Kagaigai awaonya wananchi wanaovamia vyanzo vya maji
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo. Picha na Janeth Joseph.
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji yanavyomilikiwa kihalali na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Mjini Moshi (Muwsa).
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji yanavyomilikiwa kihalali na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Mjini Moshi (Muwsa).
Amesema wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakivamia maeneo hayo na kusababisha migogoro bila sababu ilhali maeneo hayo yana hati miliki huku akisema hatavumilia kuona watu wa namna hiyo.
Kagaigai ameyasema hayo leo Septemba 9, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema eneo la Mabogini lenye ukubwa wa ekari 100 ambalo linahifadhi na kuchakata maji taka lisiingiliwe na mtu yoyote zaidi ya Mamlaka hiyo.
"Nimetembelea maeneo ya vyanzo vya maji, nimependa namna Muwsa wanavyotunza vyanzo hivi, niwaombe wananchi wangu wa Kilimanjaro tutunze vyanzo hivi vya maji, mtu yeyote asiingilie kwenye vyanzo hivi," amesema Kagaigai.
"Mwananchi yeyote anayefikiria atakwenda kwenye vyanzo hivi na kuvuruga utaratibu ambao umewekwa na Serikali, sitamvumilia na sitakuwa naye maana maeneo haya yapo kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Moshi na mkoa wetu kwa ujumla," amesema Kagaigai