Lipumba alivyojibu swali la mwanachama CUF aliyemtaja Magufuli

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema hajawahi kuwa mshauri wa Rais wa Tanzania, John Magufuli kuhusu masuala ya uchumi.

Tabora. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema hajawahi kuwa mshauri wa Rais wa Tanzania, John Magufuli kuhusu masuala ya uchumi.

Ametoa kauli hiyo jana Jumatano Oktoba 9, 2019 katika tarafa ya Usoki Wilaya ya Urambo katika ziara ya kuimarisha chama na kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Profesa Lipumba alieleza hayo baada ya kuulizwa swali na mwanachama wa CUF, Abdallah Kimani aliyedai kuwa kuna taarifa mwenyekiti huyo ni mshauri wa masuala ya uchumi wa Magufuli, ikiwa atapewa nafasi atasimamia vipi uchumi wa  wananchi.

Akijibu swali hilo Profesa Lipumba amesema hajawahi kuwa mshauri wa Rais huyo wa Awamu ya Tano, alikutana naye baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

"Tulikutana na kuzungumza na kati ya tuliyozungumza ni matatizo ya uchaguzi  wa Zanzibar.”

“Pamoja na mambo mengine nilimuomba kukutana na aliyekuwa katibu mkuu wangu (Maalim Seif Sharif Hamad- sasa amehamia ACT-Wazalendo) ambaye alikuwa mgombea urais Zanzibar alikubali na kukutana,” amesema Profesa Lipumba.

Ameongeza, “Hayo ndio mambo tuliyozungumza wakati ule wala mimi sio mshauri wa  Magufuli na hajawahi kuniomba kuwa mshauri wake.”