Kufungwa Ziwa Tanganyika: Wavuvi wasimulia wanayoyapitia
Muktasari:
- Ziwa Tanganyika lilifungwa Mei 15, 2024 na linatarajiwa kufunguliwa Agosti 15, 2024, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kusimamisha shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu kila mwaka kwa miaka mitatu mfululizo, ili kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana.
Kigoma/Katavi. Zikiwa zimepita siku 67 tangu kufungwa kwa Ziwa Tanganyika, baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara wameeleza machungu wanayopita, huku wakiishauri Serikali kudhibiti uvuvi haramu katika ziwa hilo litakapofunguliwa Agosti 15, 2024.
Ziwa Tanganyika linazunguka mikoa mitatu ya Kigoma, Rukwa na Katavi na kufanya Tanzania kulimiliki kwa asilimia 41 sawa na kilometa za mraba 13,489 kati ya kilometa za mraba 32,900 za ziwa hilo.
Ziwa hilo lilifungwa Mei 15, 2024 na kutarajiwa kufunguliwa Agosti 15, 2024, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kusimamisha shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu kila mwaka kwa miaka mitatu mfululizo, ili kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana.
Makubaliano hayo yaliazimiwa mwaka 2022 na nchi za Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinazozungukwa na Ziwa Tanganyika, pia yanahusisha utambuzi wa zana haramu za uvuvi, ili kuruhusu mazalia ya samaki kwa wingi, kudhibiti uvuvi haramu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Pia kipindi ziwa litakapofungwa, nchi wanachama watafanya utafiti wa kiwango cha samaki, utafiti wa kibaolojia na matokeo ya kiuchumi kwa watu wanaotegemea ziwa hilo kimaendeleo.
Wakizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Julai 25, 2024 wavuvi hao wamesema sababu ya kufungwa kwa ziwa hilo ni uvuvi haramu na kupungua kwa mazao ya samaki, lakini kama Serikali haitazuia watakaokuwa wanaumia ni wananchi wa kawaida.
Mvuvi na mmiliki wa zana za uvuvi, Kasia Hamimu amesema Serikali isilifungue ziwa hilo bila kuweka utaratibu mzuri wa kuvua mazao ya samaki kwa kuhakikisha wanasimamisha zana za uvuvi zisizotakiwa ndani ya Ziwa Tanganyika zinazosababisha kupungua kwa mazalia ya samaki.
“Kilichotufikisha hapa hadi ziwa kufungwa ni uvuvi haramu na kupungua kwa mazao ya uvuvi ziwani, ziwa likifunguliwa Serikali iweke utaratibu wa zana za uvuvi zitakazoingia ziwani sio kila mtu anaingia na kuvua. Hii itasaidia kuvua kwa malengo na kukomesha uvuvi haramu,” amesema Hamimu.
Naye Mvuvi wa mwalo wa Kibirizi, Marik Naseb amesema kabla ya kufungwa kwa ziwa alikuwa na mtaji wa Sh6 milioni kutokana na kukosa kazi ya kufanya amejikuta akila mtaji huo hadi kubaki na Sh1 milioni akidai hadi Agosti 15, 2024 atakuwa amemaliza mtaji wote.
Amesema hata zana zao za uvuvi zitalazimika kufanyiwa marekebisho yatakayogharimu Sh3 milioni pindi ziwa litakapofunguliwa, ili kuwa na hali nzuri ya kufanya uvuvi kwa kuwa baada ya kukaa muda mrefu bila kufanya kazi hasa mitumbwi imeharibika kwa kupigwa jua na kuliwa na mchwa.
“Tulichukua mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya shughuli zetu za uvuvi, lakini ziwa limefungwa tumebakia na madeni tu kwa sasa na sidhani kama kuna wavuvi wataweza kurudi ziwani kufanya shughuli za uvuvi baada ya ziwa kufunguliwa,” amesema Naseb.
Mvuvi na mkazi wa Karema Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi, Jordan Gerald amesema bila Serikali kuweka utaratibu mzuri wa uvuaji mazao ya samaki, ufungaji wa ziwa hilo hautokuwa na tija.
Kwa upande mwingine, Mwananchi limebaini baadhi ya wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma na Katavi wahamia kwenye uuzaji wa samaki aina ya kambale wanaopatikana kwenye mito na genge wanaovuliwa Ziwa Rukwa, huku wakiuza dagaa kutoka Ziwa Victoria.
Wafanyabiashara hao wanauza fungu la samaki Sh3,000 kwa wale wadogowadogo na Sh10,000 fungu la samaki wakubwa kiasi, huku dagaa wakiuzwa fungu moja kati ya Sh500 hadi Sh1,000.
Mfanyabiashara wa samaki soko la Buzebazeba mkoani Katavi, Sifa Hamilu amesema kwa sasa anauza samaki aina ya ngege anaowatoa mkoani Rukwa akidai analazimika kutumia Sh60,000 kama gharama ya kusafiri kufuata samaki hao.
“Bado kuni na mafuta kwa ajili ya kuwaandaa na kuwasafirisha… gharama ni kubwa tofauti na awali tulikuwa tunawapata hapahapa mkoani kwetu,” amesema.
Mfanyabiashara wa soko kuu la Mpanda mkoani Katavi, Asha Ramadhani amesema mzunguko wa biashara umekuwa mdogo tangu kufungwa kwa ziwa hilo kwa kuwa wanategemea wateja wanaoingia sokoni kwenda kununua bidhaa nyingine, kwa kuwa wanajua samaki hawapatikani kutokana na Ziwa Tanganyika kufungwa.
“Naunga mkono Serikali kufungwa kwa ziwa na likifunguliwa kutakuwa na neema nyingi ya mboga, ajira na fursa mbalimbali na hali hii ambayo wafanyabiashara wanalalamika wataisahau,” amesema Ramadhani.
Mfanyabiashara wa nafaka soko la Kibirizi mkoani Kigoma, Shedrack Tebuye amesema kabla ya kufungwa kwa Ziwa Tanganyika alikuwa akiuza bidhaa zake kuanzia Sh250,000 hadi Sh300,000 kwa siku, lakini tangu lifungwe mauzo yamepungua kufikia Sh100,000 kwa kuwa watu wamepungua eneo hilo hasa wavuvi.
Naye, Jabiri Mawazo, mkazi wa Kigoma mjini amewapongeza wafanyabiashara kwa ubunifu wa kuanza kuuza samaki kutoka maeneo mengine, badala ya kufunga biashara zao baada ya ziwa kufungwa, akidai wamegeuza changamoto kuwa fursa.
“Hata wavuvi tunasikia wamehamia Ziwa Victoria, hawasemi tu, lakini kwa kweli niwapongeze wangeamua tu kukaa nyumbani hadi ziwa lifunguliwe, lakini wakaamua kuuza dagaa wa Ziwa Victoria kujipatia kipato,” amesema