Jumuiya ya Wazazi CCM yataka kuongezwa ulinzi watoto wa kiume

Muktasari:

  • Jumuiya ya Wazazi (CCM) Mkoa wa Iringa imewataka wazazi na jamii kushiriki katika vita ya ukatili na ulawiti.

Iringa. Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Iringa imewataka wazazi kushiriki katika vita dhidi ya vitendo vya ulawiti na ushoga vinavyoanza kuonekana kama vya kawaida katika baadhi ya jamii nchini.

Akizungumza katika kikao cha Baraza Kuu la jumuiya ya mkoa huo kilichofanyika  mjini Iringa, Katibu wa Siasa na Oganaizasheni Jumuiya ya Wazazi Makao Makuu, Said King'eng'ena amesema vitendo hivyo ni moja ya changamoto zinazotakiwa kushughulikiwa na Jumuiya ya Wazazi ambayo inajukumu la kulinda malezi ya watoto na jamii kwa ujumla.

King'eng'ena aliwataka wazazi kuongeza ulinzi zaidi kwa watoto wa kiume ambao wako hatarini kuharibiwa kizazi chao na kutengeneza kizazi kisichoeleweka katika nchi hii.
" Nawaomba wazazi muongeze ulinzi kwa mtoto wa kiume kwa sababu mtoto huyu akifanyiwa kutendo hicho hawezi kuacha ataendelea kudai kufanyiwa au kufanya kutokana na mfumo wa maumbile ya huko nyuma, hivyo tuwalinde sana na kuwaepusha na vitendo hivi vya ulawiti."

Amesema kuwa maadili na malezi katika familia nyingi yamepungua kutokana na wazazi wengi kuachia majukumu kwa wadada wa kazi jambo ambalo si jema kwa upande wa malezi kwa sababu watoto wengi wanafanyiwa ukatili na kukosa sehemu ya kusemea kutokana na wazazi kutokuwa na muda wa kuwasikiliza na kuwafatilia watoto wao.