Kesi ya Profesa Mahalu, Grace hatua kwa hatua

Tuesday May 04 2021
profesamahalupic

Profesa Ricky Costa Mahalu

By James Magai

Dar es Salaam. Kuna kesi nyingi kubwa zinazohusisha watu maarufu zilizowahi kufunguliwa na kuamuliwa kwa nyakati tofauti katika historia ya mahakama Tanzania.
Moja ya kesi hizo ni ile ya uhujumu uchumi iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Ricky Costa Mahalu, mtaalamu nguli wa sheria na anayetajwa kuwa rafiki wa aliyekuwa Rais wa Tatu wa Tanzania, Hayati Benjamini William Mkapa.
Profesa Mahalu pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin walishitakiwa mwaka 2007, wakidaiwa kula njama, kutumia nyaraka za manunuzi ya jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia ili kumdanganya mwajiri wao (Serikali).
Walishitakiwa pia kwa wizi wa Euro 2,065,827 (zaidi ya Sh2.5 bilioni wakati huo) na kuisababishia Serikali hasara. Kushitakiwa kwa Profesa Mahalu ambaye aliwahi kuwa Mhadhiri na Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuliwasitua wengi. Watu wa karibu yake waliamini kesi ile ilitokana na figisu figisu za kisiasa.
Waliomshitaki walidai wamejiridhisha kuwa walikuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashitaka dhidi ya watumishi hao wa umma.
Moja ya tukio kubwa katika kesi hiyo ni pale Rais Mkapa alipoamua kuweka kando ukuu na heshima iliyoambatana na kuwahi kuwa Rais kwenda kusimama kizimbani kumtetea Profesa Mahalu.
Ni miaka 12 imepita sasa tangu kumalizika kwa kesi hiyo na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumwachia huru Profesa Mahalu na mwenzake. Pamoja na kuwa kesi hiyo iliisha miaka mingi iliyopita, kumbukumbu yake imebakia kwenye vichwa vya wengi na kuacha rekodi ya pekee katika historia ya mahakama Tanzania.
Moja ya jambo la kipekee katika kesi hiyo ni aina ya mashahidi waliotajwa katika kesi hiyo, hasa upande wa utetezi.
Mbali ya Rais Mkapa, mashahidi wengine waliotajwa kuja kusimama kizimbani kama mashahidi wa utetezi ni pamoja na Rais aliyekuwa madarakani wakati huo, Jakaya Kikwete na hayati John Magufuli ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ujenzi.
Kinachoipa kesi hiyo upekee mkubwa ni pale Rais Mkapa aliposimama kizimbani na kutoa ushahidi uliokinzana na ule wa Jamhuri, akiamini Profesa Mahalu na wenzake hawakuwa na hatia.
Uamuzi wa Rais Mkapa uliweka rekodi mbili kwa wakati mmoja. Kwanza, uliifanya kesi hiyo kuwa ya kwanza nchini kuwa na shahidi aliyewahi kushika nafasi ya ukuu wa nchi. Pili, ni kitendo cha aliyewahi kuwa mkuu wa nchi kutoa ushahidi uliokinzana na Serikali aliyowahi kuiongoza.
Hadi kesi hiyo inakwisha, si Kikwete wala Magufuli walifika mahakamani kutoa ushahidi kama walivyotajwa awali na upande wa utetezi.
Nini ulikuwa msingi wa mashtaka dhidi ya Profesa Mahalu na mwenzake? Nini ulikuwa utetezi wao? Kwa nini Rais Mkapa aliamua kwenda mahakamani kutoa ushahidi na ni nini alichokisema? Nini ulikuwa uamuzi wa mahakama? Endelea kufuatilia sehemu ya simulizi za kesi hiyo na kupata majibu wa maswali hayo….

Msingi wa mashitaka
Profesa Mahalu na mwenzake walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Januari 22, 2007. Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 01 ya mwaka 2007, Profesa Mahalu na mwenzake walisomewa mashtaka sita.
Mashtaka hayo yalikuwa ni pamoja na kula njama, kutumia nyaraka za manunuzi ya jengo la ubalozi ili kumdanganya mwajiri wao (Serikali), wizi wa Euro 2,065,827 (zaidi ya Sh2.5 bilioni wakati huo) na kuisababishia Serikali hasara. Walidaiwa kutenda makosa hayo Oktoba Mosi, 2002 wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italy lililoko mtaa wa Vialle Cortina d’Ampezzo 185 mjini Rome.
Ilidaiwa kuwa ununuzi ya jengo la ofisi hiyo ya balozi ulifanyika kwa kutumia mikataba miwili tofauti iliyotekelezwa siku moja lakini ikiwa na bei tofauti. Ununuzi huo ulidaiwa pia kutohusisha baadhi ya taratibu za manunuzi za Serikali.
 
