Jaji achambua ushahidi uliowatia hatiani kina Mbowe-8
Muktasari:
- Jana katika mfululizo wa kesi hii ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tuliona jinsi Mahakama Kuu ilivyohitimisha hoja ya uhalali wa hukumu, iliyowatia hatiani wanachama hao.
Jana katika mfululizo wa kesi hii ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tuliona jinsi Mahakama Kuu ilivyohitimisha hoja ya uhalali wa hukumu, iliyowatia hatiani wanachama hao.
Baada ya kuiweka katika mizania ya kisheria ya usahihi wake, Jaji Ilvin Mugeta aliyesikiliza rufaa ya viongozi hao aliridhika kuwa kimuundo hukumu ilikuwa imekidhi matakwa ya kisheria.
Hata hivyo, alisema kimaudhui hukumu hiyo haikuwa ikijitosheleza au ilikuwa na upungufu katika namna ya uchambuzi na uamuzi wa mambo kwa mujibu wa ushahidi kuhusiana na kila kosa waliloshtakiwa nalo. Endelea.
Mahakama Kuu baada ya kuhitimisha kwa kueleza hukumu ya Mahakama ya Kisutu ilikuwa na kasoro za kisheria katika upande wa maudhui, ilikubaliana na hoja za wakili Peter Kibatala kuwa haikufanya uchambuzi wa ushahidi kuhusiana na kila kosa, swali lililofuata ilikuwa ni nafuu au hatua zipi sasa izichukue.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, pamoja na sababu za rufaa, wakili wa warufani hao aliishambulia hukumu ya Mahakama ya Kasitu iliyowatia hatiani wanasiasa hao, huku akidai kuwa haikuwa hukumu katika macho ya kisheria kutokana na kasoro kubwa za kisheria ilizokuwa nazo.
Katika kuhitimisha hoja zake, wakili Kibatala aliiomba Mahakama Kuu kama itakubaliana na hoja zake na kuona kuwa ina kasoro kubwa za kisheria, basi aifutilie mbali na kuwaachia huru warufani hao.
Lakini Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai uchambuzi wa ushahidi uliofanywa na Mahakama hiyo ya awali ulikuwa unakidhi na ulihusu makosa yote.
Hata hivyo, aliiomba Mahakama hiyo kama itaridhika kuwa hukumu hiyo ina upungufu, ifanye uchambuzi wa ushahidi kwenye kumbukumbu kisha itoe uamuzi wake yenyewe.
Katika kutia uzito hoja kwamba Mahakama hiyo ilikuwa na haki ya kuingia katika viatu vya Mahakama ya chini, kuangalia ushahidi wote na kuupima dhidi ya uamuzi huo, Wakili Nchimbi aliirejesha Mahakama hiyo katika kesi ya Kileo Kileo na wengine wanne dhidi ya jamhuri.
Hizi ni rufaa za jinai zilizounganishwa, namba 82 ya mwaka 2013 na namba 330 ya mwaka 2015 iliyoamuriwa na Mahakama ya Rufani iliyokaa Tanga (ambayo haijaripotiwa kwenye vitabu vya sheria).
Ni msimamo wa kisheria na kutokana na uamuzi wa mashauri mbalimbali katika Mahakama za juu, hasa Mahakama ya Rufani, kuwa Mahakama inaposikiliza rufaa kwa mara ya kwanza, mbali na sababu za rufaa zinazowasilishwa, lakini pia ina mamlaka ya kurejea katika ushahidi.
Kwa uamuzi huo ambao huzifunga Mahakama zote za chini na kulazimika kuufuata, Mahakama husika ina mamlaka ya kufanya uchambuzi na kutoka na uamuzi wake kulingana na uchambuzi huo uliofanyika.
Mahakama Kuu ikiwa ni ya kwanza kusikiliza rufaa hiyo, ilikuwa na mamlaka ya kwenda kurejea ushahidi na kufanya uchambuzi kuona kama ushahidi uliopo ulikuwa unatosha kuwatia hatiani washtakiwa (warufani) au la.
Katika kufanya hivyo, ikiridhika na ushahidi uliokuwepo unatosha kuwatia hatiani basi hutoa hukumu yake kulingana na ushahidi na uchambuzi wake kwa jinsi unavyomtia au usivyomtia mrufani hatiani.
Kwa hiyo kasoro hizo za kisheria katika hukumu inayokatiwa rufaa zinakuwa zimerekebishwa kwa hukumu ya rufaa hiyo.
Kwa hiyo hitimisho la hoja za mawakili wa kila upande lilikuwa na lengo la kukwepa, kupata matokeo kinyume au yanayounufaisha.
