KCMC yaanza upasuaji wa mgongo, ubongo
Muktasari:
- Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kaskazini (KCMC) wameanzisha ushirikiano wa kutoa huduma za kibingwa za upasuaji wa uti wa mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu.
Moshi. Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kaskazini (KCMC) wameanzisha ushirikiano wa kutoa huduma za kibingwa za upasuaji wa uti wa mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu.
Lengo ni kupunguza adha ya msongamano wa wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda jijini Dar es Salaam na nchi za nje.
Hayo yameelezwa na leo Jumamosi Februari 7, 2021 na mkurugenzi mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface wakati wakiendesha shughuli ya upasuaji wa mgonjwa wa tatu wa uti wa mgongo tangu walioanza huduma hiyo.
Amesema wamekuwa wakipewa rufaa nyingi kutoka Kanda ya Kaskazini na kwamba ushirikiano huo utasaidia kumaliza changamoto ya watu kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kibingwa.
Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya mifupa na uti wa mgongo KCMC, Honest Massawe amesema hospitali hiyo ina uhitaji mkubwa wa wataalamu waliobobea wa magonjwa hayo kwa maelezo kuwa wagonjwa ni wengi.
"Ushirikiano wetu na Moi utasaidia kupunguza rufaa tulizokuwa tukizitoa kwa wagonjwa wanaofika hapa kwa ajili ya matibabu ya kibingwa, kwa wiki tulikuwa tukitoa rufaa kwa wagonjwa watano kwenda kupata matibabu ya kibingwa katika taasisi ya Moi na India kwa kuwa hatuna wataalamu wa kutosha wenye vigezo hivi," amesema Dk Masawe