Laini zisizohakikiwa kuzimwa siku moja kabla ya Valentine's Day

Muktasari:

  • Kupambana na utapeli mtandaoni na hasa kwa kutumiwa ujumbe wa ‘tuma nauli kwa namba hii’, Serikali imesema itazima laini zote zisizohakikiwa, siku moja kabla ya Siku ya Valentine.

Dodoma. Serikali imetangaza kuzima laini zote zisizo hakikiwa itakapofika Februari 13, 2023. Siku moja kabla ya Valentine's Day.

Valentine's Day ni siku maarufu ya wapendao duniani ambayo husherehekewa Februari 14 ya kila mwaka. Ni sherehe inayotumiwa kuimarisha upendo kwa watu mbalimbali pia wandoa au wachumba.
Hayo yamesema leo Jumanne, Januari 24, 2023 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.
Amesema takwimu zilizopo hadi Januari 19, 2023 laini za simu zilizosajiliwa ni zaidi ya 60.7 milioni. Laini hizi ndio zinatumika mitaani na zingine kutapeli watu kwa kutumiwa ujumbe wa ‘tuma kwenye namba hii.’
Nape amesema Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ilitoa taarifa ya kuwataka wananchi wote kuhakiki namba zao.
Kwa mujibu wa Nape tarehe ya mwisho ya uhakiki wa namba imeahirishwa mara kadhaa na leo ameahirisha badala ya kuzimwa Januari 31, 2023, lakini amesogeza hadi Februrai 13, 2023, siku moja kabla ya Siku ya Wapendanao Duniani.
“Tumeweka hivyo ili siku ya Wapendao ‘Valentine's Day’ kusiwe na utapeli wa ‘tuma nauli kwenye namba hii,” amesema Nape.
Nape amesema tangu kuanza kampeni ya uhakiki wa namba za simu kutokana na wingi wa matukio ya utapeli ni namba zaidi 58.4 milioni ndio zimehakikiwa huku zaidi ya namba 2.3 milioni hazijahakikiwa hadi sasa.
“Tunazitafuta hizi milioni mbili ziko wapi, ndio zinazofanya utapeli mitaani. Ni namba ambazo zimesajiliwa, lakini hazijahakikiwa,” amesema.
Nape amesema Serikali ilipoanza kampeni ya kusajili namba zote za simu kwa teknolojia ya alama za vidole, lengo lilikuwa kupambana na utapeli.
Amesema kampeni hiyo ilianza Mei Mosi, 2019 na kumalizika Desemba 2021, na zile zilizokuwa hazijasajiliwa zilizimwa.
Hata hivyo, amesema kulikuwa na ujanja unaofanywa na wanaosajili laini za simu kutumia kitambulisho cha Taifa cha mtu mwingine kusajili namba zingine za simu na hizo ndio wanazitafuta.
“Kuna wale ambao hawajapata vitambulisho vya Nida na wametumia vitambulisho vya jamaa zao kusajili laini zao, waende kwa waliotumia vitambulisho vyao kuhakiki namba zao.
“Waende wakaongee nao, wakubaliane, kama atakubali atoe hizo taarifa zinazotakiwa kwenye kuhakiki laini, kwa kuwa ikitumika kufanya uhalifu atakaekamatwa ni mwenye kitambulisho,” amesema Nape.