LSF yabadili mfumo wa utoaji ruzuku kwa ZMOs
Muktasari:
- Kipitia kikao cha siku mbili cha LSF na wasaidizi wa sheria, wamemepitia maandiko mradi, mipango kazi pamoja na bajeti za mashirika simamizi kwa ajili ya kuangalia upya shughuli zilizopangwa ikiwa zinaakisi malengo ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki nchini.
Dar es Salaam. Shirika la Legal Services Facility (LSF) limefanya mabadiliko ya utoaji wa ruzuku kwa wasaidizi wa kisheria (ZMOs), ili kuongeza ufanisi zaidi.
Hayo yameelezwa jana Februari 9 katika kikao kazi cha pamoja na mashirika yatakayosimamia mashirika takribani 92 ya katika kanda sita nchini ili kuongeza ubora katika kutoa huduma za msaada wa kisheria katika jamii.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho, Meneja Programu LSF, Wakili Deogratias Bwire, amesema kupitia kikao hicho wamewajenga uelewa wa pamoja wasimamizi hao kwa ajili ya kuonyesha uelekeo mzuri wa utekelezaji programu ya upatikanaji haki nchini.
“Awali, LSF ilikuwa na mfumo wa kutoa ruzuku kwa mashirika ya wasaidizi wa kisheria kupitia mashirika simamizi katika mikoa, lakini baadaye iliamua kutoa ruzuku moja kwa moja na sasa tumeamua kuwa na usimamizi wa kikanda ili kuongeza ufanisi zaidi,” ameeleza Meneja Programu.
Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi na Matokeo LSF, Said Chitung amesema kuwa kikao hicho kinalenga kuongeza usimamizi wa programu kwa kujenga uwezo kwa mashirika ya msaada wa kisheria ambayo ZMOs watayasimamia katika kanda zao.
“ZMOs hawa kazi yao kubwa ni kufanya usimamizi wa programu ya LSF katika mikoa ambayo watakwenda kuisimamia kulingana na kanda zao tulizowapa,” amesema Chitung.
Naye Ofisa fedha kutoka Shirika la Morogoro Paralegal Centre (MPLC), Regina Solomon ameeleza kuwa kikao kimesaidia kujenga uelewa wa pamoja katika utoaji wa taarifa (reporting) zenye matokeo kuhusu utekelezaji wa mradi katika maeneo ambayo ZMOs atakwenda kuyasimamia chini ya ufadhili wa Legal Services Facility.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Centre for Widows and Children Assistance (CWCA), Wakili Jane Kapufi amesema taasisi yake ambayo imechaguliwa kusimamia mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga watahakikisha mashirika ya msaada wa kisheria yanakuwa hai zaidi kiutendaji.
Kikao kazi hicho cha pamoja kimeandaliwa na LSF kwa siku mbili kuanzia 09-10 Februari 2023 Jijini Dar es Salaam, ambapo mashirika simamizi (ZMOs), waratibu wa kanda wa programu na usimamizi wa ruzuku LSF (LSF zonal Coordinators) kwa pamoja watashirikiana na secretarieti ya LSF kujenga uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki kupitia usimamizi wa kanda.