Kichanga chaokotwa kikiwa kimefariki Njoro, wananchi walaani
Mwili wa kichanga ukiwa umefunikwa na wasamaria wema baada ya mwanamke asiyefahamika kutelekeza kichanga hicho eneo lisilo na makazi ya watu.
Muktasari:
- Kichanga hicho chenye jinsia ya kike kimeokotwa leo Machi 3, 2026 katika eneo lisilo na makazi ya watu, mtaa wa Viwanda, kata ya Njoro Manispaa ya Moshi kikiwa hakijafunikwa hali ambayo imewaumiza wananchi waliofika katika eneo hilo.
Moshi. Katika hali ya kusikitisha, kichanga cha kike kimeokotwa kikiwa kimetelekezwa katika eneo lisilo na makazi ya watu, mtaa wa Viwanda, kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi.
Tukio hilo limewashtua wananchi wa eneo hilo, huku baadhi yao wakilaani vikali kitendo hicho na kueleza masikitiko yao juu ya tukio hilo la kusikitisha.
Kichanga hicho kimeokotwa leo Jumanne, Machi 3, 2026 kikiwa tayari kimefariki dunia, ambapo mwili wa kichanga hicho umechukuliwa na Jeshi la Polisi waliofika katika eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kubaini mazingira ya tukio hilo.
Akizungumza mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Monica Assey amesema tukio hilo ni la kikatili, la kinyama na linapaswa kukemewa vikali na jamii kwani linaumiza na kuacha simanzi kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
"Hili tukio ni tukio baya sana na ni chukizo mbele ya Mungu, yaani binadamu tumekuwa wakatili sana, inauma sana jamani," amesema Monica.
Baadhi ya askari waliovaa kiraia wakiwa wamebeba mwili wa kichanga, ambao ulitelekezwa mtaa wa Viwanda, kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mkazi mwingine, Adam Mnango, amesema tukio hilo limeumiza hisia za wengi na kwamba jamii inapaswa kutafakari kwa kina kuhusu matukio ya aina hiyo, ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.
“Nimeumia sana, huu ni ukatili uliopitiliza. Inaumiza sana,” amesema.
Kwa upande wake, kiongozi wa serikali ya mtaa huo, William Kavishe, amelaani tukio hilo na kutoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwasaidia wasichana wanaopata ujauzito usiotarajiwa badala ya kuwatelekeza au kuwanyanyapaa.
“Wazazi tukae karibu na watoto wetu. Ikitokea mimba isiyotarajiwa, tusitupe watoto. Waje hata katika uongozi wa serikali ya mtaa, tutajua namna ya kusaidia. Kutupa mtoto si suluhisho, ni kitendo kisichokubalika katika jamii,” amesema Kavishe.