Kimbunga Hidaya chakata mawasiliano mikoa ya Kusini- Dar

Muktasari:

  • Madaraja manne yakatika, DC Lindi na Meneja wa Tanroads wazungumzia madhara. 

Lindi. Zaidi ya madaraja manne wilayani Kilwa, mkoani Lindi katika barabara iendayo Dar es Salaam yamesombwa na maji, hivyo kukata mawasiliano kwenye mikoa ya kusini.

Hali hiyo inatokana na madhara ya kimbunga Hidaya kilichosababisha mvua kubwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amesema takwimu za juzi Mei 3, na jana Mei 4, 2024 zinaonyesha kuwapo mvua kubwa zilizotokana na kimbunga Hidaya.

Kimbunga Hidaya chakata mawasiliano mikoa ya kusini-Dar

Amesema mvua zimesababisha zaidi ya madaraja manne kukatika yakiwamo ya Somanga, Mikereng’ende, na la Mto Matandu, huku baadhi ya vijiji vikiwa vimezingirwa maji.

“Uharibu ni mkubwa hatuwezi kurekebisha kwa kipindi kifupi. Tumeshauri watu wasitishe safari au wazunguke Songea (mkoani Ruvuma) kama ni dharura ili wasije kuathirika. Ni vema watu wa Lindi wabaki Lindi na walioko njiani warudi, uharibifu ni mkubwa zaidi tutatoa taarifa baadaye,” amesema.

“Vipo vijiji ambavyo vimezungukwa na maji katika Kata ya Masoko, mto Matandu, Songasi, Mitole, Likwatu, Mavuji na Machakama. Zaidi ya watu 70 wako hatarini na maeneo hayafikiki kabisa,” amesema Nyundo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Lindi, Emil Zengo amesema Somanga Mtama tuta la barabara limesombwa na maji, ikiwa ni athari za kimbunga Hidaya.

“Baada ya mvua kunyesha kwa wingi katika ukanda wa Lindi maji yakawa mengi zaidi na kusababisha barabara eneo la Somanga Mtama kusombwa na maji.”

“Ukiwa unaelekea Lindi kama kilomita 10 kuna eneo panaitwa Mikereng’ende pia tuta limesombwa na maji  mpaka sasa jitihada zimeanza kufanyika. Tunaomba wananchi na madereva wawe na subira wasizibe barabara bali wafuate taratibu za kuegesha kwenye barabara ili tupata njia ya kupitisha vifaa vya kufanyia kazi,” amesema. 

“Kwa eneo ambalo limeathirika bado maji ni mengi ni zaidi ya mita 80 Somanga na Mikereng’ende mita 60 hatuwezi kupata magari kutoka Lindi tunapahudumia kutokea Mkoa wa Pwani,” amesema.

“Kuna maeneo maji yapo juu ya barabara, mfano Matandu hatuwezi kusema lini kazi (ukarabati) utakamilika tunaangalia wapi pameathirika zaidi kikubwa tusubiri kauli ya wizara,” amesema.