Kinachosubiriwa kesi ya kina Mbowe leo

Muktasari:

Leo Jumatatu Novemba 29, 2021 Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, inaendelea na usikilizaji wa kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi.

Dar es Salaam.  Leo Jumatatu Novemba 29, 2021 Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, inaendelea na usikilizaji wa kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi.

Kesi hiyo iko katika hatua ya usikilizwaji wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, inayohusu uhalali wa maelezo yanayodaiwa kuwa yalitolewa na mshtakiwa wa tatu, Mohamed Abdillahi Ling'wenya.

Mshtakiwa huyo wa tatu ambaye ni shahidi wa kwanza wa utetezi katika kesi hiyo ndogo leo anatarajiwa kumalizia ushahidi wake aliouanza tangu Ijumaa iliyopita, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.

Hata hivyo kabla ya shahidi huyo (mshtakiwa) kumalizia utetezi wake, kwanza mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi pingamizi la upande wa mashtaka kuhusu barua ambayo mshtakiwa huyo anaiomba mahakama hiyo iipokee kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa utetezi.

Barua hiyo Ling'wenya amemwandikia Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Ilala akiomba baadhi ya nyaraka za kuthibitisha maelezo ya ushahidi shahidii wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ndogo, kuwa mwaka 2020 alikuwa akifanya kazi kituo kituo Kikuu cha Polisi Dar. (Central) na kwamba aliwapokewa yeye ( Ling'wenya) na mwenzake kitioni hapo na kuwahofadhi majabusu.

Upande wa mashtaka ulipinga barua hiyo kupokewa kwa madai kuwa shahidi huyo (mshtakiwa) na kielelezo hicho hawajakidhi vigezo vya kupokelewa kuwa kielelezo.

Ling'wenya katika utetezi wake alipinga ushahidi wa shahidi huyo wa pili wa upande wa Mashtaka katika kesi ndogo, Ditektivu Koplo Recardo Msemwa, aliyedai kuwa aliwapokea (wao Ling'wenya na Kasekwa) Central Dar es Salaam Agosti 7, 2020, wakati akifanyia kazi hapo kabla ya kuhamishiwa Polisi Oysterbay.

Washtakiwa tayari wameshafikishwa hapa Mahakamani na bado wako mahabusu.

Mawakili wa pande zote pia wameshafika. Mawakili qa Serikali wako ofisini kwao lakini mawakili wa utetezi pamoja na wasikilizaji wako ndani ya ukumbi wa mahakama, wakisubiri taratibu kukamilika ili kesi ianze.

Mwananchi tutakuletea mwenendo wote moja kwa moja kutoka hapa mahakamani, kadri kesi itakavyokuwa inaendelea.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu Uchumi namba 16/2021 yenye mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi, vinavyodaiwa kuwa vikilenga kuleta hofu katika jamii ya Wananchi wa Tanzania

Vitendo hivyo ni pamoja na kutaka kulipua vituo vya mafuta, maeneo ya mikusanyiko ya watu, kuzuia barabara kwa miti na magogo na kutaka kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Agosti,2020, katika maeneo Moshi, Arusha na Dar es salaam.