Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikwete asimulia kwanini Serikali ilianza kufadhili tafiti

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete wakati akisikiliza maelezo kutoka kwa baadhi ya waonyeshaji katika ofisi za Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA)

Muktasari:

  • Ili kuhakikisha taasisi za tafiti nchini zinaendelea kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa, alilazimika kuhakikisha asilimia 1 ya bajeti ya Taifa inaelekezwa katika kufadhili tafiti badala ya kusubiri wafadhili wa nje.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameeleza namna alivyoanzisha mfuko maalum wa utafiti nchini, hatua iliyolenga kufufua taasisi za utafiti zilizokuwa zikidorora kutokana na uhaba wa fedha na ukosefu wa wataalamu vijana.

Kikwete aliyekuwa Rais wa Tanzania (2005–2015) ametoa simulizi hiyo jana Jumatano, Mei 6, 2026 katika ofisi ya Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) kulipokuwa na hafla iliyokutanisha wadau mbalimbali wa kilimo.

Alisema mapenzi yake kwa kilimo na utafiti yalimfanya afuatilie kwa karibu maendeleo ya taasisi za utafiti wa kilimo nchini alipokuwa madarakani.

Alisema mapenzi yake kwa kilimo yalimfanya, alipokuwa Rais, kutembelea karibu taasisi zote muhimu za utafiti wa kilimo nchini, zikiwemo Uyole, Naliendele, Ukiriguru, Tengeru, Maruku na Mlingano.

Katika ziara hizo, aligundua changamoto mbili kubwa zilizokuwa zikikabili sekta hiyo, ambazo ni idadi kubwa ya wanasayansi waliokuwa wamekaribia kustaafu huku vijana wachache wakionekana kuingia katika taaluma hiyo.

“Nilienda maeneo mengi na nilichokiona ni kwamba watafiti wengi walikuwa wazee. Nikajiuliza, mbona hakuna kizazi kipya cha wanasayansi?” amesema.

Kwa mujibu wa Kikwete, sababu mojawapo ya hali hiyo ilikuwa ni zuio la ajira mpya serikalini, hali iliyofanya vijana wengi kutoajiriwa huku wazee wakiwa ndiyo waliokalia viti maofisini, hasa katika taasisi za utafiti.

“Nikafanya jambo ambalo baadhi ya watu wanaweza kusema halikuwa la kibinadamu. Niliwaambia wale wazee, hamtastaafu sasa hivi, mtaendelea kufanya kazi mpaka pale mtakapochanganya mbegu ambazo hazipaswi kuchanganywa, kama muhogo na mahindi pamoja, ndipo tutajua sasa ni muda wa kwenda nyumbani kulea wajukuu,” amesema.

Ili kukabiliana na hali hiyo, alilazimika kuanzisha utaratibu wa kutenga asilimia 1 ya bajeti ya Taifa kwa ajili ya kufadhili tafiti nchini.

“Niliamua fedha zielekezwe kwenye Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ili isimamie mfuko huo. Taasisi za utafiti na vyuo vikuu waombe fedha, kisha tume iamue ni miradi ipi ifadhiliwe,” amesema.

Amesema uamuzi huo ulisaidia sana kwani awali tafiti nyingi zilikuwa zinafadhiliwa na wafadhili wa nje wakati ambao Serikali haikuwa ikifadhili utafiti.

Wakati huo, wafadhili walikuwa na vipaumbele vyao ambavyo si lazima viwe sawa na mahitaji ya Serikali au taasisi husika.

“Kupitia mfuko huo, karibu kila taasisi ya utafiti ilipata angalau miradi miwili iliyokuwa inafadhiliwa na Serikali. Tunafanya hivi kwa sababu tunafahamu kuwa wafadhili wana maslahi yao. Si lazima yale wanayotaka yafanane na yale ambayo Tanzania inahitaji. Ndiyo maana tulihitaji fedha zetu wenyewe kwa ajili ya tafiti zetu wenyewe,” amesema.

Mbali na kugharamia miradi ya tafiti, sehemu ya fedha hizo ilitumika kusomesha vijana katika ngazi za shahada za uzamili na uzamivu ili kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa sayansi na utafiti.

“Hivyo tuliweza kupata mbadala wa wale waliokuwa wanastaafu. Vijana wakaajiriwa, wakapewa mafunzo na taasisi zikaendelea kuwa na wataalamu,” amesema.

Mbali na yaliyofanyika, pia anasema jambo hilo lilimsukuma kuanzisha tuzo ya kitaifa ya kutambua mafanikio ya kisayansi baada ya kugundua kuwa watafiti wengi walikuwa wanafanya kazi kubwa lakini bila kutambuliwa.

“Ukifika taasisi za utafiti, mwanasayansi anakwambia hii mbegu nimeibuni mimi, hii aina nimeigundua mimi. Nikasema watu hawa wanahitaji kuthaminiwa. Kutambua mchango wa watafiti ni njia mojawapo ya kuwahamasisha vijana wengi zaidi kuingia katika sekta ya sayansi, teknolojia na ubunifu,” amesema.

Akizungumzia IITA, Kikwete amesema taasisi hiyo ni mshirika muhimu katika ndoto ya kuona kilimo cha Tanzania kinabadilika kwa kutumia sayansi.

“Mlipoanza nilikuwa na matumaini. Leo mmeonyesha nilikuwa sahihi. Mmefanya vizuri sana, kwa haraka na kwa ubora mkubwa,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa IITA, Dk Simeon Ehui amesema kilimo kinaendelea kuwa mhimili mkuu wa uchumi wa Tanzania na maisha ya wananchi wake huku nchi ikiendelea kuelekea kwenye mustakabali wenye ustahimilivu zaidi na uchumi wa viwanda.

“IITA inachangia mabadiliko hayo kwa kuboresha aina za mazao, kuimarisha usimamizi wa rutuba ya udongo na kuongeza uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mbinu bora za kilimo, pamoja na kuimarisha uwezo wa wanasayansi na taasisi za Tanzania,” amesema.

Kupitia afua maalum, IITA inawaunga mkono wakulima wadogo kwa kuanzisha mbegu na teknolojia bora kupitia suluhisho zinazotokana na utafiti ambazo huongeza uzalishaji, kukuza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi na kuwasaidia wakulima kupata mavuno bora zaidi.

Amesema taasisi hiyo pia imewekeza kuwaendeleza wanasayansi vijana na watafiti, hatua inayosaidia kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa kuendeleza ubunifu na kukuza sekta ya kilimo nchini Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

“IITA inajivunia kushirikiana na Tanzania katika kujenga sekta ya kilimo ya kisasa, yenye tija na inayowajumuisha wote. Kipaumbele chetu kiko wazi, kutoka ubunifu kwenda kwenye matokeo kwa kiwango kikubwa, ili suluhisho zilizothibitishwa ziwafikie wakulima, zitengeneze ajira kwa vijana na kuimarisha usalama wa chakula pamoja na mageuzi ya uchumi,” amesema.