Jaji Mkuu mstaafu awafunda mahakimu

Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman

Muktasari:

  • Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amewataka mahakimu wa mahakama za mwanzo kutotumia vibaya uhuru waliopewa kisheria wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kupunguza malalamiko ya wananchi.

Lushoto. Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amewataka mahakimu wa mahakama za mwanzo kutotumia vibaya uhuru waliopewa kisheria wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kupunguza malalamiko ya wananchi.

Amesema mahakimu wa Mahakama za mwanzo wanapaswa kufuata taratibu wakati wa kuendesha na kutoa hukumu kwa sababu ndiyo wanaobeba taswira ya Mahakama ya Tanzania kwa kuwa asilimia 70 hadi 75 ya kesi zipo Mahakama za mwanzo.

Amesema hayo leo Jumatano Januari 19, 2022 wakati akifungua mafunzo elekezi kwa mahakimu wakazi wapya 35 yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto.

"Mjitambue kwamba mpo katika ngazi ya uongozi huko vituoni kwenu kwa hivyo wakati wa kuendesha na kutoa hukumu fuateni taratibu" amesema Jaji Mkuu mstaafu Othman.

Mambo mengine yanayotakiwa kufuatwa na mahakimu hao ni kutambua kwamba hawafungwi na maoni ya wazee wa baraza wakati wa kutoa hukumu ili kujiweka katika mstari sahihi iwapo walalamikaji watakata rufaa.

"Kila hakimu lazima kujitayarisha kabla ya kwenda mahakamani, andikeni sababu ya kutoa maamuzi, kila hukumu lazima iwe na sababu yenye uzito" amesema.

Mkuu wa chuo cha uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Jaji Profesa Paul Kihwelu amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo mahakimu hao wapya ili wakifika kwenye vituo vyao vya kazi waweze kuendesha mashauri kwa ufanisi zaidi.