Latra yataka mabasi ya abiria yabebe ‘level seat’
Muktasari:
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) nchini Tanzania imetoa maagizo mbalimbali kwa wadau wa usafirishaji ikiwamo kuyataka mabasi yanayobeba abiria ‘daladala’ kuhakikisha wanabeba abiria kulingana na idadi ya viti ‘level seat’ ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vimeingia nchini humo na tayari watu sita wamebainika kuwa navyo.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) nchini Tanzania imeyataka mabasi ya usafirishaji abiria ‘daladala’ ndani ya jiji na mikoani kubeba watu kulingana na idadi ya siti zilizopo (Level Seat) ili kuepusha msongamano wa watu.
Kauli hiyo ya Latra inakuja wakati hofu ya wananchi wanaotumia usafiri wa umma ndani ya miji hasa Dar es Salaam ikiwa kubwa kutokana na msongamano uliokuwa ukionekana katika baadhi ya maeneo.
Latra imetoa maagizo hayo ikiwa ni baada ya kukutana na wadau wa usafiri na usafirishaji nchini, kutafakari na kuweka mikakati ya kukabiliana na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa corona.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Latra kwa vyombo vya habari jana Alhamisi Machi 19, 2020 inaeleza mbali na kubeba abiria wachache pia magari hayo yanapaswa kunyunyiziwa dawa kila mwisho wa safari.
Pia, magari hayo yametakiwa kuwa na dawa ya kuua wadudu mikononi (hand sanitizer) ili kila abiria apake kabla ya kuingia.
“Kuanzia sasa idadi ya abiria wanaoruhusiwa kwenye mabasi yanayosafiri kutoka mkoa kwenda mwingine, mijini kwenda vijijini na mabasi yote ya mijini ni kulingana na idadi ya viti vilivyopo kwenye basi,” inaeleza sehemu ya taarifa
”Kwa upande wa mabasi yaendayo haraka (BRT) yabebe idadi ya abiria kulingana na idadi iliyoainishwa kwenye leseni zake na magari ya mizigo hayaruhusiwi kubeba abiria,” inaeleza
Wakati huo pia watu wote wanaoingia na kutoka vituo vikuu vya mabasi na treni wanatakiwa kunawa mikono na maji yanayotiririka na sabuni huku wasindikizaji wakizuiwa kuingia ndani ya vituo vikuu vya mabasi na treni
Kwa upande wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) wametakiwa kuhakikisha pia treni zinapuliziwa dawa za kuua virusi kila mwisho wa safari
“Lakini wakati huo pia elimu juu ya kujikinga na virusi vya corona itolewe ndani ya vyombo vya usafiri kwa kutumia Redio na Runinga zilizopo kwenye vyombo hivyo,” alisema
Maagizo hayo pia yaliwagusa waendesha taxi, pikipiki za magurudumu mawili na matatu ambapo wametakiwa kuwa abiria wanapaka dawa ya kuua virusi mikononi (hand sanitizer) kabla ya kupanda kwenye chombo husika;
“Kamati ya pamoja iliyoundwa kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo haya na kufanya kaguzi mbalimbali ili kuhakikisha utekelezaji sahihi kwa wakati.”