Kamati vyombo vya habari yaongezewa muda
Mwenyekiti wa Kamati ya kutathmini hali ya uchumi kwa vyombo vya habari nchini, Tido Mhando.
Muktasari:
- Kamati ya kutathimini hali ya uchumi kwa vyombo vya habari nchini, imeongezewa muda kutoka miezi mitatu hadi sita ili kufanya kazi kwa umakini mkubwa.
Dodoma. Kamati ya kutathmini hali ya uchumi kwa vyombo vya habari nchini, imeongezewa muda kutoka miezi mitatu hadi sita ili kufanya kazi kwa umakini mkubwa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Tido Mhando amewaambia waandishi wa habari leo Mei 23, 2023 wakati akitoa taarifa ya shughuli zinazoendelea ndani ya kamati hiyo.
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknoloji ya Habari, Nape Nnauye aliunda timu ya watu 10 ili kufanya tathmini ya hali ya uchumi kwa vyombo vya habari, kazi ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni pamoja na Tido Mhando, Dk Rose Reuben, Joyce Mhavile, Bakari Machumu, Richard Mwaikenda, Keneth Simbaya, Jaqueline Wiso na Sebastian Maganga.
Mhando amesema muda huo umetokana na kauli ya Rais kwamba kamati hiyo inatakiwa kufanya kazi kubwa ya tathimini hiyo ili iweze kutoa matunda mazuri yenye mwelekeo wa vyombo vya habari.
“Rais alisema tusilichukulie kwa pupa jambo hilo, sisi tumeomba kuongezewa muda hadi Novemba mwaka huu tutakuwa tumekamilisha kazi iliyo bora na yenye ufanisi, tutakuja na mwongozo mzuri kwa matatizo yanayotukabili,” amesema Mhando.
Ameeleza kuwa kamati hiyo inafanya kazi kwa kujifunza hata kwa mataifa mengine yanayoizunguka Tanzania lakini baada ya kusikia hilo, baadhi ya nchi zimekaa mkao wa kusubiri kamati inatoa matokeo gani.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema muda waliomba bado ni mfupi ukilinganisha na kazi kubwa wanayokwenda kuifanya lakini watapewa ushirikiano ili wamalize kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Nape ameomba waandishi wa habari kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo kila watakapohitajika ili kufanyikisha jambo hilo kwa lengo la kumaliza mzizi wa matatizo kwa vyombo vya habari.