Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kardinali Pengo afariki dunia

Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali  Pengo enzi za uhai wake. Picha na Mtandao

Dar es Salaam. Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengoamefariki dunia saa 4:00 usiku wa Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu akiwa na miaka 82.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, iliyotolewa Februari 20, 2026 na kutiwa saini na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amesema kiongozi huyo alifariki dunia katika hospitali hiyo.

"Ninayo masikitiko makubwa kuwatangazieni kwamba leo Februari 19, 2026 saa 4:00 usiku huu, mpendwa baba yetu Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameitwa nyumbani kwa Baba wa Milele akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam," amesema.

Ameongeza kuwa kiongozi huyo wa kiroho, atazikwa Pugu Februari 28 mwaka huu.

Ratiba ya mazishi yake itaanza na kuwasili kwa mwili wake katika Kanisa la St Joseph kwa ajili ya misa itakayofuatiwa na maombi, hiyo ni Februari 27, 2026.

Hata hivyo, Desemba 24 mwaka jana, Askofu Ruwa’ichi alitoa taarifa ya Kardinali Pengo kupelekwa nchini India kwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa kumpeleka kiongozi huyo wa kiroho nchini India ulitokana na kuugua kwa muda mrefu na matibabu yake kupangwa nje ya nchi.

“Zimefanyika jitihada za kumsaidia hapa kwetu, imeonekana kwamba upo uhitaji wa kumpeleka nje ili apate matibabu ya uhakika zaidi,” ilieleza taarifa hiyo.


Kuhusu afya

Kwa mujibu wa andiko la Mzee wa Atikali, lililosambaa mtandaoni afya ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ilianza kudhoofu miaka mingi iliyopita.

Alipatwa na tatizo la mgongo na kupelekea awe anatembea kwa msaada ya mkongojo. Mwaka 2014, akihubiri katika ibada ya misa maalum iliyoandaliwa na Uwaka (Umoja wa Wanaume Katoliki) kituo cha kiroho Mbagala, Mwadhama alisema: "Kwa muda sasa nimekuwa sionekani kwa kuumwa. Najua wengi wanashangaa kumuona Askofu wao akitembea kwa mkongojo. Nawashukuru wote kwa kuniombea, sasa nina nafuu".

 Januari 1, 2016, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli na mkewe, Mama Janeth Magufuli, walimtembelea kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokuwa amelezwa. Baadaye aliruhusiwa kutoka hospitalini.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alilazimika kufanyiwa operesheni tatu za uti wa mgongo. Operesheni mbili za kwanza alifanyia India.

Alipofanyiwa operesheni ya pili nchini India, alikosa fahamu kwa siku kadhaa akiwa ICU hadi Padri Vicent Mpwaji na Sista Stela waliomsindikiza wakaingiwa na hofu na kutuma ujumbe huku nyumbani kuwa hali sio hali na kuwaomba waamini waongeze sala za kumwombea.

Alipozinduka, yule daktari aliyemfanyia oparesheni alistuka na kushangaa sana na hakujua dawa gani imemsaidia kwani alijua kuwa "Huyu mgonjwa ni wa leo au wa kesho"!

Aliporejea nchini, akashindwa kusimama wima ikabidi baadaye akafanyiwe ya tatu New York, Marekani mwezi Mei 2017.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwahi kufafanua kuwa tofauti na wengi wanavyoamini, shida yake kubwa miaka ya hivi karibuni siyo mgongo bali moyo.

Alisimulia kuwa kabla ya kufanyiwa oparesheni ya mgongo New York, madaktari walipoupima moyo wake walibaini una mushkeri sana na wakatafakari sana kama moyo wake ungeweza kuhimili operesheni hiyo.

Akafafanua kuwa ndio maana alilazimika kwenda mara mbili kwani mara ya kwanza ilikuwa ni kwaajili ya wao kumfanyia uchunguzi wa kina na kufanya tafakuri jadidi. Akapewa madawa ya moyo ya kumsaidia hususan afikapo Tanzania.

Alipokwenda kufanyiwa operesheni ya mgongo, madaktari walimwambia operesheni yake ingekuwa ya muda mrefu, masaa 8 au 9.

Mwadhama Kardinali Pengo akawaambia yeye anawaachia kila kitu, Mungu akipenda ataamka lakini kama siku zake zimefika yeye yuko tayari kwa hilo na akasema itakuwa jukumu la madaktari kuwaeleza Watanzania kilichotokea.

Operesheni ikachukua saa 12 na madaktari wakawa na hofu sana na moyo lakini akapata ahueni ya ajabu.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alisimulia pia kuwa aliwahi kupata shida kubwa ya moyo alipomsindikiza Mhashamu Askofu Titus Mdoe alipohamishiwa Mtwara ambapo alishindwa kabisa hata kuhudhuria ibada.

