Kasoro tatu Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati akifungua kongamano la kwanza la kitaifa kuhusu maandalizi ya dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Juni 8, 2024.

Muktasari:

  • Wasomi na viongozi wa kisiasa wamebainisha kasoro tatu zinazoathiri utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 wakigusa ukosefu wa utawala bora, kutozingatia masuala muhimu ya nchi, na kutowashirikisha wananchi.

Dar es Salaam. Wasomi na viongozi wa kisiasa wamebainisha maeneo matatu ambayo yanakwamisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, wakitaka yafanyiwe kazi kuelekea dira mpya ya 2050.

Mambo hayo ni kutozingatiwa misingi ya utawala bora, kutozingatia masuala muhimu ya nchi na kutowashirikisha wananchi.

Wameshauri ili kuyaweka sawa kuwe na mjadala wa kitaifa kujadili dira mpya ili iakisi uhalisia wa matakwa ya wananchi.

Wameeleza hayo leo Juni 8, 2024 katika kongamano la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


Utawala bora

Akijadili kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2025, Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga amesema dira inataja utawala bora na utawala wa sheria, lakini vitu hivyo havitekelezwi.

“Tunapenda kupiga maneno matamu ambayo hayaakisi utawala bora. Kuwa na utawala bora kunahitaji uwazi na uwajibikaji, kuheshimu sheria, kuwa na taasisi imara na maamuzi yanayozingatia sheria.

“Tatizo kubwa linatokana na utamaduni uliojengeka wa kuwa na mihimili ya utawala lakini haiheshimu mgawanyo wa mamlaka na uhalisia wa uwiano,” amesema.

Akitoa mfano, Nyanduga amesema mhimili wa Dola una nguvu kubwa kiasi cha kupuuza mihimili mingine, yaani Bunge na Mahakama. 

“Imekuwa ni utamaduni, hukumu za Mahakama zinapuuzwa. Kwa mfano, Taasisi ya Msichana Initiative ilifungua kesi na kupewa hukumu inayozingatia haki za binadamu, kwamba mtoto wa kike asiingizwe katika uhusiano, mpaka leo haijatekelezwa,” amesema.

Nyanduga amesema pia hukumu ya mgombea huru ambayo mara kadhaa mahakama za ndani na nje zilisharuhusu lakini haijatekelezwa.

“Lakini unakuta Bunge ambalo ni mhimili mwingine linatunga sheria kupinga uamuzi wa Mahakama,” amesema.

Nyanduga amesema hata mchakato wa mabadiliko ya Katiba umepuuzwa.

“Kwa miaka 30 kumekuwa na michakato ya kupendekeza mchakato wa Katiba ambayo yatasahihisha matatizo haya. Michakato hii tangu enzi za Jaji (Francis) Nyalali, Jaji (Robert) Kisanga na mchakato ulioshia mwaka 2014 wa Jaji (Joseph) Warioba,” amesema.

“Michakato hii bila kurejewa na kutafuta mapendekezo yanayohakikisha utawala bora utakuwepo, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu,” amesema.

“Inakuwaje miaka nenda rudi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anachunguza kulingana na mamlaka ya kikatiba na bado anapofikisha bungeni hatuoni matendo ya kuwajibishana? Sasa utasemaje hapo kwamba kuna dhana ya uwajibikaji katika utawala bora?” amehoji.


Imekwepa maendeleo

Katika hatua nyingine, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema Dira ya 2025 haikueleza kwa undani maana ya maendeleo.

“Wanazungumzia utawala bora kwa ufinyu, wanazungumzia uwajibikaji, kutoa motisha kwa wafanyakazi bora na kupambana na rushwa.”

“Mambo yanayohusu demokrasia, uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari hayakuchukuliwa kwenye dira. Kwa hiyo, ina maana tulikuwa na dira ya maendeleo ambayo haikuwa na maendeleo ya siasa,” amesema.

Akizungumzia umiliki wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, Dk Mbunda amerejea historia ya uanzishwaji wa dira hizo, akisema haikumilikishwa kwa mambo ya nchi, badala yake lilikuwa ni wazo la Rais wa Benki ya Dunia wakati huo, James Wolfesohn.

“Ukisoma ile dira (ya 2025), huoni ni falsafa gani inayoiongoza. Labda ni hoja ya uliberali na ukoloni mamboleo. Pengine viongozi wetu wanakosa uadilifu, wamekuwa wabadhirifu na wala rushwa, kwa sababu labda tulichukua yale bila kuingiza ya kwetu,” amesema.

Awali, akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Profesa wa Sheria Issa Shivji amesema kwa muda mrefu nchi za Afrika zimegeuzwa maabara ya majaribio ya mipango ya maendeleo na nchi zilizoendelea kwa kupanga programu za marekebisho (SAPs).

“Safari hii tusikubali kufanyiwa majaribio. Majaribio yaliyofanyika miaka 60 yanatosha. Katika kuandaa Dira ya Taifa letu tuwashirikishe wananchi kikamilifu, popote pale walipo, kupata maoni yao ya nchi wanayotaka, Tanzania wanayotamani. Matamanio yao yapewe kipaumbele, matakwa yao yawe wito wetu,” amesema.

