Kamati kuu Chadema ‘yawafyeka’ wagombea hawa

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mboe akizungumza wakati wa kikao cha kamati kuu ya chama hicho jijini Dar es salaam. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu na kulia ni Katibu Mkuu John Mnyika. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imefanya usaili kwa watia nia wa nafasi za ikiwamo ya uenyekiti, makamu na mhazini wa kanda

Dar es Salaam. Usaili wa siku mbili wa wagombea wa nafasi mbalimbali katika kanda nne za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeacha kicheko, kilio na simanzi kwa watia nia waliopenya na wanaodaiwa kukatwa majina yao baada ya kutokidhi vigezo.

Mchakato huo ulioitimishwa usiku wa kuamkia leo Jumanne, Mei 14, 2024 ulikuwa wa moto na hofu miongoni mwa wagombea kupenya kwenda katika hatua inayofuata ya kuanza kampeni ili kuwania nafasi walizoziomba katika kanda nne za chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Mwananchi Digital imedokezwa takribani watia nia 10 wamekatwa majina yao wakiwamo wanaowania uenyekiti na umakamu katika kanda za Victoria, Serengeti, Nyasa na Magharibi.

Kanda ya Serengeti ina mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu, kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Nyasa (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa) na Victoria (Mwanza, Kagera na Geita).

Mchakato wa kuwasaili wa wagombea hao ulianza kwa Kanda ya Magharibi kisha Nyasa, Serengeti na Victoria, shughuli hiyo iliendeshwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, makamu wenyeviti, Tundu Lissu (Bara) na Said Issa Mohammed wa Zanzibar.

Wengine ni Katibu Mkuu, John Mnyika, manaibu Salum Mwalimu (Zanzibar) na Benson Kigaila (Bara) na wajumbe wengine wa kamati kuu wakiwamo, John Heche, Suzan Kiwanga na Grace Kiwelu.

Mwananchi Digital imedokezwa baadhi ya wanaodaiwa kukatwa ni Emmanuel Ntobi na James Mahangi waliokuwa wakiwania uenyekiti wa kanda ya Serengeti na Daniel Mwambikile aliyetia nia Kanda ya Nyasa.

Wakati katika nafasi ya umakamu wanaoelezwa kupigwa chini ni Alex Kimbe (Nyasa), Ester Jackson, Gango Kidera na Esther Nyaburiri.

Taarifa zinaeleza miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa katika mchujo huo ni pamoja na suala la maadili, nidhamu na sababu za kisiasa ikiwamo namna ya wagombea kama wanauwezo hasa kujieleza na kujibu maswali vema.

Mwananchi imemtafuta Ntobi kujua suala hilo ambaye amesema:"Sijui chochote nasubiri uamuzi wa mwisho utakaotangazwa na kamati kuu maana kikao si kinaendelea?

Naye Kidera amejibu kama ilivyokuwa kwa Ntobi akisema:"Tunasubiri taarifa kamati kuu kwanza si bado haijatoka?

Kwa hatua hiyo, Kanda ya Serengeti imebakiwa na wagombea wawili wa uenyekiti Gimbi Masaba ambaye ni makamu mwenyekiti wa kanda hiyo anayemaliza muda wake na Lucas Ngoto aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mara.

Katika nafasi ya umakamu uenyekiti,  Serengeti imebakiwa na mtu mgombea mmoja Jackson Scania baada ya washindani wake watatu kukatwa kwa sababu mbalimbali.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya chama hicho, usaili huo ulioanza jana asubuhi Jumatatu ulimalizika usiku wa kuamkia leo Jumanne na kuanzia mchana wa leo kikao cha kamati kuu kiliendelea chini ya uenyekiti wa Mbowe, katika ofisi zao mpya za Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Usaili huo ulifanyika kwa nafasi za uenyekiti, makamu, katibu na wahazini wa jumuiya za chama hicho za wanawake (Bawacha), wazee (Bazecha) na vijana (Bavicha) ngazi ya kanda ambao nao kuna baadhi wamekatwa kutokana na sababu mbalimbali.

Wakati watia nia hao wakikatwa katika usaili, taarifa ambazo Mwananchi ilizipata zinaeleza kwenye kikao cha jana ambacho hadi tunakwenda mitambaoni kilikuwa kikiendelea, pamoja na mambo mengine kilifanya uteuzi rasmi wa wagombea.

Katika hatua hiyo, kulikuwa na uwezekano wa baadhi ya majina yaliyokatwa awali kurejeshwa kwa sababu ama kutoacha mgombea mmoja na au sababu zingine: “Hao waliokatwa yawezekana leo kwenye kikao cha majumuisho na uteuzi inayokutana wakarejeshwa.”

