Jafo aunda timu kuchunguza mabadiliko mto Mara

Muktasari:

  • Serikali imetangaza kuunda timu maalum itakayochunguza chanzo cha mabadiliko katika mto Mara yaliyopelekea maji kubadilika kuwa meusi huku viumbe hai wakiwepo samaki kufa.

Musoma. Serikali imetangaza kuunda timu maalum itakayochunguza chanzo cha mabadiliko katika mto Mara yaliyopelekea maji kubadilika kuwa meusi huku viumbe hai wakiwepo samaki kufa.

Akizungumza baada ya kufika katika mto huo kujionea hali halisi leo Jumamosi Machi 12, 2022, Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo amesema kuwa timu hiyo ya ataiunda leo ili ianze kufanya kazi mara moja.

"Nimejionea mwenyewe hali si shwari hapa kwa sababu harufu iliyopo hapa sio ile ninayoikuta kila nikija Mara kwa hiyo lazima Serikali ifanye jambo tena kwa haraka ili tupate majawabu nini chanzo na kipi kifanyike kabla watu hawajaathirika," amesema Jafo. 

Amesema kuwa katika timu hiyo anayokwenda kuunda hivi punde kutakuwepo na wataalam mbalimbali wakiwepo wataalam wa miamba na kemikali ambao watatakiwa kujua kama mabadiliko hayo yamesababishwa na kemikali au miamba.

Awali, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Mazingira (Nemc), Redempta Samuel amesema kuwa timu ya wataalam ilifika katika eneo la mto huo tangu Machi 10, 2022 kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Amesema kuwa hadi sasa wamekwishachukua sampuli 32 kutoka katika maeneo mbalimbali ya mto huo sambamba na ziwa Victoria na kwamba uchunguzi unaendelea kujua tatizo ni nini.

Katika hatua nyingine waziri Jaffo ameshindwa kuingia ndani ya mto huo kama ilivyokuwa imepangwa awali baada ya eneo la mto katika upande wa pili wa daraja la Kirumi kuzingirwa na kujaa magugu maji yaliyofika katika eneo hilo muda mfupi baada ya waziri kuwasili katika eneo hilo.