitoa mahubiri ya Ijumaa Kuu katika Parokia ya Bikra Maria wa Fatima, Askofu Kassala alitaja mifano ya kihistoria na ya sasa, akisisitiza kuwa chuki, wivu na ukosefu wa unyenyekevu vinachangia watu kutumikia vifungo bila kusikilizwa kwa makosa yao.
Kuhusiana na masuala ya kisiasa na uchumi, amesema ukosefu wa unyenyekevu na kutumia nguvu kupita kiasi kunasababisha machafuko, vita na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Mkoani Shinyanga, Askofu wa Jimbo Katoliki, Liberatus Sangu, amesisitiza umuhimu wa uvumilivu na kujitoa sadaka kwa vijana, huku akionya dhidi ya kutafuta mali au utajiri wa haraka na michezo ya kubeti.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoa wa Arusha (Ukama), Askofu Stanley Hotay,akihubiri leo Ijumaa Aprili 3 2026, katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika Viwanja vya Kanisa la Jimbo Kuu Katoliki, St Theresa Arusha.
“Tuwe na moyo wa sadaka na tusikate tamaa; mateso ni sehemu ya maisha, kama Yesu Kristo alivyoitumia kama njia ya kuleta uzima wa milele,” amesema Askofu Sangu.
Pia, ametoa wito kwa vijana kutafuta mali zao wenyewe ili kuondoa migogoro ya urithi ndani ya familia.
Jijini Dar es Salaam, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limepinga vikali adhabu ya kifo, likisisitiza kuwa hakuna ushahidi kwamba adhabu hiyo inapunguza uhalifu badala yake inakiuka mafundisho ya Biblia.
Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Chediel Lwiza, amesema:
“Kifo cha Yesu Kristo msalabani kilifanyika kwa mpango wa Mungu na kama binadamu asingeweza kufufuka, hakuna adhabu ya kifo inayoweza kurekebisha dhambi.
Waumini wa kanisa la KKKT Azan Front,wakiwa katika ibada ya Ijumaa Kuu, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga
Na sisi kwa upande wetu wa Tanzania bado kanisa halikubali na linapinga adhabu ya kifo, iwe ni kunyongwa, kupigwa risasi, adhabu yoyote ya kifo kanisa halikubali na linapinga,” amesema.
Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay, Padri Batholomew Mroso, amesisitiza kuwa maisha ya Kikristo yanapaswa kuigwa kupitia mateso ya Kristo.
“Kristo aliteswa; binadamu hapaswi kuhusika na mateso ya wengine. Upendo na huruma ni wajibu wa kila mwamini,” amesema.
Padri huyo amesema hata kama Kristo aliteswa, binadamu hapaswi kuhusika na mateso ya watu wengine.
Kutoka mkoani Tanga, Mchungaji Yohana Kakoa amehimiza waumini kutafakari mateso ya Kristo katika maisha yao ya kila siku, akisisitiza kwamba hakuna ukombozi wa mwanadamu bila kifo cha Yesu.
Amesema mateso ya Yesu si tukio la kihistoria tu, bali wito wa mabadiliko ya ndani kwa kila mwamini, na kwamba kuishi kwa upendo, amani na heshima ni mwendelezo wa upendo wa Mungu.
Aidha, alikemea vikali ongezeko la ukatili wa kijinsia, akieleza kuwa linatokana na baadhi ya watu kushindwa kuelewa neema ya Mungu.
Amewataka wananchi kuacha vitendo hivyo na kuishi kwa misingi ya upendo, amani na kuheshimiana.
Kutoka Mirerani, mkoani Manyara, Padri Aristarki Tarimo amewataka Wakristo kuenzi ndoa zao, kuepuka ushirikina na kujenga maisha yenye maadili mema.
“Maisha ya suria hayafai kwa Kikristo. Tafuteni baraka za ndoa zenu, na msiingie katika dhambi ya ushirikina ili kupata mali au mchumba,” amesema.
Amesema Wakristo wasiishi kwa mazoea majumbani mwao na wanawake wao bila kufunga ndoa, kwani fursa ya kubariki ndoa zao wanazo pindi wakiamua.
“Maisha ya suria siyo vyema kwa Wakristo, hivyo wanaoishi na wanawake bila kufunga ndoa badilikeni na kufunga ndoa kwani nafasi na fursa mnazo,” amesema Padri Tarimo.
Huko Dodoma, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki, Beatus Kinyaia, amewataka watumishi na viongozi wanaostaafu kukaa kimya na kuacha kuingilia utendaji wa waliopewa nafasi.
Ameeleza kuwa baadhi ya watu wananyimwa haki kwa sababu ya hofu ya wengine, na kwamba usaliti wa viongozi unaongeza migogoro ndani ya jamii.
“Hata Pilato alijua Yesu hakuwa na hatia, lakini hakuweza kuamua kwa sababu ya hofu. Hivyo ni muhimu waumini kutenda haki bila hofu na kiburi.
Niwaombe sana viongozi mnaostaafu iwe kwenye makanisa au hata utumishi mwingine, rudini nyumbani mkalee wajukuu, nataka mkae kimya, acheni kabisa waliopewa nafasi watende kazi yao bila hofu,” amesema Askofu Kinyaia.
Kiongozi huyo wa kiroho amezungumzia suala la haki akisema baadhi ya watu wanakosa haki zao kwa sababu ya hofu kutoka kwa wengine ambao wanaogopa kutoa haki.
Imeandikwa na Janeth Mushi (Arusha), Hellen Mdinda (Shinyanga), Geofrey Chubwa (Geita), Nasra Abdallah na Baraka Loshilaa (Dar es Salaam), Mbonea Herman (Tanga), Joseph Lyimo (Manyara) na Habel Chidawali (Dodoma).