Kampeni kupambana na ukatili wa kijinsia mtandaoni yaanza

Muktasari:
- Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kushirikiana na taasisi ya Friedrich Ebert Stiftung (FES) wameanzisha kampeni maalum ya kupambana na ukatili wa kijinsia unaofanywa kwa njia ya mtandao.
Dar es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kushirikiana na taasisi ya Friedrich Ebert Stiftung (FES) wameanzisha kampeni maalum ya kupambana na ukatili wa kijinsia unaofanywa kwa njia ya mtandao.
Kampeni hiyo inayofahamika kama ‘zuia ukatili mtandaoni’ inalenga kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na wasichana mitandaoni.
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 16, 2021 kwa niaba ya mkurugenzi wa Tamwa, Sylvia Daulinge amesema teknolojia imekuwa chanzo kipya cha udhalilishaji wa wanawake na kwamba udhalilishaji huo umekuwa na madhara makubwa hasa ya kisaikolojia na hata kusababisha vifo kwa waathirika.
“Tumeona mara kadhaa video na picha za utupu za wanawake na wasichana zikisambaa mitandaoni na matukio haya yameanza kuonekana ya kawaida.”
“Wapo ambao wamekwenda mbele zaidi na kuitumia mitandao kama fimbo ya kuwaadhibu wanawake wanapofanikiwa katika mambo fulani, tunataka jambo hili likomeshwe,” amesema Sylvia.
Kwa upande wake ofisa mradi wa FES, Anna Mbise amesema kampeni hiyo itadumu kwa mwezi mmoja na inalenga kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mitandao.
Pamoja na elimu hiyo kampeni hiyo inalenga kuhamasisha mitandao kuwa sehemu salama kwa kila mtu hususani wanawake.
Naye mrakibu mwandamizi wa polisi wa dawati la jinsia, Leah Mbunda amesema kesi hizo zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku huku wanawake wakiwa waathirika wakubwa.
“Changamoto hii imekuwa kubwa, vijana wengi wanashindwa kuitumia vizuri mitandao ili kupata tija matokeo yake wanajiingiza katika vitu visivyofaa.”
“Hata hivyo polisi tupo na tunawafuatilia wanaofanya vitendo hivi, hivyo wale wanaoathirika kwa namna moja au nyingine wasisite kutoa taarifa,” amesema Leah.