Januari 26, 2014, Mhashamu Mdoe alieleza kwenye misa Takatifu iliyofanyika Kigango cha Nzasa, Temboni jimboni humo kuwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo hali yake ilikuwa si nzuri na kuwaomba waamini wamwombee.

Ikabidi Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo arudi na alazwe Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambako Prof Mohammed Janabi aliokoa uhai wake.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Aenda India kwa Matibabu

Desemba 24, 2025, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Ruwai'chi, alieleza kuwa afya ya Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, licha ya matibabu aliyokuwa akipatiwa hapa nchini, imedhoofu hivyo alikuwa akipelekwa nchi India kwa matibabu zaidi.


Ombi lake la kuzikwa Pugu limetimia

Katika moja ya mahojiano na chombo cha habari, Kardinali Pengo enzi za uhai wake aliwahi kueleza kuhusu kuwepo kwa kaburi lake katika eneo la Pugu jijini Dar es Salaam na kwamba angependa azikwe hapo.

Alipowahi kuulizwa kwa nini alijichimbia kaburi, alisema, “Lilikuwa wazo la kusema natamani kufia hapa, kwa hiyo nitazikwa hapa pamoja na wamisionari wa kwanza waliokuja kutoa Injili hapa kwetu.

“Wazo la kwamba ningeweza nikafa watu wakasema sijui aende kuzikwa labda Tunduru, Masasi au aende kuzikwa Sumbawanga alikozaliwa, hilo ndilo nilitaka kulifuta kabisa. Nimekuja Dar es Salaam, mimi ni wa Dar es Salaam, nitabaki hapa,” alisema.

Hata hivyo, matamanio yake yametimia baada ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kutangaza maziko ya Kardinali Pengo yatafanyika Pugu jijini Dar es Salaam.


Wanavyomzungumzia

Kutokana na kifo cha kiongozi huyo, Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi akisema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho.

Amemtaja Kardinali Pengo kuwa kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.

“Taifa limepoteza kiongozi aliyelitumikia kwa uadilifu na kujitolea. Mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa,” amesema.

Rais Samia pia ametuma salamu za pole kwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), viongozi wa dini na waumini wote walioguswa na msiba huo.

Aidha, Rais Samia ameungana na Kanisa Katoliki na Watanzania kwa ujumla katika kipindi hiki cha majonzi, akimuomba Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi.

“Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe,” amesema.

Kwa upande wa Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi ametoa pole kwa wafiwa, huku akishukuru kwa maisha na utumishi wake, akisema umegusa mioyo ya wengi na kulijenga Kanisa na Taifa kwa busara, unyenyekevu na imani thabiti.

Amenukuu maneno ya Biblia 2 Timotheo 4:7–8 akisema, “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda. Baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile, wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.”

Amesema Mwenyezi Mungu amjalie pumziko la milele katika ufalme wa mbinguni, na awape faraja, subira na nguvu wote walioguswa na msiba huu mzito.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, chama hicho kimeungana na Wakatoliki kuomboleza msiba huo.

Taarifa hiyo inaeleza Kardinali Pengo amekuwa na mchango katika kulihudumia Kanisa na Taifa kupitia uongozi wake wa kiroho, maadili na huduma za jamii.

“Katika miaka yake 55 ya upadri, miaka 43 ya uaskofu na miaka 28 kama kadinali, aliweka alama ya uongozi wa unyenyekevu, mshikamano wa kijamii na kujitolea kwa ustawi wa watu,” imeeleza taarifa hiyo ya CCM.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda ameandika akimshukuru Kardinali Pengo kwa baraka, upendo na amani aliyoiacha.

“Ulikuwa nguzo isiyoteteleka na msingi imara wa umoja wa kitaifa, lala salama baba wa imani. Nakuahidi sitamwacha Yesu, na maneno yote uliyoniambia nitayatunza baba, msalimie kaka yangu John Pombe Magufuli,” ameandika.


Anavyokumbukwa na Jesca

Kwa upande wa Mbunge wa Viti Maalumu CCM na mtoto wa hayati John Magufuli, Jesca Magufuli, ameandika akieleza anavyomkumbuka Kardinali Pengo alivyosimama bega kwa bega na baba yake hadi hatua ya mwisho wa uhai wake.

“Nakumbuka jinsi ulivyosimama bega kwa bega na baba yangu mpaka hatua za mwisho za uhai wake. Asante sana kwa upendo wako baba na Mungu akulaze mahali pema peponi,” ameandika Jesca.

Amenukuu kifungu cha Biblia, Warumi 14:8: “Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana; au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana.”