Kifo cha Magufuli kilivyoripotiwa na vyombo vya kimataifa

Muktasari:

  • Mara tu baada ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kutangaza kifo cha Rais John Magufuli, habari zake zilianza kumiminika katika vyombo mbalimbali vya habari duniani, huku kila chombo kikiwa na namna yake ya uwasilishaji wa ujumbe huo.

Dar es Salaam. Mara tu baada ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kutangaza kifo cha Rais John Magufuli, habari zake zilianza kumiminika katika vyombo mbalimbali vya habari duniani, huku kila chombo kikiwa na namna yake ya uwasilishaji wa ujumbe huo.

Katika taarifa zake, Shirika la CNN la Marekani lilieleza kuwa Rais Magufuli amefariki dunia ikiwa ni wiki kadhaa baada ya kutoonekana kwake hadharani.

Shirika hilo lilimnukuu Makamu wa Rais likimtaja kama Kaimu Rais, anayetarajiwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke.

Nalo Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) liliripoti kuwa Tanzania imeingia katika maombolezo kufuatia kifo cha Rais Magufuli baada ya wiki kadhaa za wasiwasi zilizoacha mawazo tofauti kuhusu aina yake ya utawala.

Ilisema tangazo la kifo chake lilitolewa na Makamu wa Rais baada ya Serikali kuchukua muda ikisita kueleza hali yake kwa takriban wiki tatu ambazo zilizua wasiwasi kuwa amekwenda kutibiwa nje.

Katika kipindi hicho, AFP ilisema watu kadhaa walikamatwa wiki hii kwa kusambaza uvumi kuhusu afya ya Rais Magufuli katika mitandao ya kijamii.

Vilevile Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilichapisha makala maalumu kuhusu Magufuli likimtaja kama mtoto wa mkulima, kiongozi ambaye amevuta hisia mseto hasa katika siku za hivi karibuni kutokana na msimamo wake kuhusu corona.

Makala hiyo ilikumbusha alivyopachikwa jina la ‘tingatinga’ kutokana na namna alivyosimamia mipango ya ujenzi wa barabara nchi nzima akiwa Waziri wa Ujenzi, msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi na kuchukizwa na uharibifu wa fedha za umma huku akishutumiwa kwa kukandamiza wakosoaji wake na kuminya uhuru wa kujieleza

Iliongeza: “Tangu Juni 2020 alipotangaza kuwa Tanzania haina corona, Rais huyo na viongozi wengine wa Serikali walionekana kutilia shaka ufanisi wa matumizi ya barakoa na ubora wa vipimo vya corona.”