Kijiji chawakatia bima ya afya wakazi wake wote

Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka akikabidhi kadi ya bima ya afya kwa mwananchi wa kijiji cha Mundindi kilichopo wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Muktasari:
- Wakazi 3,149 wa Kijiji Cha Mundindi wilayani Ludewa wamepatiwa bima ya afya, baada ya kupata fidia kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma na kuamua kununua hati fungani iliyowawezesha kupata faida na kukata bima ya afya kwa wakazi wote.
Njombe. Wananchi 3,149 wa kijiji cha Mundindi kilichopo Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wametengeneza historia ya kipekee baada ya Serikali ya kijiji hicho kuwakatia bima ya afya wanakijiji wote ili waweze kupata huduma ya afya bila kikwazo cha fedha.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali kulipa fidia Sh15 bilioni ili kupisha miradi ya Liganga na Mchuchuma ambapo kijiji hicho kilikuwa na eneo katika eneo la mradi huo na kukiwezesha kupata fidia ya Sh464 milioni.
Kati ya fedha hizo, na Sh400 milioni kijiji kiliamua kununua hati fungani katika moja ya taasisi ya kifedha hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo Julai 12, 2024 na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundindi, Sapi Mlelwa wakati wa hafla ya kuwakabidhi kadi za bima ya afya wananchi hao, iliyofanyika kijijini hapo.
Amesema kiasi hicho cha Sh400 milioni walichonunua bondi ya hati fungani, kinawawezesha kijiji hicho chenye kaya 524, kupata gawio la Sh41 milioni kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
Amesema katika gawio la kwanza, wanakijiji walikubaliana kulipiana bima ya afya ambayo thamani yake ni Sh12.9 milioni.
“Serikali ya kijiji kwa kushirikiana na diwani wa kata hii, Wise Mgina pamoja na viongozi wengine wa ngazi zote, tuliona kuna haja wananchi wakanufaika moja kwa moja na fedha hizi kwa kukatiwa bima ya afya kwa kuwa kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu,” amesema Mlelwa.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kijiji hicho ni cha mfano kote nchini kwani viongozi wake wamefanya ubunifu mkubwa wa kuhakikisha afya za watu wao zinatunzwa.
Amemwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Stanley Mlay kuhakikisha Kituo cha Afya cha kata hiyo hakipungukiwi na dawa ili wananchi hao wanapokwenda kupata huduma wapate dawa zinazohitaji kulingana na magonjwa waliyonayo.
“Mganga mkuu, fedha hizi zilizolipwa na kijiji hiki ni nyingi na zinazojitosheleza kununua dawa za aina zote. Sasa sitegemei kusikia kuwa wanakijiji hawa wanaishia kupewa panado tu badala ya dawa ya ugonjwa husika aliokutwa nao,” amesema Mtaka.
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva amesema fedha zinazoendelea kupatikana wawekeze pia katika kuwawezesha vijana kupata elimu ya ufundi itakayowawezesha kupata ajira katika miradi hiyo mikubwa ya Liganga na Mchuchuma pindi itakapoanza na pia waweze kujiajiri.
Mbunge wa Ludewa (CCM), Joseph Kamonga amesema anaona fahari kuona fedha zilizotokana na fidia hiyo ambayo aliipigania ili Serikali iweze kuwalipa wananchi hao imeweza kuleta manufaa makubwa.
“Kwasasa sina hofu na utoaji wa huduma katika kata hii maana najua mna kituo cha afya kikubwa na chenye vifaa tiba vya uhakika pamoja gari la kubebea wagonjwa,” amesema Kamonga.
Diwani wa Kata hiyo, Wise Mgina amesema suala la kusomesha vijana lipo katika mpango mkakati na wamelenga kuwainua watoto waishio katika mazingira magumu na yatima kwa kuwasomesha kozi fupi katika vyuo vya ufundi.
Mmoja ya wananchi wa kijiji cha Mundindi, Rita Mgeni ameishukuru Serikali kwa kutoa fidia kwa wananchi ambayo imewawezesha kukata bima ya afya kwa kila mwananchi wa kijiji hicho.