Kortini kwa kuandamana peke yake Singapore

Muktasari:

Wham anakabiliwa na adhabu ya faini ya dola 3,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh6.6 milioni za Kitanzania) kwa kila kosa kama akipatikana na hatia, kwa mujibu wa nyaraka za mashtaka.

Singapore, Singapore (AFP)
Mwanaharakati wa Singapore leo Jumatatu (Novemba 23) ameshtakiwa kwa kufanya maandamano yasiyo halali akiwa peke yake baada ya kusimama nje ya kituo cha polisi akiwa ameshikilia bango lenye sura ya kicheko cha dhihaka.
Jiji hilo linalodhibitiwa vikali lina sheria kali dhidi ya upinzani ambazo zinaharamisha kufanya maandamano bila ya kuwa na kibali cha polisi.
Jolovan Wham, ambaye amekuwa na matatizo ya mara kwa mara na mamlaka, alituma picha yake mwezi Machi katika mitandao ya kijamii akiwa ameshikilia bango lenye sura iliyochorwa hovyo.
Mwanaharakati huyo alituma picha katika akaunti yake mtandaoni akiwa njiani kwenda mahakamani, akiwa amevalia fulana na barakoa zilizochorwa sura ya kikaragosi kinachocheka. 
"Kosa langu ni kufanya watu waone," alisema. 
Pia alishtakiwa kwa kuonyesha bango nje ya mahakama mwaka 2018, akiitaka serikali iondoe mashtaka ya udhalilishaji dhidi ya watu wawili walioandika habari katika mtandao wa kijamii kuhusu tuhuma za rushwa miongoni mwa viongozi wa serikali.
Wham anakabiliwa na adhabu ya faini ya dola 3,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh6.6 milioni za Kitanzania) kwa kila kosa kama akipatikana na hatia, kwa mujibu wa nyaraka za mashtaka.
Mwanaharakati huyo alitumikia kifungo cha siku kumi jela mapema mwaka huu kwa kuandaa tukio mwaka 2016 ambalo lilimuhusisha mwanaharakati maarufu wa demokrasia jijini Hong Kong, Joshua Wong ambaye alizungumzia kwa njia ya Skype.
Kibali cha maandamano hutolewa kwa nadra sana Singapore na huruhusiwa bila ya kibali cha polisi kama yanafanyika pembeni ya bustani ya jiji hilo.