Kiingereza cha Musukuma bungeni chaibua vicheko

Muktasari:

  • Kitendo cha mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu ‘Musukuma’ kunyoosha mkono na kumuuliza swali la kiingereza kwa mgombea ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), Habib Mnyaa kimeibua shangwe katika kikao cha Bunge.


Dar es Salaam.  Kitendo cha mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu ‘Musukuma’ kunyoosha mkono na kumuuliza swali la kiingereza kwa mgombea ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), Habib Mnyaa kimeibua shangwe katika kikao cha Bunge.

Katika kikao cha Bunge la leo Alhamisi Septemba 22, 2022 kunafanyika uchaguzi wa kuwapata wabunge tisa wa Eala watakaoiwakilishi Tanzania katika jumuiya hiyo.

Musukuma ambaye anatajwa kuwa na elimu ya darasa la saba, amepewa nafasi ya kuuliza swali na Dk Tulia baada ya mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka kumaliza kuuliza maswali.

Shangwe zilianza kuibuka baada ya Dk Tulia kutaja jina la Musukuma kwamba ndiye atakayeuliza swali.



Baada ya kupewa nafasi hiyo, Msukuma alisema, “thank you madame Spika (Dk Tulia) for give me this chance, Mr Mnyaa I want to ask you one question, where are you, (ulikuwa wapi) what did you do for last five years? (ulikuwa unafanya nini ndani ya miaka mitano iliyopita) Swali liliongeza vicheko zaidi kwa wabunge hasa waliokuwa wamekaa karibu na mbunge huyo.

Hata hivyo, shangwe zilizidi kuwa kubwa hatua iliyomlazimu, Dk Tulia kuwataka wabunge kuwa watulivu huku akimuuliza Mnyaa kama amesikia vizuri swali la Musukuma. Hata hivyo, Dk Tulia aliwakata wabunge kukaa kimya na kumuamuru Msukuma alirudie swali lake kwa mara nyingine.

Alipopewa nafasi Musukuma alimuuliza Mnyaa, “what did you do for last five years baada ya kumaliza kuuliza swali hilo, wabunge waliendelea kumpigia makofi mbunge huyo wa Geita Vijijini huku akionekana kutunzwa fedha za noti ya Sh10,000 na baadhi ya wabunge wenzake.

Katika kuweka mambo sawa, Dk Tulia ambaye ni mbunge wa Mbeya Mjini alinyoosha swali hilo kwa kusema ‘what did you do for past five years.

Akijibu swali hilo Mnyaa amesema, “nilikuwa nafanya kazi katika Bunge Eala kupitia kamati na nilifanya vitu vingi sana nikishirikiana na wenzangu katika miaka mitano iliyopita. Nasimama mbele yenu nikiomba kura zenu.