Kenya yaahidi kuboresha undugu na Tanzania kukuza uchumi wa nchi mbili

Friday April 30 2021
KENYAPIC

Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati John Magufuli na Balozi wa Kenya nchini Dan Kazungu wakiwa wameshika picha aliyopiga yeye na Ra

Uhusiano baina ya Tanzania na Kenya umekuwapo kwa muda mrefu na mataifa haya yamekuwa na mitazamo sawa kwenye maeneo ya utawala wa sheria, uhuru, maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na utawala bora.

Lakini kama haitoshi, mataifa haya yote yana historia inayofanana, yakiwa yamewahi kutawaliwa na Waingereza na kujipatia uhuru katika miaka ya 1960, Tanzania ikitangulia Desemba 1961 na baadaye Kenya Desemba 1963.

Uhusiano huo bado yameendelea mpaka leo hii, na kuzaa udugu ambapo Watanzania wamekuwa wakiishi vyema na Wakenya ndani na nje ya mipaka ya nchi zao.

Udugu huo umedhihirika hata kwa viongozi wakuu wa nchi hizi, utakumbuka ulianza tangu enzi za waasisi Mwalimu Nyerere na Jomo Kenyatta, mpaka Hayati Magufuli na Uhuru Kenyatta.

Utakumbuka mwezi Machi, Tanzania baada ya kupata msiba wa aliyekuwa Rais wake, Hayati John Pombe Magufuli, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alikuwa miongoni mwa viongozi wa nchi za Afrika waliohudhuria msiba huo na ambaye pia aliahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania hata baada ya kuapishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Gazeti hili limefanya mahojiano na Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa nchi hizi mbili na alizungumza haya:-

Advertisement

Swali: Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla imekumbwa na huzuni kubwa kufuatia kifo cha Hayati Magufuli. Kenya kama moja ya mataifa ndugu wa Tanzania mlizipokeaje taarifa za kifo cha kiongozi huyu mzalendo?

Jibu: Kwanza kabisa naomba kuchukua fursa hii kutoa rambirambi zetu kwa Mama Janeth, familia, jamaa na marafiki. Zaidi ya hapo rambirambi zetu ziende kwa Serikali na Watanzania wote kwa kuondokewa kwa ghafla mno kwa Rais mpendwa, mwadilifu, mwenye maono, mchapa kazi na kiongozi shupavu, Hayati Rais John Pombe Magufuli.

Tungependa pia kutuma rambirambi za pekee kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi waliofanya kazi karibu sana naye na tunawombea wote nguvu na roho ya subra wakati huu mgumu.

Kenya kama moja ya mataifa ndugu ya Tanzania tulipokea taarifa za kifo cha Rais Magufuli kwa mshtuko na huzuni nyingi sana kwa sababu hatukujua kuhusu ugonjwa uliomwandama, lakini pia Hayati Rais John Pombe Magufuli ni kipenzi cha wengi katika nchi ya Kenya. Ana marafiki wengi kule.

Isitoshe, Wakenya wengi walipenda na kufuatilia uongozi na sera zake. Rais Magufuli alikuwa Rais wa Tanzania ambaye ni kiungo muhimu katika Afrika Mashariki basi Kenya tulimwangalia kama kiongozi muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa hivyo kuondokewa na kiongozi Tanzania ni sawa na kuondokewa na kiongozi wa Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tanzania mnavyoomboleza ndivyo sisi tunavyoomboleza na kwa sababu hii, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitangaza siku saba za maombolezo na bendera kupeperushwa nusu mlingoti mpaka siku ya maziko.

Swali: Kenya mnazungumziaje juhudi za Magufuli katika kudumisha undugu na urafiki kati ya mataifa haya?

Jibu: Ijulikane kuwa Hayati Rais John Pombe Magufuli baada ya kupata hatamu za uongozi, alifanya ziara rasmi ya siku tatu nchini Kenya. Ziara hiyo ilikuwa ya manufaa, kwani ilichangia pakubwa kudumisha uhusiano wa undugu na urafiki kati ya Kenya na Tanzania.

Alipokelewa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta na waliongea mengi kuhusu mahusiano baina ya Kenya na Tanzania, na jinsi ya kuboresha maisha ya kijamii, kiuchumi na kikanda.

Pia, Rais Magufuli alishawahi kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na alipigania umoja, uhusiano, uchumi, urafiki, undugu na ushirikiano, sio tu baina ya Kenya na Tanzaia bali jumuiya nzima.

Swali: Ni zipi faida za urafiki uliokuwepo kati ya Tanzania na Kenya katika kipindi cha uongozi wa Hayati Magufuli?

Jibu: Kwanza kabisa, ni vyema Wakenya na Watanzania kujielewa kuwa wao si majirani tu, bali ni ndugu. Kuna historia ndefu ya mahusiano na ya kusaidiana katika nyanja tofauti tofauti. Pili, kumekuwa na juhudi za kudumisha biashara na uchumi.

Pia, tumekuwa na faida nyingi sana ikizingatiwa kuwa nchi zetu zimeshirikiana kwenye nyanja za kisiasa na za kikanda. Na kwa hayo yote tunashukuru juhudi za Hayati John Pombe Magufuli na ndugu yake Rais Uhuru Kenyatta kwa kufanya kazi pamoja.

Swali: Ni mambo gani ambayo Kenya itayakumbuka na kuyaenzi kutoka kwenye uongozi wa Rais Magufuli?

