Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kidato cha pili bado mwiba kwa wanafunzi Tanzania

Muktasari:

  • Baadhi ya wanaopaswa kurudia darasa wamekuwa wakiona aibu kusoma na waliokuwa nyuma yao, huku kuacha shule ikiwa ni chaguo wengine wakihisi hawana akili za kumudu maisha hivyo kutafuta njia nyingine za kujiendeleza kimaisha.

Dar es Salaam. Aibu, kutojiamini na kuhisi hawana akili vimetajwa kuwa miongoni mwa vitu vinavyowakumba wanafunzi waorudia darasa jambo linalochochea baadhi kukacha masomo.

Kurudia darasa kunatajwa kuchangiwa na maandalizi duni wanayopata wanafunzi wanapokuwa ngazi ya msingi jambo linalofanya washindwe kumudu masomo ya sekondari.

Ripoti ya Best Education 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la wanafunzi wa kidato cha pili wanaorudia darasa kati ya mwaka 2019 hadi 2024.

Wakati wanaorudia kidato cha pili wakiongezeka, wanafunzi wa darasa la nne ambao nao walikuwa vinara wa kurudia darasa idadi yao imepungua.

Kwa mujibu wa takwimu, mwaka 2019 wanafunzi 24,426 wa kidato cha pili walirudia masomo ambao waliongezeka hadi kufikia 48,334 mwaka 2023 na 53,615 mwaka 2024.

Idadi ya waliorudia kidato cha pili katika ripoti ya 2024 inabeba asilimia 92.6 ya wanafunzi wote waliorudisha darasa (kidato cha kwanza hadi cha nne) mwaka 2024.

Wakati darasa hilo lenye mtihani wa upimaji kwa kiasi kidgo likionekana kuendelea kuwa mwiba kwa wanafunzi, upande wa shule msingi wale wa darasa la nne nalo hali ni ileile.

Takwimu zinaonyesha kupanda na kushuka kwa wanafunzi wanaorudia mtihani huo kati ya mwaka 2019 hadi 2024.

Mwaka 2019, wanafunzi wa darasa la nne waliorudia walikuwa 60,470 idadi ambayo ilipaa mara tatu zaidi hadi kufikia wanafunzi 209,503 mwaka 2023.

Hatahivyo, inaonekana kulikuwapo na jitihada mbalimbali zilizofanyika ndani ya mwaka mmoja na hatimaye idadi ya walioshindwa kuendelea darasa la tano mwaka 2024 ilishuka hadi kufikia wanafunzi 151,117 ikilinganishwa na namba iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Mbali na kuwa na wanafunzi wengi wanaorudia, madarasa haya pia ndiyo yaliyobeba asilimia kubwa ya wanafunzi waliokacha masomo mwaka 2024.


Kinachosababisha

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Idara ya Uchechemuzi Shirika la Uwezo Tanzania, Greyson Mgoi amesema mujibu wa Mgoi suala la kurudia darasa humuathiri mtoto na kumfanya asijisikie raha kusoma darasa analotakiwa kuwapo.

“Mfano darasani mko 100, ila nyie wawili mmerudia mnakosa morali ya kusoma, mwingine akiambiwa arudie anaona aibu kwenda kusoma na wadogo zake yeye akionekana mkubwa,” amesema Mgoi.

Alipendekeza suala hilo linaweza kudhibitiwa kwa kuwekwa kwa utaratibu utakaowawezesha wanafunzi kurudia darasa katika shule nyingine karibu yake ambayo taarifa zao hazijulikani

“Tofauti na hapo mtoto huhisi hana akili kumbe huenda hakupata mwalimu mzuri wa kumsaidia ili aweze kumudu masomo yake ipasavyo,” amesema Mgoi.

Akizitaja sababu za mwanafunzi kufeli masomo, Mgoi amesema kunachochewa na msingi duni waliotoka nao katika ngazi za chini

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa baadhi ya tafiti walizowahi kuzifanya zinaonyesha kuwa baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba hawawezi kumudu kusoma hadithi za darasa la pili na hata hesabu rahisi za darasa la pili.

Amesema pia zipo baadhi ya shuhuda ambazo zilieleza kuwa kuna wanafunzi walikuwa wanajiunga kidato cha kwanza na hawajui kusoma.

Amesema wakati mwingine, njia ya upimaji iliyokuwa ikitumika katika mitihani ya kitaifa inayomtaka mwanafunzi kuchagua majibu ilikuwa haitoshi kumpima uelewa wake.

“Kwa sababu anaweza kubashiri mwisho wa siku anapata daraja A na B, tuwe na mtihani ya kupima vizuri kwenda ngazi inayofuata, hali ni mbaya huko chini,” amesema Mgoi.

Kuhusu mtihani wa upimaji, tayari Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limeshatangaza kuacha na mfumo wa mitihani ya kuchagua katika mitihani ya Taifa ya darasa la Saba ili kuboresha upimaji.

Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko amesema mara nyingi mtoto akirudia ya kwanza, akiambiwa arudie kwa mara ya pili anaamua kuacha shule kwani anaona si shule pekee inayoweza kumpa maisha.

“Anaona kabisa hawezi kumudu vizuri masomo, akirudia anashindwa kuendana na wenzake, anakuwa na aibu ya kukaa na wale aliokuwa amewatangulia,” amesema Nkoronko.

Amesema hali hiyo huifanya pia Serikali kutumia fedha nyingi kugharamia wanaorudia badala ya kufanya maboresho mengine ikiwemo ya miundombinu. Hali hiyo pia inaongeza msongamano darasani kwani inaongeza idadi ya wanafunzi ambao walipaswa kuhudumiwa awali.

“Tufanye tathmini ya ufundishaji, pia mwanafunzi kabla ya kwenda darasa lingine basi ni vyema kuhakikisha anamudu darasa analotoka kabla ya kuendelea mbele,” amesema Nkoronko.

Hali hii ndiyo iliyompata Anna Philipo ambaye sasa ni mama wa watoto wawili ambaye aliacha masomo baada ya kutakiwa kurudia kidato cha pili kwa mara nyingine tena.

“Sikuwa na akili za shule, nimefeli mara ya kwanza, ya pili, inaamana niliowaacha darasa la sita shule ndiyo nije kusoma nao siyo kweli. Mama wala baba hawakuonyesha kuchukia mimi kuacha masomo badala yake tulikuwa tunaenda shambani wote,” amesema Anna ambaye kazi yake kwa sasa ni kilimo.


Nini Kifanyike

Neema Kitundu kutoka Jukwaa la Wanawake Waafrika Wanaojihusisha na Elimu - Tanzania (Fawetz) amesema kwa sababu nchi inaingia katika mtaala wa amali, ambao unalenga mafunzo ujuzi ni vyema kusaidia walimu ili waweze kutoa mafunzo yanayoweza kusaidia watoto kufanya vizuri.

“Walimu wajengewe uwezo wa kufundisha kwa kutumia mbinu rafiki ambazo hazitamuacha mtoto yeyote nyuma kitaaluma, walimu wajengewe uwezo wa mtaala wa amali na wapewe mafunzo angalau mara moja kwa mwaka,” amesema Neema.

Wakati hayo yakifanyika pia wazazi na walezi wahamasishwe kuhusu umuhimu wa elimu ili wawatumikie watoto mahitaji muhimu ya shule lakini pia waweze kufuatilia maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao.

“Wanafunzi pia wajengewe uwezo wa kujitambua, kujiamini, kujithamini na Kujiheshimu ili waweze kushiriki kikamilifu tendo la ujifunzaji kwa malengo ya kutimiza ndoto zao,” amesema Neema.