Ilemela yakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, yabakiza Sh190 milioni

Muktasari:
- Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Modest Apolinary amesema manispaa hiyo ilipokea Sh1.94 bilioni za Uviko-19 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo na baada ya ujenzi wamebakisha Sh190 milioni.
Mwanza. Mbali na halmashauri nyingi nchini kufurahi baada ya kuongezewa muda wa kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye mradi wa Uviko-19, hali ni tofauti kwa manispaa ya Ilemela jijini hapa, baada ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 97 ndani ya siku 45.
Awali, manispaa hiyo iliyoko mkoani Mwanza ilikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza 114 ambapo 97 kati yake vimejengwa kupitia mradi wa Uviko-19 na 16 vilijengwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya manispaa hiyo.
Akizungumza leo katika hafla ya kukabidhi madarasa hayo kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Modest Apolinary amesema manispaa hiyo ilipokea Sh1.94 bilioni za Uviko-19 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo.
Apolinary amesema usimamizi mzuri na ufuatiliaji ulisaidia fedha hiyo kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo kwa wakati huku Sh190 milioni ikisalia kama chenji.
"Vyumba hivi vimewekewa viti na madawati 4,850 ili kuhakikisha kwamba hakuna mwanafunzi atakayejiunga kusoma masomo ya kidato cha kwanza akiwa anakaa chini," amesema Apolinary
Ameongeza kwamba kutoka na fedha hiyo kusalia, Manispaa ilitumia Sh176 kujenga ofisi ndogo za walimu 28 katika shule 25 za manispaa hiyo.
"Baada ya kujenga Ofisi ndogo za walimu tumesaliwa fedha taslimu Sh6 milioni na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh18 milioni," amesema
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel ameipongeza manispaa hiyo kwa kukamilisha nradi huo kwa wakati huku akitoa wito kwa halmashauri zilizobaki kufanya hivyo.
"Ilemela mmekuwa vinara kwa mkoa wetu, nitoe wito kwa halmashauri ambazo bado hazijakamikisha ujenzi huu kujifunza kwenu na kupata uzoefu na jinsi gani mlifanya kukamilisha ujenzi huu kwa kwa wakati," amesema Gabriel