Intaneti ya bure Mlima Kilimanjaro

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), John Yahaya akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika kampeni ya 'twenzetu kileleni 2023' msimu wa tatu, uliofanyika katika  Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Zaidi ya Watanzania 200 wanaopanda mlima Kilimanjaro kuelekea siku ya maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika, watagharamiwa huduma za mawasiliano ya intaneti bure na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ili kutambua mchango wao katika maadhimisho hayo.

Moshi. Zaidi ya Watanzania 200 wanaopanda Mlima Kilimanjaro kuelekea siku ya maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika, watagharamiwa huduma za mawasiliano ya intaneti bure na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ili kutambua mchango wao katika maadhimisho hayo.

Hayo yamesemwa jana, Desemba 4, 2023 na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, John Yahaya wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Kampeni ya 'Twenzetu Kileleni 2023' msimu wa tatu, ambao umefanyika katika Hoteli ya Springs Land, Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa tukio hilo, shirika hilo limelenga kutoa huduma za mawasiliano bure ili kutoa nafasi kwa washiriki kuwa na mawasiliano kipindi chote wakiwa katika zoezi la kupanda mlima na kutoa fursa ya washirki kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki kupitia mitandao ya kijamii.

"Washiriki wote watakaopanda Mlima Kilimanjaro, katika kipindi hiki cha Kampeni ya 'Twenzetu Kileleni', watapata fursa hiyo ya intaneti bure wafikapo kila kituo katika mlima huo, ili kutambua umuhimu wa maadhimisho haya ya miaka 62 ya uhuru wa nchi yetu," amesema.

"Tukio hili linaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya nchi yetu, katika kukuza sekta ya utalii sambamba na kuimarisha mawasiliano nchini," amesema.

Amesema, shirika hilo limeendelea kutekeleza mkakati wake wa kuimarisha mawasiliano nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna kuwepo na miundombinu ya kisasa na yenye uwezo mkubwa katika kutoa huduma ndani na nje ya Tanzania.

"Uwepo wa huduma hii ya intaneti, itakuwa ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi ya mlima wetu, ndani na nje ya nchi yetu, lakini itahamasisha Watanzania kujenga mazoea ya kutembelea vivutio vya mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ya utalii," amesema.

Pamoja na mambo mengine, amesema uwepo wa mawasiliano ya intaneti katika vivutio vya utalii nchini, itasaidia kuweka mazingira mazuri ya watalii kuwa na mawasiliano yenye uhakika wawapo katika shughuli za utalii.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Jenerali Mstaafu, George Waitara amewataka Watanzania kuendelea kuutangaza mlima huo kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika.

"Nafurahi kila mwaka kuona mwitikio mkubwa wa watu wakipanda mlima Kilimanjaro ukiongezeka na mwaka huu nimeambiwa watu zaidi ya 200 wanapanda mlima kuelekea kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wetu, hii ni hatua kubwa na watu wameitikia," amesema.

"Tusiachie watu wa nje kuja kututangazia mlima wetu, ni jukumu letu sisi wenyewe kuutangaza mlima huu, sisi wenyewe Watanzania tufanye kazi hiyo, sasahivi kumefanyika maboresho makubwa na huduma zote muhimu zinapatikana  kwa wanaopanda mlima Kilimanjaro na huduma za mawasiliano zimeboreshwa huko."

Amewataka wale wanaopanda mlima, kuhakikisha wanafuata taratibu na  maelekezo yote  wanayopewa wakati wa kupanda mlima kwa kuwa mlima hauzoeleki.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Makampuni ya Utalii ya Zara Tours, Ibrahim Othman Jama amesema idadi ya wanaopanda mlima kupitia Kampeni ya 'Twenzetu Kileleni 2023' kutakuwepo na idadi ya watu zaidi ya 200 kutoka katika mashirika, taasisi mbalimbali na watu binafsi.

"Tunalishukuru Shirika la TTCL kwa kutoa huduma za mawasiliano katika mlima Kilimanjaro, hii ni kazi kubwa ambayo imefanyika kwa kuwa itarahisisha huduma za mawasiliano kule mlimani na sisi tutahakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa nzuri," amesema.

"Tunamshukuru Rais Samia kwa kupitia  filamu yake ya  "The Royal Tour" ambayo imeweza kuleta matunda mengi kwa kutangaza vivutio vyetu vilivyopo hapa nchini ambapo kwa sasa tunaona idadi kubwa ya watalii imeongezeka hapa nchini," amesema.