Kikwete: Sina shaka Tanzania ipo mikono salama

Kikwete: Sina shaka Tanzania ipo mikono salama

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema ana imani nchi ipo salama kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anajua yaliyofanyika, yanayotakiwa kukamilishwa na yaliyopangwa kufanyika miaka mitano ijayo.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema ana imani nchi ipo salama kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anajua yaliyofanyika, yanayotakiwa kukamilishwa na yaliyopangwa kufanyika miaka mitano ijayo.

Kikwete aliyekuwa rais mwaka 2005 hadi 2015 ameeleza hayo leo Ijumaa Machi 19, 2021 katika andiko lake aliloliweka katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter huku akieleza jinsi alivyopata tabu kuandika lakini akiwataka Watanzania kumpa ushirikiano  Samia.

Leo Rais Samia aliapishwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.

“Tupeane pole Watanzania kwa msiba mkubwa uliotukuta ni pigo kubwa tena ni kubwa lisilomithilika. Rais wetu mpendwa Magufuli ametutoka ghafla bila kutazamia. I never saw this coming. John Pombe Joseph Magufuli ametutoka wakati ambapo uongozo wake ulikuwa unahitajika sana. Tulikuwa tunamhitaji kukamilisha aliyoyaanza na kufanya mazuri mengi aliyokuwa amepanga kuifanyia nchi yetu na sisi wananchi wake,” amesema Kikwete.

Katika maelezo yake Kikwete amesema wengi wanatamani Magufuli angeendelea kuwa rais na miaka mingi ijayo lakini mapenzi ya Mungu hayawezi kubadilika.

“Wajibu wetu ni kumuombea kwa mola ampe pumziko. Daima tutamkumbuka Magufuli kwa mema mengi aliyoifanyia nchi yetu. Hakika Tanzania imepoteza kiongozi mzalendo wa dhati, shupavu, mahiri na makini,” amesema.

Katika andiko lake hilo, Kikwete ameonyesha matumaini kwa Samia kwa kuwa amekuwa makamu wa rais akiwa sambamba na Magufuli hadi siku ya mwisho kiongozi huyo alipokutwa na umauti.

“Jambo la faraja kubwa kwetu Watanzania ni kuwa mrithi wake Samia alikuwa makamu wa rais wa Magufuli tangu mwaka 2015 hadi umauti ulipomkuta. Anajua undani wa yale yaliyofanyika na yanayohitaji kukamilishwa aidha anayajua yaliyopangwa kufanyika katika miaka mitano ijayo. Sina shaka kuwa Tanzania ipo katika mikono salama,” amesema.

Kikwete alimpongeza Samia kwa hotuba yake aliyoitoa leo baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam akibainisha kuwa ilikuwa nzuri yenye kujenga imani na kuleta matumaini.

“Tumuombee rais wetu kwa mwenyezi Mungu amuongoze vyema kwa kila uamuzi atakaouchukua na kila hatua atakayopiga. Niwaombe Watanzania wenzangu tumpe ushirikiano ili aweze kuiongoza Tanzania kwa ufanisi na mafanikio tunayoyatarajia.”

“Napenda kutoa salamu za mkono wapole  na rambirambi kwa mama Janet Magufuli  na familia nzima. Tuko pamoja katika majonzi na kuomboleza. Tunawaombea moyo wa subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu,” amesema Kikwete.