Mbali na hilo, kamati kuu hiyo iliyoanza Jumamosi iliyopita ya Mei 11,2024 ilikuwa ikikusanya mambo yote iliyojadili ikiwamo taarifa za uchaguzi wa chama hicho, tathimini ya maandamano ya amani yaliyofanyika baadhi ya mikoa kuanzia Aprili 22-30, 2024.

Pia, kikao hicho inaelezwa kilijadili kauli ya Lissu aliyoitoa Mei 2, 2024, mkoani Iringa kuwa kuna fedha zimemwaga katika chama hicho kuvuruga uchaguzi.

Ni kauli iliyoibua mjadala ndani na nje ya chama hicho na taarifa zinadai, Lissu alitoa maelezo katika kikao hicho.


Ufafanuzi wa Chadema

Mwananchi Digital iliweka kambi kuanzia siku ya kwanza ya kikao hicho, leo Jumanne, imezungumza na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema kuhusu masuala kadhaa yaliyoibuka ikiwamo kukatwa kwa baadhi ya wagombea.

Mrema amesema walikuwa na kikao kuanzia Mei 11, mwaka huu hadi leo ingawa awali ratiba ya kikao hicho ilipangwa kufanyika kwa siku tatu lakini Kamati kuu ili lazimika kuongezea siku moja mbele.

"Katika kikao hiki tumekuwa na ajenda nyingi ikiwamo kupokea taarifa ya chaguzi ngazi za mikoa, wilaya, majimbo, kata, mitaa, vijiji na misingi kwa nchi nzima," amesema.

Amesema kutoka na kazi hiyo kubwa ilisababisha kufanya uteuzi kwa wagombea wa kanda nne ikiwemo Victoria, Serengeti, Magharibi na Nyasa ili waingie kwenye uchaguzi.

"Jana na leo tulikuwa kwenye shughuli ya kusaili watia nia wa kanda zote nne wakiwamo wa chama, mabaraza ya chama na wagombea walikuwa wengi na kusababisha kusogeza siku moja mbele baada ya kumaliza usaili," amesema. Mrema

Amesema kwa siku ya jana kamati hiyo iliendelea na shughuli ya uteuzi na wakikamilisha hatua hiyo wataujulisha umma kwa wale walioteuliwa na ambao hawakuteuliwa na kamati hiyo.

"Maana ya usaili tuna vigezo vyetu kwa mujibu wa katiba na kanuni yetu, ni sifa gani kiongozi wa ngazi gani wanapaswa kuwa nazo kama mtu akikutwa hana hizo sifa basi moja kwa moja anaweza kuenguliwa au kushauriwa akatumikie majukumu mengine kwa sababu bado ni chama kimoja nafasi ni chache wanachama wote hawawezi kuwa viongozi," amesema.

Amesema katika kikao hicho walijadili rufaa nyingi zilizopokewa kutoka kwenye kamati ndogo iliyoundwa kule Mkoani Mtwara kwa ajili ya kushughulikia changamoto za uchaguzi.

"Kamati iliwasilisha ripoti yake kwenye kamati kuu jinsi ilivyoshughulikia rufaa hizo sasa uamuzi wa lini chaguzi zitafanyika kule ambako kamati kuu imekubaliana na warufani tutatoa taarifa yake baada ya kikao kuisha," amesema.

Amesema rufaa zilizowasilishwa na kamati hiyo zinatoka mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Kagera kutoka Jimbo la Kerwa, na Mwanza.

"Rufaa zote zitaamuliwa na kupangwa baada ya kukubaliana kamati kuu kama kamati yake ndogo iliyoundwa ilifanya maamuzi sahihi itapanga ratiba na kutangaza chaguzi hizo," amesema.

Kuhusu chaguzi za kanda hizo, Mrema amesema kulingana na ratiba ilivyo kwa sasa wanatarajia zifanyike kabla ya mwishoni mwa mwezi huu.

"Sasa ni lini kanda ipi itafanya, kamati kuu itaamua na taarifa itatolewa lakini ratiba ilivyo sasa ni kabla ya mwezi huu kanda hizo nne zitakuwa zimekamilika uchaguzi wake," amesema.

Katika hatua nyingine, Mrema amesema katika mchakato wa usaili kuna watu sita hawakufanyiwa usaili kwa sababu mbalimbali ikiwamo mmoja ni mgonjwa na mwingine kajaliwa kupata mtoto.

"Wengine ni wazee na changamoto zao walitoa taarifa na kanuni za chama chetu kinaruhusu kuwasaili watia nia kwa kutumia fomu zao kwa sababu watu wanaitwa kuja kufafanua taarifa walizojaza na kuhojiwa," amesema.

Amesema kamati hiyo ilikosa fursa ya kuwahoji lakini baadhi yao walitumia Tehama kuwahoji kwa njia ya simu kulingana na taarifa za kiafya walizoripoti.