Kesi ya Sabaya yakwama, kisa vibali vya DPP bado

Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (wa pili kushoto) akizungumza na mama yake mzazi Vida Sabaya, wakitoka katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, baada ya kesi yake kuahirishwa, juzi. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Upande wa mashitaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya,umesema kuwa utawasilisha vibali kutoka kwa mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.

Moshi. Upande wa mashitaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya,umesema kuwa utawasilisha vibali kutoka kwa mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.

Wakili wa Serikali, Susan Kimaro juzi aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi chini ya Hakimu Mfawidhi Salome Mshasha, kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo akaomba tarehe nyingine ya kutajwa ili waweze kuwasilisha vibali hivyo.

Kulingana na taratibu za kisheria, makosa ya uhujumu yanayomkabili Sabaya yanasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, isipokuwa yanaweza kusikilizwa na mahakama ya Hakimu Mkazi endapo DPP ataipa mahakama hiyo kibali.

Kutokana na ombi hili, wakili wa utetezi, Hellen Mahuna anayesaidiana na wakili, Emmanuel Antony, alisema wao hawana kipingamizi lakini wakili Antony yeye akahoji kama hati ya mashitaka ya awali ndio ambayo itatumika kwenye usikilizaji.

Akijibu suala hilo, Hakimu Mshasha aliwataka mawakili hao wasubiri upande wa mashitaka uwasilishe nyaraka hizo kwanza ndio suala hilo litaweza kufahamika na akapanga Novemba 7, 2022 kuwa ndio siku kesi hiyo itatajwa tena mahakamani.

Utaratibu wa kisheria ni kuwa siku hiyo, kama vibali vitakuwa vimewasilishwa, upande wa mashitaka unaweza kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali (PH) kama watakuwa tayari, au kuomba tarehe nyingine itakayotumika kumsomea PH.

Jana Sabaya alitimiza siku 145 akiwa mahabusu gereza la Karanga tangu afikishwe mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 1, 2022 akiwa na washitakiwa wenzake wanne ambao hata hivyo waliachiwa baada ya kukiri makosa na kulipa faini.

Sabaya anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi inayohusisha kuunda genge la uhalifu, kutumia vibaya madaraka yake na kujipatia Sh30 milioni huku wakijua wakati wanazipokea, zilikuwa ni zao la uhalifu ambalo ni rushwa.

Juni Mosi mwaka huu, Sabaya na wenzake wanne walipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwa mara ya kwanza na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi iliyohusisha kuunda genge la uhalifu,kutumia vibaya madaraka, na kudai rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Alex Swai.

Hata hivyo, Septemba 6 mwaka huu, mahakama hiyo iliwaachia huru washitakiwa wanne ambao ni Sylivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey, baada ya kukiri makosa yao na mahakama kuwahumu kulipa kila mmoja faini ya Sh50,000 na fidia ya Sh1 milioni kwa mwathirika.