Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Krismasi ilikuwa shwari - Polisi

Muktasari:

Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa alisema jana kuwa hali ilikuwa shwari japo kulikuwa matukio madogo ya uhalifu.

Dar/Mikoani. Jeshi la Polisi limesema hakuna matukio makubwa yaliyoripotiwa wakati wa Sikukuu ya Krismasi.

Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa alisema jana kuwa hali ilikuwa shwari japo kulikuwa matukio madogo ya uhalifu.

Alisema juzi alipigiwa simu kwamba kuna vibaka wamevunja banda na kuiba kuku na mwingine aliibiwa simu na mkoani Dar es Salaam polisi walifanya operesheni kwenye Ufukwe wa Coco na maeneo mengine.

Mwakaluka alisema viongozi wa dini waliwahamasisha waumini kulinda amani na kukaa na familia wanaposherehekea sikukuu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema hali ilikuwa shwari ingawa waliwakamata watu 25 katika kituo cha mabasi yaendayo mikoa ya Kusini cha Temeke Sudan wakituhumiwa kuwabughudhi abiria.

“Hakuna tukio lolote kubwa la kihalifu lililoripotiwa isipokuwa haya madogomadogo,” alisema.

Kilimanjaro, Arusha, Tanga

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema hakuna tukio kubwa lililotokea licha ya kuwapo idadi kubwa ya watu mkoani humo na msongamano wa magari.

Alisema juzi kulikuwa na uhaba wa magari ya kwenda Rombo lakini walishughulikia suala hilo.

Alisema jana asubuhi kulitokea ajali iliyomhusisha mtoto wa miaka sita ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Mkoa wa Arusha ambao miaka ya nyuma ulikuwa ni miongoni mwa maeneo yenye uhalifu wakati wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka, umeripotiwa kuwa shwari.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles Mkumbo alisema, hajapokea taarifa za uhalifu.

“Arusha imeendelea kuwa shwari na hakuna tukio kubwa la uhalifu ambalo limeripotiwa,” alisema.

Mkoani Tanga nako hakuna ripoti ya matukio yoyote ya uhalifu iliyotolewa katika sikukuu hiyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema jana kuwa hakukuwa na matukio yoyote ya kihalifu yaliyoripotiwa kutokea katika wilaya zote za mkoani hapa hadi jana.

Alisema siku tano kabla ya Krismasi, Jeshi la Polisi lilijipanga kwa kuweka ulinzi katika maeneo ambayo yana rekodi za uhalifu siku za sikukuu ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea bila bughudha.

Akizungumzia sikukuu hiyo, mkazi wa Amboni, Pascal Mbung alisema ilipooza kutokana na ukata.

“Kwa mfano mtaani kwetu Amboni, sikukuu zote nyama buchani huwa ni bidhaa adimu kwa kukosekana lakini jana hadi jioni mabucha yalikuwa na nyama,” alisema.

Rukwa, Mtwara

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema hakuna matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza kutokana na ulinzi kuimarishwa.

Alisema maeneo yote yaliyokuwa na mikusanyiko yakiwamo ya nyumba za ibada na kumbi za starehe, ulinzi uliimarishwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya alisema, “Hali ni shwari wananchi walisherekea sikukuu ya Krismasi kwa utulivu na amani.”

Mwanza, Kagera

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi na wa Kagera, Agustino Ollomi kwa nyakati tofauti walisema sherehe zilimalizika salama.

Kamanda Ollomi alisema ingawa mji wa Bukoba huwa na mkusanyiko mkubwa wa watu, hakupokea taarifa yoyote ya uhalifu au kupotea kwa watoto.

Kamanda wa Polisi Mwanza, Msangi alisema hali ilikuwa shwari na hapakuwa na tukio lolote la uhalifu wala uvunjifu wa amani lililoripotiwa.

Ajali mbaya Singida

Wakati hali ikielezwa kuwa shwari katika mikoa mingine, mkoani Singida mtu mmoja amefariki katika ajali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema juzi ilitokea ajali iliyohusisha gari lililokuwa likiendeshwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Juma Kilimba (50).

Alisema Kilimba alipata ajali saa 12:30 asubuhi katika Kijiji cha Misigiri wilayani Iramba akitokea jijini Dar es Salaam akirejea nyumbani kwake Iramba.

Kamanda Magiligimba alisema gari hilo liliingia kwenye shimo na kuacha njia kisha kupinduka matairi yakiangalia juu baada ya kukatika steering road hivyo Kilimba kushindwa kulimudu.

Alisema mtoto wa miezi 10, Fatuma Kilimba alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba.

Alisema Kilimba na abiria mwingine, mwanafunzi wa Chuo cha IFM, Judi Ikoty (21) walipata majeraha na walitibiwa katika hospitali hiyo na kuruhusiwa.

Alisema majeruhi wengine ni mfanyabiashara Emmy Hiari (44) aliyevunjika mkono wa kushoto, Venance Kilimba (10) mwanafunzi wa darasa la nne na Manale Kilimba (9), mwanafunzi darasa la tatu.

Kamanda Magiligimba alisema majeruhi watatu wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya St. Gasper iliyopo Itigi na hali zao zinaendelea kuimarika.

Imeandikwa na Pamela Chilongola, Janeth Joseph, Mussa Juma, Burhani Yakub, Mussa Mwangoka, Jesse Mikofu, Phinias Bashaya, Gasper Andrew na Mary Sanyiwa.