Ma-RC waja na vipaumbele

Ma-RC waja na vipaumbele

Muktasari:

Siku chache baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa mikoa, viongozi hao wameanza kuripoti maeneo yao ya kazi huku wakibainisha vipaumbele vyao.

Mikoani. Siku chache baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa mikoa, viongozi hao wameanza kuripoti maeneo yao ya kazi huku wakibainisha vipaumbele vyao.

Baadhi ya walioripoti ni Adam Malima (Mwanza), Rosemary Senyamule (Dodoma), Kanali Ahmed Abass Ahmed (Mtwara), Anthony Mtaka (Simiyu) na Nurdin Babu wa Kilimanjaro.

Wakuu hao wa mikoa ni miongoni mwa walioapishwa Jumatatu hii Ikulu jijini Dar es Salaam na wengine kuhamishwa vituo vya kazi.

Kwa upande wa Malima, ametoka Tanga, Mtaka (Dodoma), Rosemary (Geita) huku Kanali Ahmed akipandishwa kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Pwani.

Jana, Rosemary baada ya kukabidhiwa ofisi na Mtaka alivitaja vipaumbele vyake kuwa ni utunzaji wa mazingira, kuinua uchumi na Taifa.

“Kitu ambacho nimesikia wananchi wakiniambia kabla sijafika, ni migogoro ya ardhi na maji, lakini kwa mji wa Dodoma. Ninaweza kuwa na vipaumbele vyangu maana huko kote nilikokwenda nimekuwa nikifanya mambo ya mazingira na uchumi,” alisema Rosemary.

“Nimekuwa mwalimu wa kufundisha na kufanya watu wabadilike, sasa ni obvious nikienda kokote huko lazima niyafanye, lakini kwa Dodoma vipaumbele vyangu vitategemea pia vipaumbele vya Taifa, kwa maana ya sura ya Dodoma ya makao makuu,” alisema.

Akikabidhi ofisi hiyo, Mtaka alisema bado ndoto yake katika mkoa anaoongoza ni kuhakikisha unakuwa katika tarakimu moja katika matokeo ya mitihani ya Taifa.

Mtaka alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja kimekuwa ni elimu na uchumi unaohusu watu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk Fatuma Mganga alisema migogoro ya ardhi imekuwa ikisumbua Dodoma, Mtaka alianza kushughulikia lakini haijaimalizia.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, Halmashauri ya Dodoma Mji inaongoza nchini kwa kuwa na migogoro mingi ya ardhi.

Katika Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed aliwataka watumishi wa ofisi ya mkoa kuzidi kutoa huduma kwa wananchi kwa sababu ndiyo dhamana waliyopewa.

Mambo mengine ni kukusanya mapato kwa kadiri ya uwezo wao na kuhakikisha wananchi wanahesabiwa ifikapo Agosti 23, mwaka huu.

Kanali Ahmed alisema yale yote yaliyoanzishwa na Meja Jenerali Marco Gaguti anayachukua kama sehemu ya kuanzia kazi zake.

“Jambo kubwa ninaloweza kuwaahidi ni utumishi uliotukuka na kuyaenzi waliyoyaanzisha na mengine ambayo Mwenyezi Mungu atanipa utukufu wa kuyaanzisha basi nitayaenzi,” alisema Kanali Ahmed.

Kwa mwaka mmoja na miezi miwili ambao Gaguti alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara atakumbukwa kwa kuanzisha utoaji wa zawadi ya magari, pikipiki, baiskeli na fedha taslimu kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri.

“Tamaa yangu baada ya kukaa mwaka mmoja na miezi miwili hapa, nitakapokuja tena Mtwara, nikute maendeleo ya mkoa kwa kasi kubwa katika yale ambayo tulifikiria na mengine mengi zaidi,” alisema Gaguti wakati akiaga.

“Huwa napata tabu sana kuaga hata sijui nianzie wapi, lakini yote ni mambo ya shukrani, leo nitatoa shukani tu, Juni 26, 2019 nilichaguliwa kuwa mkuu wa wilaya ya mkoani Kigoma na baadaye Kagera, kisha Mtwara Juni 2021,” alisema Gaguti.

Wakati Babu akitua Kilimanjaro na kupokewa na watumishi mbalimbali wa mkoa huo alisema, “nawashukuru kwa kunipokea, mmenionyesha upendo na ushirikiano mkubwa, Mungu awabariki sana, tutaendelea kushirikiana pamoja.”

Mkoani Mwanza, Malima alikabidhiwa ofisi huku Robert Gabriel akibainisha vipaumbele saba ambavyo ni kuongeza ukusanyaji wa mapato, uboreshaji wa huduma za kijamii na Mwanza kupata timu inayoshiriki Ligi Kuu.

Vingine ni kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma na kuimarisha ulinzi na usalama wa mkoa huo.

Pia, alisema atasimamia utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo na kufanya tathmini ya hali ya huduma za jamii, ikiwemo afya, elimu, maji, miundombinu na miradi ya umeme.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila aliahidi kutekeleza kauli ya Serikali ya kuinua uchumi wa mkoa huo kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi.

Chalamila alisema hayo katika makabidhiano ya ofisi hiyo baina yake na mkuu wa mkoa aliyekuwepo, Meja Generali Charles Mbuge.

“Nitapitia kabrasha la mkoa nijue niko wapi, natoka wapi na nakwenda wapi; naomba Wanakagera waniunge mkono,” alisema Chalamila.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge alikabidhi majukumu matatu ya kitaifa kwa mkuu wa mkoa huo ili aweze kuyasimamia na kuyafanyia kazi, ikiwamo sensa, kilele cha mbio za mwenge pamoja na mradi wa bomba la mafuta. Katibu tawala wa mkoa wa Kagera, Toba Nguvila aliahidi kumpa ushirikiano Chalamila.

Imeandikwa na Sharon Sauwa (Dodoma), Mwanamkasi Jumbe (Mtwara), Janeth Joseph (Kilimanjaro), Mgongo Kaitira (Mwanza) na Alodia Dominic (Kagera).