Kilimo cha pamba si cha Kubahatisha-Mwanri
Balozi wa pamba nchini Tanzania, Agrey Mwanri akiwa ameshika zao la pamba kwenye mkutano wa hadhara wenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha pamba wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Muktasari:
- Wakulima wa pamba nchini wametakiwa kuacha mazoea ya zamani na kuzingatia kanuni zote za kilimo bora kuanzia maandalizi ya mashamba, upandaji, utunzaji hadi uvunaji ili kuongeza ubora wa zao hilo na kipato chao.
Shinyanga. Balozi wa Pamba Tanzania, Agrey Mwanri amewataka wakulima kuachana na utaratibu wa kurusha mbegu ovyo mashambani na badala yake kuzingatia kanuni za kilimo bora ili kuongeza uzalishaji, ubora wa pamba na kipato.
Akizungumza leo Julai 15, 2026 katika ziara ya kutoa elimu kwa wakulima wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mwanri amesema kilimo cha pamba kinahitaji kuzingatia hatua zote kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji, utunzaji hadi uvunaji.
“Tunataka mkulima azalishe kwa tija. Pamba haitaki bahati, inahitaji kufuata kanuni za kilimo bora,” amesema.
Amesema ubora wa zao hutegemea kwa kiasi kikubwa mbegu na nyuzi zake, akibainisha kuwa mbegu huchangia asilimia 58 ya uzito wa pamba na nyuzi asilimia 42, hivyo matumizi ya mbinu sahihi huongeza thamani ya zao.
Mwanri pia amewataka wakulima kung'oa na kuteketeza maotea ya pamba mara baada ya mavuno ili kuzuia wadudu na magonjwa yanayoweza kuathiri msimu unaofuata.
Baadhi ya wakulima wa zao la pamba wakiwa katika mkutano wa utoaji elimu wilayani Kishapu. Picha na Hellen Mdinda.
Amesema baadhi ya wakulima hudhani dawa hazina ubora, ilhali changamoto mara nyingi husababishwa na kuendelea kuwepo kwa wadudu kutokana na kutofanyika usafi wa mashamba.
Kuhusu uvunaji, amesema bado baadhi ya wakulima hutumia njia ya ‘ukombakomba’, inayochanganya pamba na uchafu kama majani, maganda na vikonyo, jambo linaloshusha ubora na bei ya zao, wakati mwingine hadi kufikia takribani Sh600 kwa kilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi amesema wilaya hiyo inaendelea kusimamia zao la pamba ili wakulima wanufaike. Amesema katika mwezi mmoja wa mauzo, Kata ya Bubiki iliuza kilo 364,000 za pamba zenye thamani ya zaidi ya Sh451 milioni, huku Kata ya Idukilo ikiuza kilo 289,377 zenye thamani ya zaidi ya Sh358.8 milioni.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Peter Masindi akizungumza katika mkutano na wakulima wa zao la Pamba wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Ameongeza kuwa Wilaya ya Kishapu kwa ujumla imeingiza zaidi ya Sh13 bilioni kupitia mauzo ya pamba, jambo linaloonyesha mchango mkubwa wa zao hilo katika uchumi wa wananchi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Joachimu Gobanya amesema bodi itaendelea kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa kanuni za kilimo bora ili kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba nchini.
Baadhi ya wakulima, akiwamo Paulo Kulwa, wameipongeza Serikali kwa kuwafikia na elimu hiyo, wakisema itawasaidia kuboresha uzalishaji na kuongeza kipato.