Lampard atabiriwa mabaya Chelsea

Lampard atabiriwa mabaya Chelsea

Muktasari:

  • Frank Lampard anapewa nafasi kubwa ya kuwa kocha anayefuata kuonyeshwa mlango wa kutokea katika Ligi Kuu England kutokana na matokeo mabaya ya Chelsea.

London, England. Frank Lampard anapewa nafasi kubwa ya kuwa kocha anayefuata kuonyeshwa mlango wa kutokea katika Ligi Kuu England kutokana na matokeo mabaya ya Chelsea.

Kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Leicester, juzi usiku, kimemuacha mkongwe hyuyo wa Chelsea katika presha kubwa.

Chelsea imeshaonekana kuwa nje ya ubingwa wa Ligi Kuu England ikiwa nyuma ya vinara, Leicester City kwa pointi tisa.

Ikiwa katika nafasi ya nane, pia wapo pointi tano nyuma ya mstari wa kufuzu kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ikiwa imecheza mechi nyingi kuliko wapinzani wao wa nafasi hiyo.


Lakini kitu kinachoiumiza Chelsea kwasasa ni uwezo waop mdogo wa kupambana uwanjani kwa ajili ya kutafuta matokeo.

Lampard anajua kabisa jinsi mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich alivyo mwepesi kufanya uamuzi kama ataona matokeo hayo yanaiyumbisha timu.

Bilionea huyo Mrusi alishawahi kuonyesha kuwa hasiti kumtimua kocha ambaye ataonyesha kiwango kibovu, na alishafanya hivyo hata wakati Lampard akiwa bado mchezaji.

Na wadau mbalimbali wa soka wametabiri kuwa mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi kwa Lampard kama hatabadili matokeo ya sasa haraka iwezekanavyo.

Msemaji wa kampuni moja ya kubeti ya Betfair, alisema: “Frank Lampard ana alama 7/2 kuwa kocha ajaye wa kutimuliwa Ligi Kuu England kabla ya mchezo huu (wa juzi) kuanza.

“Lakini kama atafungwa katika mchezo huu (dhidi ya Leicester) na kuonyesha kiwango kibovu, basi atapewa alama 8/11 za kutimuliwa kazi.”

Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Andriy Shevchenko amepewa alama 7/5 za kuwa kocha ajaye wa kuchukua nafasi ya Lampard.

Chelsea itakuwa na mechi ngumu mbili nyumbani dhidi ya Wolves na Burnley kabla ya kusafiri kuifuata Tottenham, mchezo unaotajwa kuwa mgumu zaidi. Lakini kabla, watacheza na Luton, mchezo wa Kombe la FA.

Tayari Chelsea imeripotiwa kuanza kuangalia makocha ambao wanazungmza kijerumani kwa ajili ya kumrithi Lampard.

Katika orodha hiyo wapo kocha wa zamani wa PSG, Thomas Tuchel, Julien Nagelsmann wa RB Leipzig na mkongwe wa Ujerumani, Ralf Rangnick, ambao watasaidia kuwaweka sawa Kai Havertz naTimo Werner.