Utetezi wa Profesa Mahalu, Martin
 Katika utetezi wake, Profesa Mahalu alikana mashtaka hayo na kudai kuwa alipofika katika ubalozi huo alikuta ofisi hizo zikiwa na hali mbaya, hali iliyosababisha kutoa fedha zake za mfukoni na kununua samani zenye hadhi ya ofisi ya ubalozi.
 Alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete, wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pia alifika katika ofisi za ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya na kwamba aliunga mkono hoja yake kuwa ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi.
Alisema mwanzoni mwa Juni, 2001, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alimpigia simu akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya kutaka kila ofisi ya ubalozi inunue jengo lake, itapitishwa na Bunge.
Alidai kuwa Katibu Mkuu alimtaka yeye na maofisa wengine wa ubalozi kuanza kutafuta majengo. Alisema baada ya hapo aliwaagiza maofisa wake kwenda kutafuta majengo ndani na nje ya Jiji la Rome kwa ajili ya kulinunua.
 Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya jengo hilo kupatikana, Rais Kikwete alitia saini kuridhia bei ya ununuzi wa jengo hilo ya Euro 3,098,741.58 na alitetea uamuzi wake huo alipoliambia Bunge Agosti 3, 2004.
“Wakati wa Mkutano wa 16 wa Bunge, kikao cha 39 kilichofanyika Agosti 3, 2004, Kikwete alithibitisha kuwa jengo hilo liligharimu Euro 3,098,741.58 kwa kuanzia,” alisema Mahalu na kuendelea:
“Mheshimiwa hili linaweza kuthibitika ukisoma kumbukumbu za Bunge za kitabu cha mwaka 2004 ukurasa wa 169 aya ya pili,” alisema Profesa Mahalu huku akinukuu aya hiyo: “Mwaka 2001/2002 Wizara ilinunua jengo Roma kuondokana na adha ya kupanga nyumba za watu na kulipa kila mwaka. Machi 16, 2002 ilitoa hundi ya kwanza ya malipo Euro700 kati ya Euro 3,098,741.58.”
Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Profesa Mahalu ambaye alikuwa amebeba  kabrasha kubwa la vielelezo, alitoa nyaraka mbalimbali zilizokuwa zimejaa kwenye kabrasha hilo.
Nyaraka hizo zilionyesha hatua mbalimbali za mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, ikiwemo barua ya kwanza iliyoonyesha mchanganuo wa ununuzi wa jengo ambazo alizikabidhi serikalini.
Profesa Mahalu alidai kuwa Septemba 2001, Waziri huyo wa Mambo ya Nje (Kikwete) alimpa nguvu ya kisheria ya uwakilishi (special power of attorney) ya ununuzi wa jengo hilo la ubalozi.
“Aliniagiza kununua jengo hilo la ubalozi lililopendekezwa na Serikali na Machi 24, 2004, nilimwandikia barua Kikwete na kwenye barua hiyo niliambatanisha nyaraka za ununuzi wa jengo hilo baada ya kulinunua,” alisema Balozi Mahalu.
 Profesa Mahalu alidai mbali ya kumwandikia Kikwete, pia aliipeleka barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi, pamoja na kwa Waziri wa Fedha.
Alieleza kuwa katika ununuzi wa jengo hilo kulikuwepo na mikataba miwili ambayo Serikali iliridhia, yaani mmoja wa bei rasmi na mwingine wa bei isiyo rasmi.
Balozi Mahalu pia alidai kuwa upande wa mashtaka haukueleza kama mama mwenye jengo hilo la ubalozi lililonunuliwa alikuwa amelipwa fedha pungufu ya bei iliyokubaliwa au aliwahi kupeleka malalamiko kuwa hakuwahi kulipwa malipo yake.
Alihitimisha utetezi wake kwa kusisitiza kuwa yeye si mbadhirifu kama anavyoshtakiwa. Na kwa kuithibitishia mahakama hilo, alitoa nishani na tuzo mbalimbali alizowahi kutunukiwa nchini Italia kutokana na uaminifu na utendaji kazi mzuri wa kuboresha uhusiano kati ya Tanzania na nchi hiyo.
 Kwa upande wake, Grace Martin alidai kuwa Balozi Mahalu hakuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta faida kwa taifa kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.
Akiongozwa na Marando kutoa utetezi wake, Grace alidai: “Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, Balozi Mahalu hakutenda mashtaka yote sita yanayomkabili, aliwasilisha mikataba miwili kama taarifa iliyofanyika kihalali.”
Pia alihoji sababu ya upande wa Jamhuri kutomleta mmiliki wa jengo hilo la ubalozi kukana risiti hiyo au Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kuulizwa juu ya ununuzi wa jengo hilo kwa kuwa walikwenda nchini humo kufanya uchunguzi.

Je, nini kiliendelea? Endelea kufuatilia simulizi ya kesi hii ya kusisimua kesho.

Advertisement