Kairuki na kibarua hiki Tamisemi

Muktasari:

  • Siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Angellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wanazuoni wametaja kibarua kitakachomkabili wizarani humo.


Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Angellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wanazuoni wametaja kibarua kitakachomkabili wizarani humo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wanazuoni hao walisema kuutafsiri muunganiko wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ni miongoni mwa vibarua vigumu kwa Kairuki, kwa kuwa ndilo jukumu mama la waziri wa Tamisemi.

Kairuki aliteuliwa na Rais Samia Oktoba 2, mwaka huu akichukua nafasi ya Innocent Bashungwa, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mwingine katika uteuzi huo ni Dk Stergomena Tax, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akichukua kijiti kutoka kwa Balozi Liberata Mulamula.

Uteuzi wa Kairuki ndani ya Tamisemi unamfanya kuwa mwanamke wa tano kushika wadhifa huo katika wizara hiyo tangu mwaka 1961.

Kabla yake, mawaziri wanawake waliowahi kuhudumu nafasi hiyo ni Anna Abdallah, Celina Kombani, Hawa Ghasia na Ummy Mwalimu.

Hata hivyo, uteuzi wa Kairuki unafanya katika kipindi cha miezi 18 ya Rais Samia madarakani, wadhifa wa Waziri wa Tamisemi uongozwe na watu watatu, wengine ni Ummy Mwalimu na Innocent Bashungwa.

Kibarua kitakachomkabili

Akizungumza na Mwananchi jana, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema Kairuki anaingia katika wizara hiyo akiwa na vibarua vitatu vigumu.

Alikitaja kibarua cha kwanza ni kutafsiri muunganiko wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Usimamizi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ni kibarua kingine, alichokisema Dk Mbunda kuwa kitamkabili Kairuki katika majukumu yake hayo mapya.

Alisema kusimamia uwiano wa ukusanyaji mapato na matumizi ya makusanyo hayo katika shughuli za maendeleo ya wananchi ni kazi nyingine mbele ya Angella.

“Kwenye mapato hapo kuna watu wanatafuta mbinu ya kuiba na wengine wanapambana kukwepa kulipa kodi, hizi zote ni kazi za Kairuki kuhakikisha anadhibiti yasitokee,” alisema Dk Mbunda.

Hata hivyo, Dk Kelvin Musini alisema waziri huyo anawajibika kuwa kiungo sio tu wa wananchi na Rais, bali Tamisemi na wizara nyingine.

“Kwa sababu Tamisemi inabeba wizara zote, waziri wake anapaswa kuelewana na mawaziri wenzake wote, kuwe na muunganiko kati ya wizara hiyo na nyingine, hapo kazi itakuwa rahisi,” alisema Dk Munisi.

Ili kurahisisha kazi ndani ya wizara hiyo, Dk Munisi ambaye pia ni mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora UDSM, alisema Kairuki anapaswa kutambua majukumu ya wizara hiyo ni huduma kwa wananchi.

“Kukitokea huduma zinalegalega huko Kazulamimba au Mpanda, atakayenyooshewa kidole ni waziri husika, hivyo ni lazima ahakikishe anasimamia utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Dk Munisi.

Pia, alisema kibarua kingine kwa Kairuki ni kutambua vema sera zinazoihusu wizara hiyo ili aimarishe usimamizi wake.

Hata hivyo, yapo madai ya ugumu katika utendaji ndani ya wizara hiyo kama inavyoelezwa na mawaziri waliowahi kuiongoza.

Paul Kimiti, aliyekuwa Waziri wa Tamisemi mwaka 1982 hadi 1984, alisema ugumu katika wizara hiyo unatokana na wingi wa sekta zinazosimamiwa.

“Huwezi kuwa mtaalamu wa elimu, wakati huohuo uwe mtaalamu wa afya na Serikali za Mitaa na mambo mengine, kwa namna yoyote utadanganywa tu, kwa hiyo inahitaji ujue mambo mengi,” alisema Kimiti.

Hata hivyo, alisema wanaopewa nafasi hizo wanajikuta wanasimamia maeneo ya taaluma zao au wakati mwingine wanakosa eneo la kushika.

Kimiti alitaja mabadiliko ya kuiondoa wizara kutoka Ofisi ya Rais na kuirudisha Ofisi ya Waziri Mkuu ni moja ya hatua zitakazofaa kuimarisha utekelezwaji wa majukumu yake.

“Huko mbele hii wizara iangaliwe, Waziri Mkuu ndiyo mtendaji mkuu wa Serikali, ukimpa Tamisemi ni majukumu yake na atasimamia vema, lakini kazi hii ukimpa Rais unamuonea, ofisi yake ni nyeti inapaswa kusimamia utawala wa jumla,” alisema Kimiti.

Waziri mwingine aliyeiongoza Tamisemi, Anna Abdallah alisema zamani ili kuwa waziri wa Tamisemi, ilikupasa ubobee kitaaluma au uzoefu katika Serikali za Mitaa.

“Sio kila mtu anaweza kuongoza Tamisemi, lazima apatikane mbobezi wa Serikali za Mitaa, hivi ndivyo tulivyofanya zamani na chuo maalumu kilikuwa Mzumbe, mtu akitoka hapo anakuwa ameiva,” alisema Anna.

Mbali na ubobezi, alisema zamani kulikuwa na Tume ya Serikali za Mitaa iliyohusika hata na masuala ya nidhamu, kitu ambacho kwa sasa haifahamiki kama kipo au la.

“Mimi kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Tamisemi, nilianza kuwa mkuu wa wilaya kisha mkoa, kwa hiyo nilibobea kwenye Serikali za Mitaa hadi nateuliwa wizarani haikuwa ajabu.”