Katiba ya Tanzania inavyoeleza baada ya Rais kufariki dunia

Katiba ya Tanzania inavyoeleza baada ya Rais kufariki dunia

Muktasari:

  • Baada ya Rais wa Tanzania John Magufuli kufariki dunia, hakuna uchaguzi mwingine unaofanyika badala yake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ataapishwa kuwa Rais kwa kipindi kilichosalia katika muhula wa miaka mitano.

Dar es Salaam. Baada ya Rais wa Tanzania John Magufuli kufariki dunia, hakuna uchaguzi mwingine unaofanyika badala yake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ataapishwa kuwa Rais kwa kipindi kilichosalia katika muhula wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 37 (5), baada ya Samia kuapishwa atashauriana na chama anachotoka (CCM) kisha atamteua mtu atakayekuwa makamu wa Rais.

Katiba

37 (5) Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais

kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu

kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa

kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais

ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi

cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya

40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka

Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na

uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua

asilimia hamsini ya Wabunge wote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kifo cha Rais Magufuli, zilitangazwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo akisema Magufuli alifariki dunia saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo baada ya kulazwa katika hospitali hiyo tangu Machi 6.