Joto lapanda uteuzi wa wakuu mikoa, wilaya

Friday April 16 2021
jotopic

Rais Samia Suluhu akifurahia jambo na Makamu wake, Dk Philip Mpango walipokutana Ikulu jijini Dodoma juzi kwa ajili ya kufanya mazungumzo. Picha na VPO

By Habel Chidawali
By Bakari Kiango

Dodoma/Dar es Salaam. Kutokana na hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Aprili 6 baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao pamoja na wakuu wa taasisi aliowateua na kudokeza kuhusu mabadiliko atakayoyafanya kwenye halmashauri, wachambuzi wa siasa wanasema kuna viashiria vya jambo hilo kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Kwenye hotuba hiyo, Rais Samia alisema kazi iliyobaki mbele yake ni kuwateua wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri kutimiza safu ili kazi iendelee.

Wakati kauli hiyo ikipandisha joto kwa wateule waliopo wenye hofu ya kutemwa, kuna kila dalili za mabadiliko hayo kufanyika wakati wowote kutokana na nyendo za Rais siku za karibuni.

Kitendo cha Rais Samia kukutana na makamu wake, Dk Philip Mpango jana jijini Dodoma, kinatafsiriwa kuwa na jambo kubwa linaloweza kutokea baada ya majadiliano yao.

Akiizungumzia Wizara ya Tamisemi, Rais alisema wakati wowote atafanya uteuzi wa viongozi hao.

“Hivi karibuni tutafanya nafasi za wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ili kusudi tukamilishe safu ili kazi iende ikafanyike,” alisema Rais Samia.

Advertisement

Licha ya muda mfupi aliokalia kiti, Rais Samia anatajwa kuwa mtu asiyetabirika kwamba anaweza kufanya lolote na kwa wakati wowote, huku akibebwa na uzoefu kwani wengi anaufahamu utendaji wao kwa karibu.

Rais Samia aliapishwa Machi 19, siku mbili tangu kutangazwa kwa kifo cha Rais John Magufuli. Hata hivyo katika kipindi kifupi ameshabadilisha baadhi ya mawaziri, makatibu wa wizara na wakuu wa taasisi za umma.

Machi 28, alianza kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko kupisha uchunguzi wa madai ya ubadhirifu wa zaidi ya Sh3 bilioni.

Katika hotuba hiyo, Samia alimnyooshea kidole aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo kwamba wizara yake imejaa wizi na kumtaka aeleze kama ameshindwa ili asaidiwe, lakini siku chache baadaye alimtoa kwenye wizara hiyo na kumpeleka ofisi ya Makamu wa Rais akasimamie Muungano na Mazingira.

Mabadiliko mengine aliyafanya kwenye baraza la mawaziri na makatibu wakuu katika baadhi ya wizara na kuwabadilisha baadhi ya wakuu wa taasisi na mashirika ya umma.

Maoni ya mchambuzi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus amesema baada ya Rais kuteua mawaziri na makatibu wakuu, kinachosubiriwa sasa ni mabadiliko kwenye ngazi za mikoa, wilaya na halmashauri kama alivyoahidi mwenyewe.

Kristomus alisema kitendo cha Rais Samia kurudi Dodoma na kukutana na Dk Mpango kinaashiria huenda mchakato wa uteuzi ukakamilika hivi karibuni na mabadiliko hayo kutangazwa kwa wananchi.

“Rais Samia wakati anaapisha makatibu wakuu alidokeza kuwa hatua ya uteuzi inayofuata ni kukamilisha safu ya uongozi kwa kuwapanga wakuu wa mikoa, makatibu tawala, wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

“Rais pia alieleza kuwa kazi nyingi za kuwatumikia wananchi zinafanywa na ofisi za mikoa na wilaya. Hivyo angependa kuona anapanga safu yake mapema ili kazi iendelee,” alieleza Kristomus.

Mchambuzi huyo alieleza katika siku za karibuni baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakilalamikiwa kwa utendaji mbovu, kukiuka misingi ya utawala bora na baadhi yao kufikisha umri wa kustaafu.

Alisema wananchi wamesubiri kwa muda mrefu kuona anafanya mabadiliko Tamisemi ambayo ni sawa na kusema ndio Serikali ya Tanzania Bara kwa kuwa inahusika na utawala wa ngazi zote kuanzia mikoa mpaka wilaya.

Lakini, baada ya ukimya uliotokea siku mbili tatu zilizopita, alisema watu wengi wana shauku ya kuyasikia mabadiliko hayo.

“Huenda anahitaji muda mrefu kufanya mabadiliko kwa kuwachambua wateule hao kulingana na hali ilivyo mikoani kwa kushauriana na washauri wake na kupitia utendaji wa kila mkuu wa mkoa, wilaya na watendaji wengine.

“Kutokana na hilo, tutegemee mabadiliko makubwa kwa ngazi za wakuu wa mikoa kwani huenda utendaji wa baadhi ukawa umemvutia Rais hivyo kuwateua tena kuendelea kuwatumikia wananchi kwenye nafasi hiyo na wengine akawapumzisha kwa maslahi ya umma,” aliongeza.

Kristomus aliongeza kuwa Rais anaweza kuamua kuhamisha baadhi yao na kuwarudisha kwenye ofisi zao za zamani kama ataona wameshindwa kukidhi vigezo vya utumishi serikalini.

“Baadhi ya walioteuliwa walikuwa wafanyakazi wa taasisi za umma hivyo wanaweza kurudishwa nafasi zao za zamani na kuendelea na majukumu au kupelekwa Tamisemi kwenda kuwa maofisa wa kawaida,” alisema Kristomus.

Advertisement