Amelitaja Azimio la Arusha kuwa mfano wa Dira ya Taifa, akisema katika hilo wananchi walidhamiria kujenga nchi ya kijamaa, nchi ya usawa na isiyo na matabaka ya wafanyakazi na wasio na wafanyakazi.

“Nchi isiyo na unyonyaji, ukandamizwaji, uteswaji, nchi inayojitegemea, inayojitawala na kufanya maamuzi yake yenyewe. Mtazamo wa kifalsafa nyuma ya Azimio la Arusha ulizama kwenye msingi wa binadamu wote ni sawa,” amesema.


Ataka mjadala kitaifa

Kuhusu ushirikishwaji wa wananchi, Profesa Shivji ameitaka Serikali kutoishia kukusanya maoni yao kwa ujumbe wa simu na mitandao, kisha kuwapa wataalamu wachache kuyachakata, bali wananchi wote wajadili kwa ujumla.

“Kwa maoni yangu, dira haiwezekani bila kuwa na mjadala wa kitaifa ili kufikia mwafaka wa Taifa wa Tanzania tunayotaka.”

“Tusifanye tunayozoea, wananchi wanatoa maoni, sms, mtandao na kadhalika, halafu wataalamu ndio watachambua maoni yao, hapana. Tuwe na mjadala wa kitaifa,” amesema.

“Popote walipo wananchi, vijijini, viwandani na pengine ili kujenga mwafaka wa kitaifa wa nchi tunayotaka. Hii ndio dira yetu na mengine ya kupanga mipango ya muda mrefu na muda mfupi itafuata,” amesema.

Kuhusu hilo, kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameungana naye akisema:

“Lazima na ni muhimu kwa watu wenye kufanya maamuzi na wenye ushawishi wa kimaamuzi (viongozi wa Serikali, watumishi wa Serikali, wanasiasa wa upinzani, wafanyabiashara, watendaji wa mashirika ya umma, wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyakazi, wanasanaa, wanafunzi), wakubaliane mwafaka wa kitaifa.”

Akijadili hilo, Profesa Samuel Wangwe amesema kinachotakiwa katika dira mpya ni kila mwananchi ashirikishwe na ajiamini kwa kila kinachopangwa.

“Suala la msingi, ningetaka kuiona Tanzania mtu mmoja mmoja anajiamini na mpango uliopangwa katika halmashauri yake na nchi yake, umepangwa vile anavyotaka kuona,” amesema.

“Jamii inayojiamini tangu ngazi ya chini mpaka halmahauri inajiamini kwamba haya tuliyopanga tumeshiriki na tunaendelea kushiriki kuangalia kama yanafanyika,” amesema.

Akitahadharisha kuingiliwa na mataifa wahisani, Profesa Wangwe amesema nchi inapaswa kujitegemea na kutoendeshwa na wafadhili. 

Mwanaharakati wa haki za wanawake na mwanasiasa mkongwe, Getrude Mongella amesema Dira ya 2050 inapaswa kuleta ukombozi wa uchumi.

“Nisingependa kuona mtu na jembe la mkono, nisingependa mwanamke jikoni anapuliza moto mpaka kamasi zinamtoka,” amesema.


Ongezeko la umasikini

Profesa Ibrahim Lipumba, nguli wa uchumi na Mwenyekiti wa CUF, amesema upimwaji wa Dira ya Maendeleo inayomalizika hauakisi uhalisia.

“Umasikini hivi sasa ni asilimia 26, lakini kiwango hicho ni kwa kipimo tunachotumia ambacho mtu mzima akitumia Sh50, 000 kwa mwezi anahesabika si masikini,” amesema.

“Sasa utajiuliza hapa, Sh50,000 kwa mwezi mtu mzima kwamba unaweza kuishi, wengi tutakuwa tunajiuliza hili haliwezekani. Asilimia 48 ya Watanzania kwa kipimo cha kimataifa wanaishi kwenye umasikini. Kwa hiyo umasikini ni mkubwa zaidi kuliko ile asilimia 26,” amesema.

Ili kuondokana na umasikini katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, amesema Serikali iweke lengo la kukuza uchumi shirikishi, katika miaka 25 inayokuja ukuaji wa uchumi kwa asilimia 10.


Alichosema Dk Mpango

Akifungua kongamano hilo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametaja mambo makuu matano, ikiwemo tatizo la ajira kwa vijana akisema yanapaswa kuingizwa katika maandalizi ya dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Amesema dira ya mwaka 2050 lazima ijengwe kutokana na dira ya 2025 iliyopo mbioni kumalizika, ibainishe kwa undani changamoto kuu za ndani na nje, ijenge uelewa wa pamoja wa misingi ya mikakati endelevu ya kuhakikisha ulinzi wa Taifa na mipaka na kujikita katika utafiti.

“Kwa maana hiyo dira ya 2050 lazima itambue mahitaji hayo na ibebe matamanio ya kundi hilo kubwa la watu wetu, ni muhimu dira hiyo ikabainisha fursa na changamoto za muundo na mwenendo wa idadi ya watu katika Taifa letu,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipangme tangu mwaka jana Watanzania 800,000 walitoa maoni kuhusu dira hiyo kwa kwa njia mbalimbali.

“Tulianza maoni kwa njia ya simu ya mkononi na kupitia mitandao, watu wengi wamejitokeza kati yao wengi ni vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 ambao ni asilimia 80 ya wote waliotoa maoni,” amesema.