Kliniki afya ya uzazi muhimu hata kwa wanaume

Muktasari:

  • Wanaume wenye wenza wanyonyeshao wametakiwa kushiriki kikamilifu katika huduma za afya ya uzazi, ili waweze kupata elimu ya afya ya uzazi na umuhimu ya kunyonyesha watoto.

Tanga. Wanaume wenye wenza wanaonyonyesha wametakiwa kushiriki kikamilifu katika huduma za afya ya uzazi, ili waweze kupata elimu ya afya ya uzazi na umuhimu ya kunyonyesha watoto.

 Wito huo umetolewa leo Desemba 8 na mratibu wa afya ya mama na mtoto jijini Tanga, Ester Kimweri katika mahojiano maalumu juu ya umuhimu wa unyonyeshaji katika makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

 Kimweri amesema pamoja na hali ya unyonyeshaji katika jiji hilo kufikia asilimia 94,  kuna changamoto ndogo ambazo zinatakiwa ziondolewe ili kufikia ukamilifu wa unyonyeshaji wa waoto.

Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na wanawake wanaonyesha kuwa na mawazo au msongo hivyo kuathiri mtiririko wa maziwa, kuwepo kwa harufu kali kama za marashi, vipodozi udi na kadhalika na wenza (wanaume) kutokuwa karibu na wake zao wanaponyonyesha.

“Jamii inatakiwa kubadilika kimtazamo na kuliona jambo hili kuwa linawahusu wote, mama na baba.

“Wasimwache mama aje peke yake katika kliniki ya afya ya uzazi. Katika kliniki hizo kunatolewa elimu mbalimbali ya afya ya uzazi, ikiwemo umuhimu wa mama kunyonyesha kwa muda unaotakiwa,” amesema Kimweri.

Amesema ni hatari kwa baba kutokuwa karibu au kutohudhuria kliniki hizi kwa sababu yeye pia anatakiwa kujua ni aina gani ya chakula ambacho mama anatakiwa kula na ambacho kitaongezea kiwango cha maziwa kwa mama au ni huduma gani ambayo mama anatakiwa kuipata ili maziwa yatoke sawasawa.

Naye Mganga Muu wa Wilaya ya Lushoto, Dk Godfrey Andrew , amesema kuwa kunyonyesha kuna umuhimu kwa ajili ya kujenga akili ya mtoto na upendo.

Amesema kuwa wilayani Lushoto tatizo la wanawake kutonyonyesha watoto kwa angalau miezi sita ya kwanza halipo.

“Tatizo hilo liko mijini zaidi kwa sababu wanawake wanaogopa matiti yao kulegea. Wanawafikiria kina baba zaidi ya watoto,” amesema.

Naye Ofisa Lishe wa Mkoa, Sakina Mustafa amewataka kina mama kunyonyesha watoto angalau miezi sita kwa sababu asipofanya hivyo kinga yake itakuwa chini na kuwa na uwezekano wa kuambukizwa magonjwa kutokana na kinga kuwa chini.

Hata hivyo, Amina Mbwana wa mtaa wa Kasera jijini Tanga alieleza kuwa awali alikuwa haoni umuhimu wa kunyonyesha sababu aliamini kwenye kuanza kumlisha vyakula laini balada ya maziwa na kwamba baada ya elimu hii atajitahidi kubadilika pindi atakapojifungua mtoto mwingine.