Prime
Kombo apandishwa kizimbani kimyakimya, asomewa mashtaka matatu
Muktasari:
- Kada wa Chadema aliyetoweka kwa siku 29 na kubainika kushikiliwa na Polisi, jana Julai 16, 2024 amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga na kusomewa mashtaka matatu.
Dar es Salaam. Hatimaye kada wa Chadema, Kombo Mbwana aliyetoweka kwa siku 29 na kubainika kushikiliwa na Polisi, jana Julai 16, 2024 amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga na kusomewa mashtaka matatu.
Kombo aliyetoweka tangu Juni 15, 2024 baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake katika Kijiji cha Komsala Handeni mkoani Tanga, alibainika kushikiliwa na Polisi, baada ya Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, ACP Zacharia Bernard kutoa taarifa Julai 14, 2024 akieleza kumshikilia kwa tuhuma za kutumia vifaa vya kielektroniki pamoja na laini za simu zisizosajiliwa katika kutekeleza uhalifu, kinyume cha sheria za nchi.
Jana, Julai 17, 2024 ndugu wa Kombo waliruhusiwa kuonana naye katika Kituo cha Polisi cha Chumbageni jijini Tanga, hata hivyo hawakuambiwa iwapo atafikishwa mahakamani.
Lakini leo Julai 17, 2024 walipofuatilia kituoni hapo waliambiwa kuwa Kombo ameshapandishwa kizimbani na amepelekwa rumande katika gereza la Maweni Tanga.
Mashtaka yanayomkabili
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ya kesi namba 19759/2024, ambayo Mwananchi imeiona leo Julai 17, 2024, Kombo ameshtakiwa kwa makosa matatu ambayo ni pamoja na kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume cha kifungu 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.
Katika kosa hilo, inadaiwa Juni 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya wilaya na Mkoa wa Tanga, Kombo alikutwa akimiliki laini ya Tigo ikiwa na namba (ICCID), 8925502042093621824 iliyosajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umilikiwa wa laini hiyo.
Shitaka la pili, ni kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na mtu mwingine kinyume cha Kanuni ya 4(1)©, 12(3) na 21(1) ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Kanuni za usajili wa laini za simu) za mwaka 2020 zikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 52 cha Sheria ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Sura ya 306 RE 2022).
Katika shtaka hilo inadaiwa Juni 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya wilaya na Mkoa wa Tanga, Kombo alikutwa alikutwa akimiliki laini ya laini ya Tigo yenye ICCID 8925502042093621824 ya namba 0719 672 633 ambayo awali ilikuwa ikimiliwa na mtu aliyesajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa, bila kusajili namba hiyo kwa mamlaka.
Shitaka la tatu kwa mujibu wa hati hiyo ni kushindwa kuripoti mabadiliko ya umiliki wa laini ya simu kinyume cha 4(1) © na 21(1) ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Kanuni za usajili wa laini za simu) za mwaka 2020 zikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 152 cha Sheria ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Sura ya 306 RE 2022).
Imedaiwa Juni 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya wilaya na Mkoa wa Tanga, Kombo alikutwa alikutwa akimiliki laini ya laini ya Tigo yenye ICCID 8925502042093621824 ya namba 0719 672 633 iliyokuwa ikimilikiwa na mtu aliyesajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa bila kujulisha mamlaka.
Dhamana ya kesi hiyo ipo wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanataosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja na barua ya mtendaji wa mtaa na vitambulisho vya Taifa (Nida). Mshtakiwa ameshindwa kutumiza masharti ya dhanama, amepelekwa mahabusu.
Nje ya Mahakama
Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga, Michael Haule ameliambia Mwananchi kuwa leo wamechelewa kukamilisha masharti ya dhamana kwa kuwa hawakujua ameshtakiwa katikamahakama gani.
“Baada ya kuhangaka sana, tulikwenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, tukauliza wahusika, yupo ofisa mmoja alituambia kuwa Kombo ameshtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga.
“Tulipokwenda kule ndio tukapewa hati ya mashtaka. Leo hatuwezi kukamilisha masharti ya dhamana kwa kuwa muda wa Mahakama umekwisha,” amesema.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Tanga, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Benson Kigaila, amekosoa kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura aliyekanusha jeshi hilo kuhusika na tuhuma za utekaji.
Kigaila amesema tukio la kukamatwa kwa Kombo lina viashiria vya utekaji.
IGP Wambura akizungumza juzi Julai 15, 2024 mkoani Simiyu akiwa katika ziara ya kuzungumza na maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) alisema jeshi hilo halihusiki na utekaji, bali limekuwa likiwaokoa wanaotekwa.
“Sasa tunataka IGP atuambie, huu ndio mtindo wa Polisi kukamata watuhumiwa? Ni sheria gani inaruhusu polisi waende wamevaa kiraia, waende wakamkamate mtu bila kumwambia kwa nini wanamkamata.
“Polisi ili akukamate anajitambulisha kwako kwamba ni ofisa wa Polisi na kuonyesha kitambulisho chake, anakukamata kwa sababu moja, mbili tatu. Ndugu wa Kombo walikuwa na haki ya kujua kwa nini Komnbo anakamatwa na anapelekwa wapi.
“Siku 29 ndio wanakuja kutuamnbia wako naye na hawajampeleka mahakamani. Ni sheria gani hiyo ya Jeshi la Polisi au sheria zilizoandikwa Tanzania ambazo Polisi wanazotumia kumshikilia Kombo. IGP atuambie,” amesema.
Tukio la kutekwa kwa Kombo lililotokea Juni 15, 2024 kijijini kwao Kwamsala wilayani Handeni, Tanga ambapo watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake wakidai eneo analojenga nyumba yake ni la kwao.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.