Kifungoni kisa wivu wa mapenzi

Kifungoni kisa wivu wa mapenzi

Muktasari:

Mume aliamua kumpiga mkewe baada ya kugundua kuwa alikuwa akiishi na mwanamume mwingine.

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo ya Buguruni imemhukumu kifungo cha nje cha miezi minne mkazi wa Tabata Segerea, Baraka Athuman (33) baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga mke wake Kuluthum Khamis kwa kutumia mwiko wa ugali kutokana na wivu wa mapenzi.

Pia, mahakama hiyo imemwamuru mshtakiwa amlipe mkewe huyo kiasi cha Sh20,000 kama fidia ya matibabu

Akitoa hukumu hiyo juzi Hakimu, Gladness Njau alisema ushahidi uliotolewa na mlalamikaji pamoja na mume wake Athumani kukiri mahakamani hapo kumpiga Kurutum sehemu mbalimbali ya mwili wake, ulitosha kumtia hatiani. Alidaiwa kumpiga kwa mwiko wa ugali baada ya kumfumania akiishi na mwanaume mwingine.

Alisema kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mlalamikaji pamoja na mshtakiwa mwenyewe mahakama hiyo imejiridhisha kuwa ni kweli alimpiga Kurutum sehemu mbalimbali ya mwili wake na kumsababishia maumivu makali mahakama hiyo inamtia hatiani.

Utetezi wake ulivyokuwa

Njau alisema katika utetezi wa mshtakiwa Athuman aliotoa mahakamani hapo alidai ni kweli alimpiga mke wake kutokana na wivu wa mapenzi.

Athuman ambaye ni dereva wa magari makubwa alidai mke wake alifunga naye ndoa mwaka 2014 na walifanikiwa kuishi miaka sita Oktoba 27 mwaka 2020 saa 3 asubuhi Kuluthum alimweleza anaenda kazini alikuwa anauza duka la dawa ndipo alimwambia asiende kwa kuwa siku hiyo alitaka washinde wote nyumbani.

Mshtakiwa huyo alidai baada ya kumweleza hayo mke wake alimkatalia na kudai anaelekea kazini, ndipo alimwambia akitoka ndani ya nyumba hiyo atoke na nguo zake.

Athuman alidai baada ya kumweleza hayo mke wake alichukua nguo zake na kutoka nazo nje na kuondoka hivyo alitegemea angerudi nyumbani hapo.

Alidai alitegemea mke wake ameenda kukaa kwa ndugu zake na alipofuatilia alibaini hayupo ndipo alianza kumfuatilia ili kujua anaishi wapi.

Mshtakiwa huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa Januari 21 mwaka huu alibaini mke wake anaishi na mwanaume mwingine eneo la Tabata Bima ndipo alipoamua aliamua kwenda ili akamfumanie.

Alidai alipofika kwenye nyumba hiyo na kumgongea alitoka huku akiwa amevaa kanga moja ndipo alianza kumpiga kwa kutumia mwiko wa ugali.

Alichosema Kuluthum

Hakimu Njau alisema ushahidi uliotolewa na Kuluthum, alidai Oktoba 27 mwaka 2020 mume wake alimuacha kwa maneno bila ya kuandikishiana sehemu yeyote baada ya kumkatalia kubaki nyumbani ili washinde pamoja.

Mlalamikaji huyo alidai siku hiyo alipokuwa akijiandaa kwenda kazini alimwambia asiende kazini akitoka kwenye nyumba hiyo yeye siyo mke wake ndipo aliamua kuchukua nguo zake na kuondoka nazo.

Alidai alimshangaa mshtakiwa huyo kuendelea kumfuatilia wakati walishaachana, kwani alimtamkia kuwa endapo atakatoka ndani ya nyumba hiyo yeye siyo mke wake.

Kuluthum alidai siku ya tukio mshtakiwa huyo alimgongea mlango na alipofungua akaanza kumpiga na mwiko wa ugali sehemu mbalimbali na kumsababishia mkono wake kuteguka.

Alidai wakati akiendelea kupigwa mshtakiwa huyo alikuwa anamlazimisha ampigie mwanaume ambaye anaishi naye ili aongee naye.

Wakati akilazimisha hayo ndipo jirani yake alienda kutoa taarifa kwa mjumbe wa serikali ya mtaa huo.

Kuluthum alidai baada ya kipigo hicho alienda polisi na kupewa fomu ya matibabu P3 ya polisi na alipoenda hospitali alitibiwa kwa gharama zaidi ya Sh10,000.

Hakimu Njau alisema kifungu cha 240 Sura ya 16 ya kanuni ya adhabu inasema mtu yeyote ambaye bila uhalali anamshambulia mtu mwingine, atakuwa ametenda kosa na kifungo chake ni mwaka mmoja

Alisema: ‘‘Kutokana mlalamikaji kuwa ni mwanandoa, mahakama imeangalia hilo, hivyo inakuhukumu mshtakiwa kifungo cha nje cha miezi minne na hutakiwi kufanya chochote katika kipindi hicho.

Pia mahakama hiyo imemwamuru mshtakiwa kumlipa kiasi cha Sh20,000 ikiwa ni fidia ya gharama alizotumia hospitali wakati anajiuguza majeraha yaliyotokana na kipigo hicho.