Jeshi la polisi kujenga maabara za upelelezi kila kanda

Muktasari:
- Maabara hizo zitasaidia kupanua wigo wa uchunguzi wa makosa kwa sababu badala ya kufanya upelelezi kwenye maabara ya Dar es Salaam, kila kanda itafanya upelelezi kwenye maabara yake.
Dodoma. Jeshi la Polisi nchini limeanza ujenzi wa maabara za sayansi za upelelezi wa makosa ya jinai kwenye kanda sita nchini ikiwemo Zanzibar.
Maabara hizo zimetajwa kwamba zitaharakisha uchunguzi wa kesi za makosa ya jinai zinatarajia kukamilika katika kipindi cha miaka mitano.
Mkuu wa Kitengo cha Uhalifu wa Kimtandano, Joshua Mwangasa leo Machi 21 wakati akizungumza kwenye mkutano wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama wa mtandao kwa wakuu wa upelelezi na maafisa usalama wa polisi nchini.
Mwangasa amesema Maabara hizo zitasaidia kupanua wigo wa uchunguzi wa makosa kwa sababu badala ya kufanya upelelezi kwenye maabara ya Dar es Salaam, kila kanda itafanya upelelezi kwenye maabara yake.
Ofisa huyo wa polisi amesema maabara hizo zitakuwa katika kanda ya Ziwa, kanda ya Kaskazini, kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kanda ya Kati, kanda ya Pwani na Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camilius Wambura amesema mafunzo hayo yatakuwa endelevu lengo likiwa ni kila askari wa upelelezi kuwa na elimu kuhusu makosa ya mtandao.
“Mafunzo haya ni lazima yawe endelevu kwa sababu teknolojia inabadilika, hivyo na sisi inatulazimu kuwapa mafunzo mara kwa mara ya kukabiliana na makosa yanayofanywa mtandaoni,” amesema Wambura.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Jimmy Yonazi amelitaka Jeshi la Polisi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujua nini maana ya makosa ya mtandao ili waepukane nayo.
“Nitoe wito kwa DCI, kupitia elimu wanayoipata hapa, waitumie kuelimisha jamii nini maana ya makosa ya mtandao na namna ya kuchukua tahadhari ya kuepuka makosa ya mtandao. Kuna wakati utamwadhibu mtu lakini kumbe hata hajui nini makosa ya kimtandao,” amesema.