Kamati ya Bunge yamulika kasi ya ujenzi Bandari ya Uvuvi Kilwa

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya  bunge  ya viwanda kilimo, mifugo  na uvuvi  David  Kihanzile (katikati) akipokea  maelezo ya mradi ujenzi wa  bandari ya uvuvi Kilwa  kutoka kwa waziri wa mifugo na uvuvi Abdala ulega. Picha na mwanja ibadi

Kilwa. Kamati ya Kudumu ya Bunge  ya  Viwanda Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi   imesema haijaridhiishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa  na kuitaka Serikali na mkandarasi wa ujenzi wa mradi kuongeza  kasi ya ujenzi ili uweze kukamilika kwa wakati kama ulivyopingwa.

Akizungumza baada ya kamati hiyo kusomewa taarifa na kufanya ukaguzi wa  eneo la ujenzi mwenyekiti wa kamati hiyo  David Kihonzile amesema hajaridhishwa na  kasi ya utekelezaji  wa mradi huyo ambao umepangwa kukamilika mwenzi Septemba 2024.

"Kamati  imesomewa taarifa na kukakagua eneo la ujenzi wa bandari lakini hatujaridhika na mwenendo wa kasi ya ujenzi tumeiangiza Serikali kusimamia kwa  ukaribu mradi huu ili uweze kukamili mapema kama ilivyokusudiwa,” amesema Kihenzile ambaye ni  mwenyekiti wa kamati hiyo.

Aliongeza kuwa serikali ni vyema wakawa waangalifu wakati wa ulipaji fidia maeneo ya wananchi ili kusiwe na malalamiko.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdala Ulega  amesema kuwa wamepokea ushauri wa kamati na watasimamia utatuzi wa changamoto zilizopo kwa ukaribu ili mradi ukamili  kwa wakati kama ulivyokusudiwa.

"Serikali  ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameamua kwa vitendo kusimamia  ujenzi wa miradii mikubwa ikiwemo wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa ili  kutatua tatizo la ajira  kwa vijana na kuongeza uchumi wa nchi,” amesema Ulega.

Ulega amesema  kuwa gharama ya ujenzi wa mradi huo mpaka kukamilika utatumia  Sh282 bilioni na unatarajia kukamilika Septemba  2024  na tayari fedha Sh50 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuendelea  kulipa gharama za mradi.