Jaji Warioba ashauri mkataba wa bandari upitiwe upya

Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba

Muktasari:

  • Jaji Warioba amesema katika mkataba huo kuna vipengele vinavyotia wasiwasi, hivyo viangaliwe kabola ya kwenda kwenye mikataba mingine.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amezungumzia mkataba wa uendelezaji na uboreshaji bandari kati ya Tanzania na Dubai, akisema una vipengele vinavyotia wasiwasi, hivyo unapaswa kupitiwa upya ili kuondoa wasiwasi huo.

Mkataba huo ulisainiwa Oktoba 25, 2022 na serikali hizo mbili, ulipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Juni 10, 2023, huku ukizua mabishano miongoni mwa Watanzania.

Akizungumza jana Juni 23, 2023, Jaji Warioba amesema licha ya kuwepo kwa utendaji mbovu katika bandari za Tanzania, kuna haja ya kujifunza kwenye mikataba iliyopita ili makossa yaliyopita yasije yakarudiwa.

“Nimeusoma huo mkataba wa makubaliano. Mimi niliamini kwa sababu sio mara ya kwanza tumekuwa na mikataba ya aina hii, tumekuwa na mikataba hii katika maeneo mbalimbali. Sasa tunapofanya hii mikataba tujifunze humo nyuma mapungufu gani yalikuwepo.

“Ni kweli kwamba mkataba ule una vipengele ambavyo vingezua wasiwasi, hili tusilikwepe tuliangalie tuone tutakavyoweza kuboresha hiyo,” amesema.

Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema hakukuwa na maandalizi ya mapema katika kuingia mkataba huo.

“Nadhani tumechelewa katika utaratibu huu, kwa sababu tulikuwa na TICTS (Tanzania International Container Services) pale, tulijua mwisho wake umefika, tungejua tungefanya mapema, kwa sababu bandari ni muhimu sana.

“Haitoshi tu kusema haya ni makubaliano, hayo yanayozunguzwa yatakuja kwenye mikataba mingine, hapana. Waangalie hayo yapo kwenye mkataba huo, ambayo yanaleta wasiwasi watafute njia ya kuyaondoa,” amesema.