Janga la moto Kariakoo lafichua mambo mazito

Janga la moto Kariakoo lafichua mambo mazito

Muktasari:

  • Moto uliolipuka katika Soko Kuu la Kariakoo na kuteketeza mali za wafanyabiashara umeonyesha kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini lina changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kukabiliana na majanga ya moto na rasilimali watu.

  



Dar es Salaam. Moto uliolipuka katika Soko Kuu la Kariakoo na kuteketeza mali za wafanyabiashara umeonyesha kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini lina changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kukabiliana na majanga ya moto na rasilimali watu.

Moto huo ulioteketeza soko la kihistoria, umewaacha zaidi ya wafanyabiashara 225 wakipoteza mali zao, huku Serikali ikipoteza fursa za biashara na kodi.

Tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameunda kamati inayohusisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuchunguza chanzo na ukubwa madhara ya moto huo.

Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alipotembelea eneo hilo, ilibainika kuwa visima vinavyotakiwa kutoa maji kwa ajili ya kuzimia moto havikuwa na presha ya kutosha kusukuma maji kuuzima.

Simbachawene alisema upo umuhimu wa sekta zinazohusika, hasa Wizara ya Maji kuhakikisha maeneo yote yanapata maji yenye presha kubwa.

“Kilichosababisha hapa ni kukosekana kwa hivi visima, lakini pia majengo haya yalijengwa zamani na yalikuwa hayazingatii sana misingi ya kitaalamu ya kupambana na matukio ya moto wala mifumo ya utoaji taarifa, ikiwamo alamu.

“Kuna mambo mengi yenye changamoto nyingi. Hatuwezi kurudi kwenye maisha yaleyale kukiwa na changamoto zilezile,” alisema Simbachawene.

Juzi Kikosi cha Zimamoto cha Dar es Salaam kililazimika kufuata maji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), umbali wa kilometa 9.7 kutoka Kariakoo baada ya kuishiwa maji.

Jana, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Mkoa wa Dar es Salaam, Bakari Mrisho alimwambia Simbachawene kuwa visima vilivyopo vya maji kwa ajili ya kuzima moto viko vinne, lakini vinavyofanya kazi ni vitatu.

Alisema kimoja kipo mtaa wa Nyati, kingine kwa aliyekuwa Meya, Abuu Juma na kilichopo mtaa wa Ushirika.

“Jirani na hili soko hakuna kisima na hivyo vilivyopo havina presha. Hatukuweza kupata kabisa maji hadi tulipofuata Uwanja wa Ndege. Hawawezi kulaumu sana kwani jengo hilo lilijengwa kabla sheria ya kuweka visima kwa ajili ya kuzimia moto havijawekwa, kwa sasa wanalo jukumu la kuwaambia waweke,” alisema Mrisho.

Katika tukio jingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alielekeza barabara zote zibaki wazi na kuwa wafanyabiashara wa soko dogo wanaweza kuendelea na shughuli zao za biashara kutokana na kutoathiriwa na moto.

Si Dar pakee

Kilichotokea Kariakoo kinaweza kutokea mahali pengi nchini, kwa mfano, Mkoa wa Kilimanjaro wenye wilaya sita, ni Manispaa ya Moshi pekee yenye gari la Zimamoto ambalo ni kuukuu, na halina uwezo wa kuzima moto katika majengo yanayozidi ghorofa moja.

Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu alisema kutokana na gari pekee la Zimamoto kuwa ni bovu au kuhitaji kubadilishiwa vipuri, gari la Kiwanda cha Sukari cha TPC kilichopo umbali wa kilometa 23 kutoka mjini ndilo limekuwa linasaidia kukabiliana na majanga ya moto.

Vilevile, kama ilivyo kwa Kariakoo, mfumo wa visima vya maji uliokuwa katika mitaa mingi haifanyi kazi kuanzia miaka ya 2000.

“Gari lipo lakini ni la zamani, vipuri ni vibovu, jambo ambalo lilisababisha mwaka huu mwezi wa tatu nyumba moja kuungua mpaka ikaisha kwa sababu gari ni bovu,” alisema.

Kamanda wa Zimamoto, Mkoa wa Kilimanjaro, Inspekta Abraham Ntezidyo alisema changamoto Kilimanjaro majengo mengi ni ya zamani na hayana mfumo wa kukabiliana na moto.

“Ni machache yenye mifumo. Mifumo yake inahitaji ukarabati, tumeendelea kufanya ukaguzi na kutoa ushauri, lakini baadhi ya wamiliki wamekuwa wakilalamikia suala la bajeti,” alisema Inspekta Ntezidyo.

Majiji ya Tanga na Arusha yana mifumo mizuri ya visima vya maji ambavyo huwezesha magari ya Zimamoto kuchukua maji wakati wa harakati za kukabiliana na majanga ya moto.

Kamanda wa jeshi hilo Tanga, Fatma Ngenya aliliambia gazeti hili kuwa mifumo hiyo ya visima iko vizuri katika jiji hilo na wilayani, isipokuwa baadhi ya visima huzibwa wakati wa utengenezaji au ukarabati wa barabara.

Alisema kwa Tanga kuna mfumo wa jumla ya visima 335 kwenye mitaa mbalimbali, lakini kutokana na shughuli za utengenezaji barabara na kupanua majengo baadhi vimeziba na kubaki 230 vinavyofanya kazi.

Kwa Jiji la Arusha kuna visima 70 maalumu kwa kutoa maji yanapotokea majanga ya moto, kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Zimamoto mkoani humo, Yusuph Semtana.

Semtana alisema sasa hakuna hofu ya zimamoto katika Jiji la Arusha kukosa maji kwa kuwa kuna visima 70 vilivyojengwa kupitia mradi ambao ulizinduliwa Desemba 2018 kwa gharama ya Sh520 bilioni.

Changamoto ya watumishi

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa katika mikoa kadhaa umebaini kuwa idara hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi kiasi cha baadhi ya wilaya kutokuwa na mtumishi hata mmoja wa idara ya Zimamoto.

Kwa mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto, Omary Simba alisema licha ya upungufu wa watumishi na vifaa, ubora wa vifaa vilivyopo haukidhi mahitaji ya sasa, hasa ya kuzima moto katika majengo makubwa na marefu yanayoendelea kujengwa mkoani humo.

Ukaguzi wa vifaa

Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, Joseph Masabeja alisema ukaguzi wa vifaa vya kuzimia moto na kutoa elimu ni suala linalofanywa na jeshi hilo na hutoa hati kwa kila jengo baada ya ukaguzi. Hata hivyo, bila kuhusisha na tukio la moto Kariakoo, Masabeja alisema ni muhimu kila nyumba na jengo kuwa na miundombinu ya kung’amua moshi na kupiga king’ora ili watu waweze kuudhibiti moto mapema.

Mwigulu azungumzia fidia

Akizungumza kwenye mahojiano na Kituo cha televisheni cha Clouds TV, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali itaanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya bima mbalimbali ili yanapotokea majanga wafidiwe hasara itakayotokea.

Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema na Florah Temba (Moshi), Burhan Yakub (Tanga), Mussa Juma (Arusha), Fortune Francis, Ephrahim Bahemu na Peter Elias (Dar) pamoja na Beldina Nyakeke (Mara) na Samirah Yusuph (Simiyu).