Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichotokea kesi ya wanaokabiliwa na mashtaka 20, kujipatia Sh5.7 bilioni

Baadhi ya washtakiwa wa kesi ya uhujumu uchumi wanaokabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni.

Muktasari:

  • Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Agosti 30, 2024 na Juni 28, 2025, katika makao makuu ya Benki ya Equity Tanzania Limited yaliyopo Ilala, ambapo waliiba jumla ya Sh5.7 bilioni mali ya benki hiyo.

Dar es Salaam. Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa wanane wanaokabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni, imeieleza Mahakama kuwa wanasubiri ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili wakamilishe mchakato wa majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo baina yao na mshtakiwa Fredrick Ogenga.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Thawab Issa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Jumanne, Juni 23, 2026, wakati kesi hiyo ilipoitwa.

Mbali na Fredrick ambaye ni mfanyabiashara, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Jasmine Elphas ambaye alikuwa ofisa wa Benki ya Equity makao makuu.

Wengine ni Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul na Jefferson Ogenga, wote ni wafanyabiashara.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu, mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited.

Wakili Issa ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga.

"Kesi imeitwa leo kwa ajili ya kutoa mrejesho, kwa sababu tarehe iliyopita tuliomba ahirisho kwa ajili ya kusubiri mchakato wa maridhiano ya kosa na tulipangiwa tarehe ya leo kwa ajili ya kukamilisha mchakato," amedai Issa.

"Hata hivyo, kwa leo, tumekumbana na kikwazo cha idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ambaye yupo nje ya nchi kikazi na anatarajia kurejea nchini Jumatano ya wiki hii na tumejaribu kutafuta wasaidizi wake lakini imeshindikana na tumeambiwa yeye pekee ndiye mwenye mamlaka ya kutoa kibali (idhini)," alidai Wakili Issa.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili wa utetezi Meshack Dede anayemtetea mshtakiwa Frederick, aliiomba mahakama ipange tarehe fupi kwa ajili ya kukamilisha majadiliano hayo ili mteja wake aweze kuimaliza kesi hiyo.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Issa aliiomba mahakama ipange tarehe ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Kiswaga, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 2, 2026 kwa ajili ya DPP kutoa idhini.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana.

Katika kesi ya msingi, kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 18447 ya mwaka 2025.

Kwa mujibu wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Agosti 30, 2024 hadi Juni 28, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh5.7 bilioni mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited.

Katika tarehe hizo, mshtakiwa Jasmine na Ogenga, wakiwa ndani ya makao makuu ya Benki ya Equity iliyopo Ilala, waliiba Sh3.6 bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika akaunti ya clearing and settlement mali ya Benki ya Equity.

Washtakiwa wengine wanadaiwa kuwa katika tarehe hizo, katika makao makuu ya Benki ya Equity iliyopo Ilala, waliiba Sh728 milioni mali ya benki hiyo.

Pia ilidaiwa kuwa kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025, katika makao makuu ya benki hiyo, waliiba Sh26 milioni kutoka akaunti ya benki hiyo.

Mashtaka mengine ni kujipatia fedha na kutakatisha fedha.