Jibu: Kenya inauenzi uongozi wa Rais Magufuli hasa ikizingatiwa jinsi yeye alivyoonyesha uzalendo wa hali ya juu. Alipenda Watanzania na nchi yake Tanzania. Alikuwa mzalendo. Alikuwa kiongozi mwenye maono, ari kubwa na mchapa kazi.

Alithibiti shughuli za Serikali na za umma na alisisitiza sana kudumisha uchumi wa Tanzania na Watanzania. Ndipo Tanzania ikafika uchumi wa kati miaka mitano kabla ya malengo yake.

Mwisho kabisa Rais Magufuli alikuwa kiongozi shupavu aliyejiamini na kuamini ndoto za Uafrika kwa ujumla, zikiwemo za bara letu kujikomboa kiuchumi na kisiasa. Haya ni mambo ambayo tutayakumbuka na kuyaenzi.

Swali: Kwa namna gani Kenya itauenzi urafiki wa Rais Kenyatta na Hayati Magufuli?

Jibu: Ni ukweli usiopingika kwamba Dk Magufuli na Rais Kenyatta walikuwa zaidi ya marafiki. Walikuwa ndugu wa dhati. Rais Uhuru Kenyatta hasiti kuliambia taifa la Kenya, Wakenya na Watanzania kuwa sisi sio majirani tu; sisi ni ndugu. Rais Kenyatta haongei tu, bali anaonyesha kwa vitendo.

Ndipo Hayati Rais Magufuli alipofika Kenya kwa ziara rasmi alisisitiza akamtembelee mamake mzazi Mama Ngina Kenyatta nyumbani kwake. Vivyo hivyo, Rais Uhuru Kenyatta alipofunga safari ya kumtembelea Rais Magufuli kwake Chato, alilala kule na akapata fursa ya kumtembelea mama yake Rais Magufuli aliyekuwa anaugua.

Pia, alipata fursa ya kuonyeshwa makaburi ya familia na jamaa wa ukoo wa Rais Magufuli. Hiyo inaonyesha taswira ya undugu, si urafiki pekee. Ikumbukwe kuwa wakati wa ziara hii ya Rais Kenyatta kule Chato, alikabidhiwa zawadi maalumu, yaani tausi wanne na mwenyeji wake Rais Magufuli.

Hii ilikuwa ishara tosha ya undugu na upendo wa dhati wa hali ya juu baina ya marais hao na nchi zetu. Sote tuliyasikia maneno ya upendo ya Rais Magufuli aliposema kwamba hajawahi kutoa tausi kwa Rais yeyote bali alikuwa tayari kumkabidhi Rais Kenyatta. Huo ni upendo wa dhati na Kenya inaendelea kuuenzi uhusiano huu.

Swali: Baada ya kifo cha Dk Magufuli, Tanzania imepata Rais mpya, Samia Suluhu. Je! nini Rais Samia akitarajie kutoka Kenya?

Jibu: Kwanza ijapokuwa bado tuna huzuni kwa kumpoteza Rais Magufuli, tungependa kuchukua nafasi hii ya kipekee kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan katika wadhifa wake mpya wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunamuombea kila la heri katika majukumu yake mapya na mazito.

Rais Samia Suluhu atarajie upendo wa dhati, uhusiano wa karibu, undugu na ari ya kufanya kazi pamoja ili kubadilisha hali na maendeleo ya watu wetu, nchi zetu, ukanda wetu na jumuiya yetu.

Kama tulivyosema hapo awali, Rais Uhuru Kenyatta anawachukulia Watanzania na viongozi wao kama ndugu sio jirani. Hivyo basi itoshe tu kuwa, Kenya itafanya juhudi zote kudumisha undugu huu wenye madhumuni ya kufanya kazi pamoja na kuboresha uchumi wa nchi zetu na watu wetu.

Swali: Kuna mikakati ya kiuchumi na kimaendeleo ambayo Hayati Magufuli na Rais Kenyatta waliipanga na kwa bahati mbaya hawajafanikiwa kuitekeleza. Je! kwa namna gani Kenya itaiendeleza mikakati hiyo kwa kushirikiana na Rais Samia?

Jibu: Ni kweli, ipo baadhi ya miradi na mipango ya maendeleo ambayo ilikuwa katika mipangilio na iliyofuatiliwa kwa karibu sana na viongozi hawa. Mfano mmoja ni barabara mpya kutoka Malindi, Kenya mpaka Bagamoyo kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (Africa Development Bank) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

NYAPICCC

Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati John Magufuli akizungumza pembeni ya Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta wakati wa ziara yake nc

Mradi mwingine ni mpangilio wa kuunganisha umeme kati ya Kenya na Tanzania. Ijapokuwa Rais Magufuli hayupo tena tunaamini kuwa, chini ya uongozi wa Rais Samia, miradi hii na mingineyo itafanikishwa.

Swali: Kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi na Hayati Magufuli kama Makamu wa Rais, Kenya mnamzungumziaje Rais Samia na nini matarajio yenu kwake?

Jibu: Kenya inamheshimu sana Rais Samia na itaendelea kumpa heshima zote kama Rais wa taifa hili. Rais Kenyatta anamchukulia Rais Samia kama dada yake. Hii inaashiria kuwa yuko tayari kujenga uhusiano wa karibu naye kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu.

Matarajio yetu ni hawa viongozi wetu washirikiane na kufanya kazi pamoja ili kuzistawisha nchi zetu, na Jumuiya yetu, ikizingatiwa kuwa umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.

Tukiungana kama Wakenya na Watanzania, hakuna chochote ambacho kitaweza kutuzuia kufanikisha malengo yetu, na juhudi zetu za kuimarisha uchumi wetu.

Advertisement