Wakati wakili Kibatala akiomba Mahakama ikijiridhisha tu kuwa hukumu hiyo ina kasoro kubwa za kisheria kiasi cha kuifanya isiwe halali, iishie hapo, alijua kuwa kama Mahakama ikienda mbali na kufanya uchambuzi wa ushahidi inaweza kuridhika na ushahidi na ikaendelea kuwatia hatiani wateja wake.
Hivyo, kuwepo kwa kasoro hizo za kisheria kwenye hukumu ya Mahakama ya Kisutu hata za kuifanya isiwe halali kusingekuwa na manufaa yoyote kwa wateja wake.
Asingeweza kutabiri kuwa Mahakama baada ya kurejea kufanya uchambuzi wa ushahidi huo ingetoka na uamuzi gani, lakini badala yake hatua ya Mahakama kwenda kwenye ushahidi ilikuja kuwa na manufaa zaidi kwa wateja wake.
Lakini mawakili wa Serikali wakati wakiiomba Mahakama kama itajiridhisha kuwa hukumu hiyo ilikuwa na kasoro za kisheria, basi ichukue jukumu la kufanya uchambuzi wa ushahidi kwenye kumbukumbu kisha ifanye uamuzi wake yenyewe, nao walikuwa na matarajio ya kunufaika na uamuzi huo.
Walijua kuwa kama Mahakama ingeridhika na ushahidi huo basi kasoro hizo za kisheria katika hukumu hiyo zisingekuwa na athari yoyote kwa upande wake kwa kuwa Mahakama ingeweza kurekebisha kasoro za kisheria katika hukumu ya Mahakama ya Kisutu kwa kutoa hukumu yake ambayo bado ingewatia hatiani.
Baada ya kusikiliza hoja hizo za pande zote, Jaji Mugeta katika uamuzi wa hatua gani ya kuchukua, alikubaliana na hoja za wakili wa Serikali Nchimbi kurejea na kufanya uchambuzi wa ushahidi uliopo na kutoa uamuzi wake yenyewe.
Jaji Mugeta alisema kuna sheria kesi nyingi zinazotoa mamlaka kuwa Mahakama inayosikiliza rufaa husika kwa mara ya kwanza inaweza kuingia katika viatu vya Mahakama ya chini na kurekebisha kasoro kwenye hukumu hiyo.
Katika kuweka uzito uamuzi wake huo, Jaji Mugeta alirejea katika kesi mbili kati ya hizo nyingi, akisema iliamuriwa hivyo katika kesi ya Dinkarai Ramkrishna Pandya dhidi ya Jamhuri (1957) E.A 336 (Kitabu cha Sheria za Afrika Mashariki, ukurasa wa 336).
Kesi nyingine aliyoirejea ni ya Damson Ndaweka dhidi ya Ally Said Mtepa, rufaa ya madai namba 5/1999, iliyoamuriwa na Mahakama ya Rufani Arusha (haijaripotiwa).
Baada ya kuainisha kesi hizo kati ya nyingi zinazotoa mamlaka kwa Mahakama inayosikiliza rufaa kwa mara ya kwanza kurejea na kufanya uchambuzi wa ushahidi, Jaji Mugeta akaanza kuchambua shtaka moja baada ya lingine na kuona namna gani ushahidi uliopo umethibitisha au haukuweza kuthibitisha shtaka husika.
***
Katika kesi ya msingi washtakiwa walikuwa ni mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye pia alikuwa mbunge wa Hai, Dk Vincent Mashinji (katibu mkuu wakati huo ambaye sasa ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti) na aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Wengine walikuwa ni manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara, sasa katibu mkuu) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mweka hazina wa Baraza la Wanawake (Bawacha) na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Pia, walikuwamo aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha na mbunge wa Kawe, Halima Mdee; aliyekuwa mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na aliyekuwa mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.
Warufani hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama kutenda kosa, mkusanyiko haramu, kufanya ghasia/fujo, baada ya ilani ya polisi, kuhamasisha hisia za uadui kwa nia ovu, kuamsha chuki, uchochezi na kushawishi utendaji kosa.
Pia, walikuwa wakidaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 wakati Jeshi la Polisi lilipotumia nguvu kuwazuia na kuwatawanya wao na wanachama waliokuwa wakiandamana kwenda ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, ambaye pia alikuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni.
Walikuwa wakienda katika ofisi hiyo kudai barua za utambulisho wa mawakala wao waliokuwa wanatarajiwa kusimamia uchaguzi mdogo wa Kinondoni.
Wote walitiwa hatiani lakini wakakata rufaa kupinga hukumu, isipokuwa Dk Mashinji pekee.
Nini alichokibaini katika ushahidi uliopo kwa kila shtaka lililokuwa likiwakabiliwa washtakiwa (warufani)? Usikose kesho