LIVE: Hatua kwa hatua maandamano Chadema Dar

Muktasari:

  • Maandamano ya Chadema yaliyoitishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe yameruhusiwa na Jeshi la Polisi kufanyika leo Januari 24, 2024 jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Maandamano yaliyoitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yameendelea kutikisa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam huku viongozi, wafuasi na wanachama wakishiriki.

đź”´#LIVE: Mbowe, Lissu waongoza maandamano Chadema

Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kufanyika kwa maandamano hayo leo Januari 24, 2024 akisema lengo ni kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni.

Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa yote ya mwaka 2023.

Lengo lingine la maandamano ni kuishinikiza Serikali kusikiliza maoni ya wananchi na kutaka itengeneze mpango wa dharura wa kukabiliana kwa kupanda gharama za maisha kwa Watanzania na mfumuko wa bei.

Alfajiri ya leo, Januari 24, 2024, wananchi walianza kujitokeza maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya maandamano huku wakiwa na mabango yenye ujumbe unaoelekezwa kwa viongozi wa Serikali.


Hali ilivyokuwa

Maandamano yalianzia Mbezi Luis, Kariakoo na Buguruni ambako wananchi wengi  walijitokeza wakiwa wamebeba mabango na kuimba nyimbo mbalimbali huku polisi wakiimarisha ulinzi katika maeneo hayo.

Katika Kituo cha Daladala cha Mbezi, baadhi ya wanawake waliibuka kwenye maandamano ya amani ya Chadema wakiwa wamevaa viroba (magunia) vyenye ujumbe tofauti.

Wanawake hao wanaofanya biashara ya kuokota chupa, wamesema wamebuni vazi hilo wakilenga kufikisha ujumbe kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Baadhi ya wanawake wameibuka kwenye maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia ya Maendeleo(Chadema) wakiwa wamevaa viroba (magunia) vyenye ujumbe tofauti.

“Tumevaa hivi kwa kuwa kitu rahisi kukipata kwa sasa ni kiroba, maisha yamekuwa juu na familia nyingi zinateseka tukiwamo sisi,” amesema mmoja wa wanawake hao.

Kwa nyakati tofauti wamesema wao sio wanachama wala wafuasi wa Chadema, lakini wanashiriki maandamano hayo kama wananchi wa kawaida kutokana na kuvutiwa na ajenda za Chadema kwenye maandamano hayo.

Mbowe, Kigaila, Lema watinga Buguruni maandamano Chadema

Maandamano hayo ya amani yanayoanzia Stendi ya Daladala ya Mbezi Luis yanaelekea ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) hapa nchini.

Huko Kariakoo, Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi njiani kuelekea Barabara ya Morogoro, Shekilango, Igesa - Sinza na kuishia Barabara ya Sam Nujoma ofisi za UN.

Maandamano hayo yameanzia Buguruni kupitia Karume – Kariakoo kisha Barabara ya Morogoro kuelekea Barabara ya Sam Nujoma.

Mwananchi  Digital imeshuhudia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa wamesimama kwa makundi wakiimarisha ulinzi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekutana na wafuasi na wanachama wa Chadema na kuwapa salamu za kubariki maandamano hayo akidai ni za Rais Samia Suluhu Hassan.

Chalamila anayeongoza shughuli za usafi jijini Dar es Salaam, leo asubuhi aliwasili eneo la Mbezi Luis ambako maandamano ya chama hicho cha upinzani yalianzia.

Akiwa katika eneo hilo, Chalamaila amewataka wafuasi na wanachama wa Chadema waendelee kuandamana na kufikisha ujumbe wao.

Pia, amesema wakati Chadema wakiendekea na maandamano, yeye na watu wake wanaendelea na usafi, akisisitiza Rais Samia ameyabariki maandamano hayo na kila mmoja anapaswa kulinda amani.

“Nawapa salamu za Rais, ninyi endeleeni kuandamana na sisi tunaendelea na usafi,” amesema Chalamila huku akishangiliwa na wafuasi na wanachama wa chama hicho waliokuwa wakiimba, kucheza na kupiga makofi  huku baadhi ya nyimbo wakimtaja Rais Samia  na sukari bei juu.

Saa nne asubuhi leo, Mbowe aliwasili Buguruni na kuanza maandamano hayo kuelekea ofisi za UN.

Katika maandamano hayo, Mbowe aliambatana na watoto wake watatu huku akitoa ujumbe kwamba maandamano hayo hayatakoma na yatasambaa nchi nzima.

“Tunataka miswada iondolewe bungeni na tupate mwafaka wa kitaifa ili miswada hiyo itakaporejeshwa bungeni itibu matatizo yaliyosababisha uvunjifu mkubwa wa haki mwaka 2020 na chaguzi zote za marudio yaliyowahi kufanyika,” amesema Mbowe.


Chadema Kilimanjaro

Viongozi, wanachama na baadhi ya wafuasi wa Chadema, Mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na mwenyekiti wake, Michael Kilawila, wamesafiri usiku ili kushiriki maandamano ya amani yaliyoandaliwa na chama hicho jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema  amesema ukimtoa yeye na Kilawila, yumo pia mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Grace Kiwelu, wajumbe wa kamati ya utendaji ya mkoa huo na wilaya zake.

Amesema kwa takwimu za awali waliosafiri usiku ambao tayari wamewasili Dar es Salaam alfajiri ya leo Januari 24, 2024, ni zaidi ya watu  60.

Chadema Kilimanjaro wanogesha maandamano Dar, Katibu wa mkoa, Basil Lema afunguka kila kitu

Lema amesema baada ya Dar es Salam, wanajipanga kufanya maandamano makubwa mikoa ya kanda ya kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara na wataanzia jijini Arusha.


Mbeya nao wajiunga

Wakati Chadema ikiendelea na maandamano ya amani leo, baadhi ya viongozi wa chama hicho kutoka Mkoa wa Mbeya, wamejumuika na wenzao wa Dar es Salaam kuongeza nguvu.

Akizungumza kwa simu leo akiwa jijini Mbeya, mwenyekiti wa chama hicho mkoa  humo, Joseph Mwasote amesema wamejumuika pamoja ili kufikisha ujumbe waliokusudia kwa watawala.

Mwasote amesema jambo hilo ni la Watanzania wote, hivyo wameamua kushiriki na wenzao wa Dar es Salaam na wakirejea Mbeya watapanga ratiba ya lini watafanya maandamano.

“Hata mimi nilipaswa kuwapo Dar es Salaam leo kwa sababu tayari nilikuwa nimeshaanza safari jana, lakini kutokana na changamoto za kifamilia ilinilazimu nigeuze lakini wenzangu wameendelea na safari na tayari wapo huko,” amesema Mwasote.

Hata hivyo, amesema viongozi wa juu bado hawajatoa maelekezo yoyote akibainisha baada ya kumaliza Dar es Salaam, wanasubiri utaratibu akisisitiza kuwa Mbeya wapo tayari.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa kwa sasa Mbeya wapo kwenye operesheni maalumu ya uchaguzi kuanzia ngazi msingi, kata, wilaya na mkoa yenye mkakati wa kujipanga kupata viongozi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Wanaoshiriki uchaguzi huu lazima wawe wanachama waliojisajili kidigitali kama inavyotakiwa kwa sasa, hii tunaamini kwa mwitikio ulivyo, chaguzi zote mwaka huu Chadema itapasua kila eneo,” amesema Mwasote.