Kiongozi wa wafugaji achukuliwa na wasiojulikana nyumbani kwake, Polisi…
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya.
Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilayani Namtumbo Jiganga Kayungilo, amevamiwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana na watu waliodai kuwa ni askari na kuondoka naye.
Dar es Salaam. Hofu na sintofahamu vimetanda miongoni mwa wafugaji katika Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilayani humo, Jiganga Kayungilo, kuchukuliwa waliodai kuwa ni askari na kuondoka naye katika mazingira yanayozua maswali.
Sintofahamu hiyo imetokana na uvamizi wa watu waliodai kuwa askari na kuondoka naye pamoja na fedha taslimu Sh14 milioni.
Taarifa za awali zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo WhatsApp zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumatatu Juni 15, 2026, katika Kijiji cha Ligunga, Kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo.
Taarifa hizo zinadai watu hao waliovalia kininja walifika nyumbani kwa Kayungilo saa sita usiku, wakafanya msako ndani ya nyumba zake wakidai wanatafuta silaha anayomiliki.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosambazwa na Katibu wa Kanda ya Kusini wa Chama cha Wafugaji, Prisca Kaponda, baada ya upekuzi huo kutofanikisha kupatikana kwa silaha yoyote, watu hao walifanikiwa kukuta fedha taslimu Sh14 milioni ndani ya sanduku la Kayungilo, wakazichukua na kuondoka naye kwenda kusikojulikana.
Kaponda amesema ndugu na majirani wote hakuna anayefahamu alipo kiongozi huyo wala waliomkamata, kiasi cha kuzua hofu kwa wafugaji wa eneo hilo.
“Tumepata taarifa za kusikitisha. Makamu Mwenyekiti wetu amechukuliwa na watu wasiojulikana baada ya kuvamiwa nyumbani kwake. Hadi sasa hajulikani alipo. Wafugaji tunaishi kwa hofu kubwa sana na tunaomba mamlaka husika zichukue hatua za haraka na jamii itusaidie kupaza sauti ili ukweli wa jambo hili ujulikane,” alisema Kaponda katika taarifa hiyo.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Wilaya ya Namtumbo, Masemba Wanga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mazingira ya kutoweka kwa kiongozi huyo bado ni ya kutatanisha.
“Tukio hilo limetokea kweli. Makamu wetu amechukuliwa na watu wasiojulikana na mpaka sasa hatuna taarifa zaidi kuhusu alipo. Tunaendelea kusubiri viongozi wa Jeshi la Polisi wakamilishe kazi zao ili kujua kilichotokea na hatua zinazofuata,” amesema Wanga.
Kauli ya Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, amethibitisha kupokea taarifa za uwepo wa tukio hilo, akisema Jeshi la Polisi wilayani humo tayari linaendesha uchunguzi wa kina ili kubaini waliotekeleza uvamizi huo, walikotoka na sababu za kufanya walichofanya.
“Ni kweli kuna taarifa hizo. Kuna mwananchi mmoja mkazi wa Ligunga alivamiwa na watu waliojieleza kuwa ni askari ambao walidai wamefuata silaha. Silaha hiyo hawakuikuta, lakini walikuta fedha taslimu Sh14 milioni, wakazichukua na kuondoka na muhusika huyo.
Tangu jana tupo huko tunaendelea na upelelezi ili kubaini hao ni akina nani na kwa nini walifanya hivyo. Tutakapopata majibu, nasi tutazungumza,” amesema Chilya.